Teknolojia : Msigwa Aipongeza TCRA kwa Kuwalea Mabloga (TBN) na Waandishi wa Mtandaoni - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Thursday, 18 December 2025

Teknolojia : Msigwa Aipongeza TCRA kwa Kuwalea Mabloga (TBN) na Waandishi wa Mtandaoni


Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kulea na kuwawezesha waandishi wa habari wa mitandaoni na mabloga, badala ya kuwashughulikia kwa mtazamo wa adhabu, ili kujenga tasnia imara na yenye tija ya habari nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, aliipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa mwelekeo wake wa kulea wadau wa sekta ya habari badala ya kuchukua hatua kali za kinidhamu.

Msigwa alisema mwelekeo huo unaendana na falsafa ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo inalenga kushirikiana na wadau mbalimbali kwa manufaa ya taifa.

Aliitaja Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA) kuwa ni wadau wakubwa wa serikali katika tasnia ya habari, akisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika kusambaza taarifa na kujenga mawasiliano kati ya serikali na wananchi.

“Serikali imewaamini waandishi wa mitandaoni, sasa nanyi muendelee kuonesha imani kwa serikali. Ushirikiano wetu umeendelea kuimarika na changamoto zinazojitokeza tunazitatua kwa pamoja,” alisema Msigwa.

Akikanusha madai kuwa waandishi wa habari wa mitandaoni ni dhaifu, Msigwa alisema wanatekeleza wajibu wao ipasavyo na wana nafasi kubwa ya kutumia kalamu zao kujenga taifa.

“Nimekuwa nikisisitiza waandishi tutumie kalamu zetu kujenga nchi. Mnafanya kazi sahihi na mnalinda maslahi ya taifa,” aliongeza.

Msigwa aliwahakikishia waandishi ulinzi wa serikali, akisema endapo sheria, kanuni au sera zitabainika kuwa kikwazo katika utendaji wao, zitafanyiwa marekebisho kwa maslahi mapana ya taifa.

Alitangaza pia kuanza kwa maandalizi ya mafunzo kwa waandishi wa habari kwa kushirikiana na TCRA, akiwataka kuyapokea kwa mtazamo chanya kama sehemu ya kuongeza weledi na taaluma.

Kuhusu masuala ya kodi, Msigwa alisema serikali itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutatua changamoto zinazowakabili waandishi wa mitandaoni, akitambua mchango wao katika kuitangaza nchi na kuvutia uwekezaji.

Aidha, alieleza kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ipo katika mchakato wa kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kuwawezesha waandishi wa habari, hususan wa mitandaoni.

Akizungumzia mazingira ya sasa ya kimataifa, Msigwa alisema vita vya dunia ya sasa vimehama kutoka silaha za kijeshi kwenda kwenye taarifa, akisisitiza kuwa vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kulinda na kuipromote nchi.

Aliwahimiza waandishi kuhakikisha majukwaa yao yanatumika kulinda maslahi ya taifa na kuonya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao yanayoweza kuharibu taswira ya Tanzania.

Hata hivyo, Msigwa alionesha kusikitishwa na tabia ya baadhi ya waandishi kunyamaza wanapodhalilishwa, akiwataka kusimama na kulinda hadhi ya taaluma yao.








No comments:

Post a Comment