Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MSIBA wa msanii nyota wa uchekeshaji
hapa nchini, Hussein Mkiety, maarufu kama 'Sharomilionea' umegusa
hisia za wengi, huku King Majuto akikimbizwa Hospitali baada ya
kushikwa na presha, hivyo kutishia usalama wake.
Mtoto wa King Majuto, Hamza Majuto,
aliimbia HANDENI KWETU kuwa hali ya baba yake inaendelea vizuri
kutokana na kuumizwa zaidi na msiba wa Sharomlionea anayetamba katika
ulingo wa filamu na muziki hapa nchini.
Msanii huyo alikufa jana saa mbili za
usiku Maguzoni, kilimita chache na kijijini kwao Lusanga, wilayani
Muheza mkoani Tanga, baada ya gari lake alilokuwa akisafiria lenye
namba za usajili T478 BVR Toyota Harrier kupinduka na kusababisha
kifo chake.
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga,
Constantine Masawe, alikiri kutokea kwa msiba huo na kusema kuwa
mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Teule, Muheza, mkoani
Tanga kwa taratibu za mazishi zinazopangwa na familia yake.
“Marehemu alikufa majira ya saa mbili
za usiku kwenye barabara ya Segera alipokuwa anatoka Dar es Salaam
kwenda Muheza, hivyo mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya
Teule, huku gari lake likihifadhiwa pia kwasababu haliwezi kutembea,”
alisema Masawe.
Taarifa za kifo cha msanii huyo
aliyeibukia hivi karibuni na kufanya vema katika ulingo huo zilianza
kuzagaa saa tatu za usiku, ikiwa ni dakika chache baada ya kufariki
katika ajali hiyo ya kusikitisha kwa nyota huyo.
Katika mitandao yote ya kijamii kuanzia
saa tatu za usiku zilizagaa habari zake, huku kila mmoja kiwa na
hisia tofauti zilizotokana na madai ya kifo cha msanii huyo, ambaye
baadaye jeshi la Polisi lilithibitisha kwa kupitia Kamanda wake,
Masawe.
Sharomilionea ameshacheza filamu nyingi
za uchekeshaji na kujipatia sifa kubwa, ikiwamo ile ya Sharo
Millionea, Imekula Kwako, Jini Mahaba, Porojo na nyinginezo
zinazofanya vyema katika tasnia ya filamu nchini.
Katika filamu ya Jini Mahaba,
Sharomillionea anayetamba pia kwa msemo wake wa ‘Umebug Men’,
anacheza kama mtu maarufu anayekwenda kujitambulisha kwa wake zake
(Kingwendu) na kushangazwa na hali zao za maisha.
Sharomillionea anamshangaa mama yake
mkwe anavyochambua mboga za majani wakati yeye sio utaratibu katika
maisha yake. “Huyu ndio mama yako Men? Mbona anachambua majani,”
aliuliza huku anakunja mdomo wake na kujifuta uso.
Maneno hayo yanamuumiza mama yake mkwe
na kuamua kumuita mume wake (Kingwendu) na kuja kushangaa Sharobalo
alivyokuwa katika mueneko wa super Star na kujikuta akipagawa
alipoanza kukejeliwa na mkwe wake.
Mbali na filamu hiyo ya Jini Mahaba,
mkali huyo pia ametamba katika filamu nyingi pamoja na nyimbo mbili
alizorekodi, huku pia akililiwa na wasanii wenzake kutokana na
ushirikiano wake, mara baada ya kuibuka kisanii.
Wasanii wengi waliozungumzia kifo cha
Sharomillionea wakiongozwa na Steve Nyerere, walionyeshwa
kuchanganyikiwa kwa msiba wa msanii aliyeanza kutokea peupe na
kutamba mno katika sanaa ya uchekeshaji.
Sharomillionea aliyetokea katika ubavu
wa nguli wa vichekesho nchini, King Majuto, anazikwa kesho Jumatano,
kijijini kwao Lusanga, huku wasanii wengi wakitarajia kuhudhuria
msiba na mazishi ya nyota huyo aliyeipenda pia nyumbani kwao Muheza.
|
KAPINGA ATANGAZA FURSA ZA UWEKEZAJI NISHATI NCHINI SAUDI ARABIA
-
*📍Saudi Arabia*
*Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Kongamano la
Wafanyabiashara na Wawekezaji nchini Saudi Arabia litaongeza uwe...
1 hour ago
No comments:
Post a Comment