Baadhi ya
vitu vya marehemu Sharo milionea vilivyokamatwa baada ya msako mkali
baina ya Polisi na wananchi wa Kijiji Songa Kibaoni.
Na Mashaka Mhando,Tanga
WATU
wanaosadikiwa kuiba vitu vya marehemu Hussein Mkiety maarufu kwa jina la
'Sharo Milionea' aliyefariki kwa ajali ya gari katika kijiji cha Songa
Kibaoni wilayani Muheza Novemba 26 mwaka huu, wamesalimisha baadhi ya
vitu hivyo kwa mwenyekiti wa Kijiji hicho huku wakiendelea kuishi
mafichoni kuogopa kutiwa mbaroni.
Watu hao
wamesalimisha vitu hivyo baada ya Mkuu wa wilaya ya Muheza Subira Mgalu
ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama kuwatangazia kwamba
wale wote waliomwibia marehemu watasakwa na kuchukuliwa hatua za
kisheria kufutia kitendo walichokifanya kutokuwa cha kiungwana.
Mkuu huyo
pamoja na jeshi la polisi wilayani humo waliendesha msako juzi usiku
lakini hawakuweza kuwakuta watu baada ya kuzihama nyumba zao kuogopa
kutiwa mbaroni na mkuu huyo kuwalazimsha baadhi ya familia walizozikuta
kuendesha zoezi la kuwataja watu wanaohofiwa kwamba huenda watakuwa
wamchukua vitu hivyo.
Kamanda
wa polisi mkoani Tanga ACP Constatine Masawe, aliwaeleza waandishi wa
habari ofisini kwake kuwa, usiku wa kuamkia juzi mwenyekiti wa kijiji
hicho Abdi Zawadi alipelekewa vifaa mbalimbali ikiwemo nguo ambazo
marehemu alikuwa amezivaa pamoja na spea tairi ambalo waliling'oa na
kutokomea porini.
Kamanda
huyo alitaja vitu vilivyokabidhiwa kwa mwenyekiti huyo kuwa ni pamoja na
begi lake lililokuwa na 'viwaro' nguo zake, betri ya gari hilo
lililokuwa na namba T 478 BVR aina ya Toyota Harrier, saa yake ya
mkononi, simu yake aina ya Blackberry na redio ya gari iliyokuwa pia
imeng'olewa na wezi hao.
Kamanda
huyo alisema vitu hivyo vilipelekwa na mtu mmoja ambaye kwasasa jeshi
hilo linashindwa kumtaja jina lake kwa vile alijitambulisha kwamba ana
undugu na wezi hao ambao walimpa vitu hivyo avipeleke kwa uongozi wa
kijiji hicho hatua ambayo alidai kwamba wanafanya uchunguzi ili kuwatia
nguvuni wale wote waliohusika na tukio hilo.
Alisema
waliweka mtego baada ya kusikia kwamba kuna mwizi mmoja wapo anaitafutia
mteja simu ya mkononi ya marehemu lakini wakati wameweka mtego huo
kijana huyo alipokuwa akijadiliana bei na mtu waliyemweka, alibaini na
alipompa mkononi alikimbia vichakani kuogopa kukamatwa.
Kamanda
huyo aliwashukuru baadhi ya wananchi wa kijiji hicho pamoja na Mkuu wa
wilaya kuhakikisha wanashirikiana na jeshi hilo ili kuwabaini na
kuwakamata wote waliohusika katika tukio hilo ambalo limetokea huku
wananchi kadhaa wakiomboleza kifo cha msanii huyo ambaye alizikwa
kijijini kwao Lusanga wilayani Muheza juzi.
Katika
hatua nyingine kamanda huyo alisema katika matukio ya ajali yaliyotokea
mwezi huu wa Novemba jumla ya ajali 10 zilitokea ambazo zimesababisha
vifo ni 7 na zilizosababisha watu kujeruhiwa ni tatu, kati ya hizo watu
12 walipoteza maisha na wengine wanane walijeruhiwa.
Kamanda
Masawe alisema jumla ya makosa 2,365 yalitendeka na kupigwa faini
iliyosababisha serikali kujiingiza kiasi cha sh. 70,950,000 hatua ambayo
kamnada huyo alisema haioneshi kwamba watumiaji barabara wamekuwa
wakifuata, wakitii sheria za usalama barabarani.
No comments:
Post a Comment