Taasisi ya Benjamin W. Mkapa (BMF) jana imekabidhi vitendea kazi (baiskeli 158, mabegi 150, mabuti 25 na makoti ya mvua 25) vyenye thamani ya Shs 33,985,000 kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mej. Jenerali (Mstaafu) Raphaeli Muhuga kwa lengo la kuwasaidia Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na urahisi zaidi.
Taasisi ya Mkapa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma pamoja na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi inatekeleza mradi wa Ukimwi na Kifua Kikuu chini ya Shirika la Save the Children kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.
Mradi huu unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka 3 katika mikoa ya Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma unalenga kuisaidia Serikali kupunguza maambukizi ya Kifua kikuu kwa 25% na kupunguza vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu kwa 50% mpaka kufikia 2020. Pamoja na hayo mradi unalenga kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi, Kupunguza vifo vitokanavyo na Ukimwi, kutokomeza unyanyapaaji na kuongeza upatikanaji wa urahisi wa huduma za Ukimwi hasa upimaji wa VVU.
Katika kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa Taasisi ya Mkapa imetoa mafunzo mbalimbali katika ngazi ya jamii ikiwemo mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii 183 juu ya ubainishaji na ufuatiliaji wa wagonjwa wa kifua kikuu ndani ya jamii. Pamoja na hayo jana imekabidhi baiskeli 158, mabegi 150, mabuti 25, na makoti ya mvua 25 kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi zitakazotumiwa na wahudumu hao katika utekelezwaji wa majukumu hayo ya ubainishaji na ufuatiliaji wa wagonjwa wa kifua kikuu na ukimwi kwenye jamii husika.
Afisa mradi kutoka Taasisi ya Mkapa Bw. David Magiri akikabidhi nyaraka za vifaa kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mej. Jenerali (Mstaafu) Raphaeli Muhuga, kulia kwake ni Katibu Tawala Katavi, Ndg. Paul Chagonja
Bi. Flora Cosmas, Mhudumu wa Afya ngazi ya Jamii akimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mej. Jenerali (Mstaafu) Raphaeli Muhuga, baada ya kupokea baiskeli iliyotolewa na Taasisi ya Mkapa.
Mkuu wa Mkoa Katavi Mhe. Mej. Jenerali (Mstaafu) Raphaeli Muhuga, Katibu Tawala Katavi, Ndg. Paul Chagonja, Afisa Mradi wa Kifua Kikuu na Ukimwi Taasisi ya Mkapa, Ndg. David Magiri katika picha ya pamoja na Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii katika halfa ya kukabidhiwa vitendea kazi kutoka Taasisi ya Mkapa.
Katibu Tawala Mkoa wa Katavi, Ndg. Paul Chagonja akiendesha moja ya baiskeli zilizotolewa na Taasisi ya Mkapa kwa lengo la kuwasaidia ufanyaji kazi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii mkoa wa Katavi
Hafla ya ukabidhishwaji wa vitendea kazi kwa Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii mkoa wa Katavi.
No comments:
Post a Comment