Matukio : Kamati ya Kudumu ya Bunge Yatembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) tawi la Mbeya - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Wednesday, 22 March 2017

Matukio : Kamati ya Kudumu ya Bunge Yatembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) tawi la Mbeya



Na mwandishi wetu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe Angellah Kairuki amesema kwamba serikali itahakikisha kwamba Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) tawi la Mbeya kinakuwa na majengo yake ili kupunguza gharama za uendeshaji.
Kwa sasa chuo hicho kinatumia majengo ya kukodi ambayo ni mali ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya,majengo hayo yapo eneo la soko Matola, Chuo kinahudumia wakazi wa Nyanda za Juu Kusini.
Akiwasilisha taarifa ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania tawi la Mbeya mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala na Serikali za Mitaa Waziri Kairuki alisema gharama ya kodi ya shilingi milioni 24 kwa mwezi ni kubwa na kwamba serikali iko katika mchakato wa kuhakikisha kwamba chuo hicho kinamilikishwa mjengo hayo ili kupunguza gharama za uendeshaji.
Aidha Waziri huyo alisema kwamba serikali itahakikisha kwamba chuo kinakuwa na wakufunzi wa kutosha ili kuendesha kozi zake kwa ufanisi.
Mkuu wa TPSC Dk.Henry Mambo aliiambia kamati hiyo kuwa tawi la Mbeya linakua kwa kasi kwani kwa sasa lina wanafunzi 1236, tawi hilo lilizinduliwa mwaka 2014 likiwa na wanafunzi 453.
“Tawi linakuwa kwa kasi na sisi kama chuo tunaziona changamoto za kukua kwa chuo na tunajitahidi kukabiliana nazo, baadhi ya changamoto hizo ni mahitaji ya miundombinu ya kufundishia,”
Alisema pamoja na changamoto hizo, serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba chuo kinafanya kazi zake kwa ufanisi na kutoa elimu kwa watumishi wa umma na watumishi wa umma wa tarajiwa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala na Serikali za Mitaa Josson Rweikiza alikipongeza chuo hicho na kusema kuwa kina mchango mkubwa kwa maendeleo ta taifa hili.
“Changamoto ni muhimu katika uhai wa kila kitu, kama hakuna changamoto basi hakuna maisha, tunawapongeza na kuwatia moyo katika kutekeleza majukumu yenu,” alisema.


Awali Waziri Kairuki alisema kuwa TPSC hutoa ushauri wa kitaalam kwa Wizara, Idara, Wakala za Serikali , Mamlaka za Serikali za Mitaa na sekta binafsi.
Baadhi ya shauri hizo za kitaalam ni katika maeneo ya miundo na mifumo ya utumishi , mpango mkakati ,Mkataba wa huduma kwa mteja , tathmini na uchambuzi kazi , tathmini ya utoaji huduma katika utumishi wa umma na usimamizi wa mchakato wa ajira.
Waziri aliyataja baadhi ya majukumu ya Chuo kuwa ni kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi wa wa umma ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Mafunzo hayo ni katika Nyanja mbalimbali zikiwemo menejimenti ya usimamizi na rasilimali watu, menejimenti, uongozi na utawala, utunzaji wa kumbukumbu na usimamizi wa fedha .
Pia kinatoa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya cheti na stashahada katika maeneo ya menejimenti na utawala, utunzaji wa kumbukumbu na uendeshaji wa ofisi, mafunzo ya uhazili,usimamizi wa fedha za umma , ununuzi na ugavi,huduma za maktaba utawala wa serikali za mitaa, sheria na teknolojia ya habari na mawasiliano.
Chuo kina matawi sita mbayo ni Dar es Salaam, Mtwara, Tabora, Singida Tanga na Mbeya.

1 comment:

  1. Napenda kuuliza kunauhusiano gani kati ya utumishi na wanafunzi wa utumishi wakiwa chuoni?

    ReplyDelete