Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kukamata madawa ya kulevya aina ya mirungi viroba 202 viliyokuwa vinasafirishwa kuingia nchini vikitokea nchi jirani ya Kenya (Picha na Rashid Nchimbi wa jeshi la Polisi Arusha).
Askari wa Jeshi la Polisi wakiharibu madawa ya kulevya aina ya mirungi kwa kukata kata na kumwagia mafuta. Madawa hayo yalikamatwa saa 1:00 asubuhi leo eneo la Engikareti lililopo wilaya ya Longido Mkoani hapa.(Picha na Rashid Nchimbi wa jeshi la Polisi Arusha)
Na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa
limewakamata watu wanne wakiwa na madawa ya kulevya aina ya mirungi. Watu hao
walikuwa na jumla ya viroba 202 vya madawa hayo ambayo yalikuwa kwenye gari
aina ya Mitsubishi Canter lenye namba za usajili T 306 BUN.
Akizungumza na waaandishi wa habari
nje ya jengo la Makao Makuu ya Jeshi hilo Mkoani hapa, Kamanda wa Polisi Mkoani
hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas aliwataja watuhumiwa hao
kuwa ni Joel Alfayo Lukumay (37), Rahim Azizi Gilla (35), Ibrahimu Solomon
Katambwei (40) na Musa Lazaro Mollel (38) wote ni wakazi wa Mkoa wa Arusha.
Alisema tukio hilo lilitokea leo saa
1:00 asubuhi katika eneo la Engikareti lililopo wilayani Longido mkoani hapa.
Aliongeza kwa kusema kwamba, mafanikio hayo yametokana na taarifa toka kwa raia
wema ambao waliwasiliana na jeshi hilo, ambapo mara baada ya kupata taarifa
hiyo waliweka mtego katika eneo hilo na kufanikiwa kulikamata gari hilo ambalo
lilikuwa linatokea nchi jirani ya Kenya.
Kamanda Sabas aliwashukuru wananchi
wa Mkoa wa Arusha kwa ushirikiano wao
mkubwa unaofanywa kwa jeshi hilo na kuwaomba waendelee kutoa taarifa za
uhalifu na wahalifu kwani kama wananchi wakiamua uhalifu unaweza ukapungua kwa
kiasi kikubwa.
Baadhi ya waaandishi na askari
waliokuwa kwenye eneo hilo walishuhudia viroba hivyo vikiwa na majina ya watu
pamoja na uzito wa kila mzigo huku wengine wakidai kwamba inawezekana gari hilo
huwa linabeba mizigo ya watu mbalimbali ambao wanakuja kugawana mara baada ya
kuingia Arusha Mjini.
Kutokana na tukio hilo Jeshi la
Polisi Mkoani hapa linaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na pindi upelelezi
utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili. Aidha
taarifa za ndani ya jeshi hilo zinasema kwamba gari hilo lilishawahi kukamatwa
tarehe 16 mwezi Machi mwaka jana ambalo lilikutwa na madawa ya aina hiyo na
kesi yake ilikwishafikishwa mahakamani na bado shauri hilo bado linaendelea.
No comments:
Post a Comment