Mazungumzo ya dharura yanafanywa kutwa leo, kuhusu madeni ya Ulaya na Marekani, ili kutuliza masoko ya fedha kabla hayakufunguliwa Jumatatu.
Macho sasa yako juu ya Ulaya baada ya madeni ya Marekani kutajwa kuwa yamepungua hadhi.
Kuna wasiwasi kuwa msukosuko sasa utaikumba Utaliana.
Linalosumbua mabenki kwa sasa ni madeni ya Utaliana, yaani kiwango cha riba ambacho Utaliana inabidi kulipa ili kuweza kukopa, sambamba na kupungua kwa thamani ya madeni hayo.
Na mabenki yanaona kuwa Benki Kuu ya Ulaya, (ECB), inaweza kuingilia kati kurejesha imani tena ili gharama za mkopo kwa Utaliana zisipande mno.
Mabenki yanataka ECB inunue madeni ya Utaliana, kama ilivonunua mikopo ya Jamhuri ya Ireland, Ureno na Ugiriki siku za nyuma.
Endapo Benki Kuu hiyo ya Ulaya, ECB, haikufanya hivo kesho, Jumatatu, kuna uwezekano kuwa masoko ya fedha yatatibuka tena.
Na ndio maana mkutano wa dharura unaofanywa leo wa halmashauri kuu ya ECB ukaonekana kuwa muhimu sana, kwa sababu baadhi ya wajumbe wa halmashauri wanapinga kununua madeni ya Utaliana.
No comments:
Post a Comment