Matukio : Mkurugenzi Mkazi wa USAID bwana Andy Karas atembelea walengwa wa TASAF mkoani Iringa. - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


20 Nov 2017

Matukio : Mkurugenzi Mkazi wa USAID bwana Andy Karas atembelea walengwa wa TASAF mkoani Iringa.


Na Estom Sanga – Iringa

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani –USAID-bwana Andy Karas amepongeza jitihada za serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF katika kuwafikia wananchi wanaokabiliwa na umasikini kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ambao umeanza kuonyesha mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali nchini, jambo linalovutia wadau wa maendeleo kuendelea kusaidia jitihada hizo.

Bwana Karas ameyasema hayo alipokutana na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika kijiji cha Igingilanyi kata ya Nduli katika halmashauri ya Wilaya ya Iringa ,mkoani Iringa ambako licha ya kuelezwa namna TASAF inavyoendelea kutekeleza Mpango huo, lakini pia alishuhudia namna walengwa wa mpango huo walivyoboresha maisha yao kwa kutumia fedha za ruzuku za mfuko huo.

Amesema hamasa inayoonyeshwa na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika kujiletea maendeleo kwa kuanzisha miradi midogo midogo kwa kutumia fedha zinazotolewa na Serikali kupitia TASAF, imelivutia Shirika hilo na kuahidi kuwa litaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuboresha utaratibu wa kuwainua wananchi kiuchumi .

Bwana Karas amesema utaratibu wa kuwafikia na kuwasaidia moja kwa moja wananchi wanaoishi katika mazingira magumu ya kiuchumi umekuwa ukitumika katika nchi nyingi duniani na umeonyesha mafanikio makubwa kwa kusisimua shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kaya masikini .

Aidha Mkurugenzi Mkazi huyo wa USAID amevutiwa na masharti ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia TASAF hususani katika nyanja za elimu, afya, lishe na uwekezaji kwenye shughuli za kiuchumi kwa walengwa wa Mpango huo kuwa umeamusha ari ya kutokomeza umasikini miongoni mwao.

Akiwa katika kijiji hicho cha Igingilanyi kata ya Nduli bwana Karas alitembelea baadhi ya kaya za Walengwa wa TASAF na kujionea namna walivyonufaika na ruzuku ya Mpango huo kwa kuanzisha miradi midogo midogo ya ufugaji wa kuku na nguruwe na kutumia sehemu ya mapato yao kuboresha makazi kwa kujenga nyumba za matofali na kuezeka kwa mabati.

“ni jambo jema sana mnalolifanya kwa kuwekeza katika elimu ya watoto wenu na kuboresha makazi yenu kwa kutumia ruzuku mnayoipata” alisisitiza bwana Karas.

Bwana Karas pia alionyesha kuvutiwa na utaratibu wa kuanzisha vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana unaofanywa na Walengwa wa Mpango huo wa Kunusuru Kaya Maskini ambao alisema ukiimarishwa utatoa fursa kubwa zaidi kwa wananchi hao kukuza shughuli zao za kiuchumi kwa kukopeshana kwa riba ndogo ikilinganisha na ile inayotozwa na taasisi za kibenki.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Miradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF,Bwana Amadeus Kamagenge alimweleza Mkurugenzi Mkazi huyo wa USAID kuwa licha ya Serikali kupitia Mfuko huo kuendelea kutoa ruzuku kwa Kaya Masikini sana katika mikoa yote nchni ,hivi sasa umeanza kujikita zaidi katika kuhamasisha walengwa kuanzisha vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana kwa kuwatumia wataalamu walioko kwenye maeneo yao wakiwemo Maafisa wa Maendeleo ya Jamii, kilimo, Mifugo na biashara ili waweze kuboresha shughuli za kiuchumi kwa walengwa.

“Mkakati huo umeanza kuonyesha mafanikio kwa kuwaongezea walengwa kwa Mpango huo kipato na kuwapa uwezo wa kubuni na kusimamia kwa ufanisi miradi yao midogo midogo wanayoianzisha.

Hata hivyo bwana Kamagenge amesema mafanikio yaliyoanza kupatikana kwa kaya za walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini yameibua kilio kutoka kwa kaya nyingine ambazo hazikuingizwa kuingizwa kwenye Mpango huo kutaka nazo pia zijumuishwe kwenye utaratibu huo. Hadi sasa TASAF inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika vijiji 9,835 ambayo ni sawa na asilimia 70 ya vijiji na shehia zote Tanzania bara na Zanzibar.

Mkurugenzi M kazi wa Shirika la Misaada la Marekani –USAID-bwana Andy Karas (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na mmoja wa walenwa wa TASAF katika kijiji cha Igingilanyi kata ya Nduli wilaya ya Iringa baada ya kutembelea nyumba aliyoijenga mlengwa huyo (nyuma yao ) baada ya kupata ruzuku kutoka TASAF.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Misaada la Marekani USAID bwana Andy Karas akipokea zawadi ya kuku kutoka kwa mmoja wa walengwa wa Mpango wa kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na TASAF katika kijiji cha Igingilanyi wilaya ya Iringa Vijijini ambako akutana na walengwa wa Mpango huo kuona namna wanavyonufaika na Mpango huo.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Misaada la Marekani nchini USAID bwana Andy Karas akisoma taarifa kwenye mkutano wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika kijiji cha Igingilanyi kata ya Nduli wilaya ya Iringa Vijijini ambako alitembelea kuona namna walengwa wa Mpango huo wanavyonufaika na ruzuku inayotolewa na serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF.
Baadhi ya Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika kijiji cha Igingilanyi wilaya ya Iringa Vijijini wakiwaburudisha wageni kutoka Shirika la Misaada la Marekani –USAID waliotembelea kijiji hicho kuona shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na TASAF .
Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Misaada la Marekani Bwana Andy Karas akisalimiana na mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika kijiji cha Igingilanyi kata ya Nduli wilaya ya Iringa Vijijini wakati alipotembelea kijiji hicho.Katikati yao ni Mkurugenzi wa miradi wa TASAF bwana Amadeus Kamagenge.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad