Matukio : Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii Yaipongeza TASUBA. - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Sunday, 19 March 2017

Matukio : Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii Yaipongeza TASUBA.



Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye akimkaribisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Peter Serukamba (kulia) pamoja na Wajumbe wengine mara baada ya kuwasili katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) kwa ajili ya kukagua mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Peter Serukamba pamoja na Wajumbe wengine mara baada ya kuwasili katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) kwa ajili ya kukagua mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA), Dkt. Helbert Makoye akiwaeleza jambo Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, mara baada ya kuwasili katika taasisi hiyo kwa ajili ya kukagua mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017.

Mkuu wa Kitengo cha Muziki wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) Bi.Rhoda Mitanda (kushoto) akiwaeleza Wajumbe wa Kamati ya Kudumua ya Bunge ya Huduma na Maendeleo kuhusu namna vifaa mbalimbali vya muziki na kazi zake mara walipowasili katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kukagua mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, wakionyeshwa vifaa vitumikavyokatika uhariri wa kazi za sanaa walipoingia katika moja ya Studio ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) kujionea utendaji kazi wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Peter Serukamba akiongea na Wafanyakazi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) mara baada ya kuwasili katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kukagua mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Wafanyakazi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) wakijadiliana wakati wa kikao 17 Machi, 2017.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye akiongea na Wafanyakazi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) wakati wa kikao cha kukagua mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017.










Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakitoa maoni yao wakati wa kikao cha kujadili na kukagua mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017.


Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Wafanyakazi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) wakisikiliza maoni mbalimbali yaliyolenga kuiboresha taasisi hiyo wakati wa kikao cha kujadili na kukagua mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017.

Wanafunzi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) wakionyesha umahiri wao katika sanaa mbalimbali mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii baada ya kumalizika kikao kilicholenga kukagua mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi pamoja na Wanafunzi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) mara baada ya kumalizika kwa ziara iliyolenga kufanya ukaguzi wa mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo, 17 Machi, 2017. (Picha/Habari na Benedict Liwenga-WHUSM)




KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) kwa juhudi zake inazozifanya katika kuibua na kukuza vipaji vya Vijana nchini.


Pongeza hizo zimetolewa leo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani na Wajumbe wa Kamati hiyo wakati walipoitembelea taasisi hiyo kwa ajili ya kukagua mradi wa ukarabati wa taasisi hiyo.


Akiongea wakati wa kikao na Watendaji wa Taasisi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Peter Serukamba amesema kwamba, suala la muziki, filamu na utamaduni ni suala la kipaji, hivyo halihitaji elimu kubwa kwa vijana, bali kuwepo na mazingira mazuri yatakayowezesha wenye vipaji na wasio na vipaji waweze kupata fursa ya kujifunza na kuonyesha vipaji vyao.


Mhe. Serukamba amelishauri Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kuweka mazuri ambayo hayatawabana vijana ambao hawakupata fursa ya elimu lakini wana vipaji, hivyo ameshauri vijana nchini wapewe fursa ya kujifunza na vipaji vyao viendelee kuibuliwa.


Sambamba na hilo, Mhe. Serukamba ameishauri taasisi hiyo kutoa elimu ya lugha mbalimbali kama vile lugha za Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kijerumani, Kichina na nyinginezo ili ziweze kuwasaidia vijana hao wawapo nje ya nchi na pindi wanapokuwa wameiva katika masomo yao ndani ya chuo hicho.


“Chuo hiki naomba kione namna ya kufundisha lugha pamoja kwamba mnafundisha muziki, basi vema mkawafundisha vijana wetu lugha mbalimbali ili waweze kwenda Duniani, kwasababu kama watakuwa na tatizo la lugha itawapa shida”, alisema Serukamba.


Kuhusu suala la bajeti katika taasisi hiyo, ameshauri kwamba, Uongozi wa taasisi hiyo haunabudi kujitangaza ili waweze kupata fedha za kutosha badala ya kulalamika kwamba hawana fedha.


“Lazima Mkuu wa Chuo uende mbali zaidi kwasababu vitu mnavyofundisha hapa katika taasisi yenu ni vya kipekee, havifundishwi kwingine, hivyo una fursa kubwa ya kujitangaza na kuweza kupata fedha za kukisaidia chuo hiki, kwa mfano unaweza kuwatafuta watu toka sekta binafsi ambao hawa wataweza kukusaidia kama vile makampuni mbalimbali hapa nchini”, aliongeza Serukamba.


Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye amesema kwamba, moja ya changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiikabili taasisi hiyo ni mmomonyoko wa kingo za mpaka wa taasisi hiyo ambao umesababishwa na bahari kusogelea eneo la taasisi hiyo hali ambayo inahatarisha majengo yake, hivyo amefafanua kuwa tayari Wizara iliwasiliana na Ofisi ya Makamu wa Rais upande wa Mazingira ambao wao tayari walifika na kupima athari za mmonyoko huo.


Ameongeza kuwa, kwa hivi sasa kinachosubiriwa ni fedha ambazo zitatumika kuanza ujenzi wa kingo ambayo itasaidia kuepusha mmomonyoko huo unaofanywa na maji ya bahari.


“Hili eneo la taasisi ya TaSUBA watu wa NEMC walishafika na kupima na tunategemea katika mwaka ujao wa fedha, fedha itapatikana ili kuanza ujenzi wa kingo katika eneo hili ili tuweze kuzuia maji ya bahari kuendelea kuharibu eneo la taasisi hii”, alisema Mhe. Nnauye.


Kuhusu suala la elimu itolewayo katika taasisi hiyo, amesema kwamba anakubaliana na mapendekezo ya Kamati kwamba, vijana wapewe fursa ya kufundishwa kwa kuangalia vipaji vyao na isiwe lazima sana kuangalia elimu waliyonayo kwani wako vijana wengi ambao wana vipaji lakini hawakupata fursa ya kuelimika, lakini pia na wale walioelimika wanayo nafasi ya kujifunza ndani ya chuo hiko.


Awali akitoa taarifa ya taasisi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dkt. Helbert Makoye amesema kwamba, taasisi anayoiongoza ni taasisi iliyotukuka na inafundisha masuala mbalimbali ya Sanaa, inakuza viwango vya Sanaa, inakuza matumizi ya Sanaa kama vile maonyesho mbalimbali yenye kutoa elimu kwa jamii.


“Hapa chuoni pia tunafundisha watendaji kwenye masuala ya Sanaa lakini pia Wasimamizi, tunawandaa Watafiti na Washauri wa Sanaa na utamaduni kwa ngazi ya Taifa na Kimataifa”, alisema Dkt. Makoye.

No comments:

Post a Comment