Matukio : Waziri, Mhe. William Lukuvi Akabidhi zaidi ya hati 1,350 Mkoani Morogoro - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


8 Feb 2017

Matukio : Waziri, Mhe. William Lukuvi Akabidhi zaidi ya hati 1,350 Mkoani Morogoro


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amekabidhi hati miliki za ardhi 1,361 kwa wakazi wa vijiji vya Hembeti na Dihombo wilayani Mvomero mkoani Morogoro.

Waziri Lukuvi amegawa hati hizo na kuwasisitiza wananchi wa wilaya ya Mvomero kuhakikisha wanapata hati za umiliki wa ardhi pamoja na kuwataka viongozi wa vijiji kote nchini kuhakikisha wanakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji kuendelea katika maeneo yao.

Pia amesema ili mwananchi aweze kujikimu kimaisha ahakikishe anazitumia hati miliki hizo za kimila kujiletea maendeleo na anaweza kuomba mkopo benki kwa kutumia hati hiyo ili kuendesha shughuli zake za kujipatia kipato kupitia eneo analomiliki kisheria.




Nae Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe amewataka wananchi kuzitunza hati hizo walizokabidhiwa na kuyatumia mashamba yao waliyomilikishwa kwa kuyalima na sio kuyauza au kukodisha kwa watu wengine na wao kubaki masikini.




Waziri Lukuvi pia alimtaka Mkuu wa mkoa wa Morogoro ayaainishe mashamba mengine makubwa yasiyoendelezwa na kugeuka kuwa mashamba pori ili amshauri Rais kuyafutia umiliki wa mashamba hayo na kurudishwa kwao ili kuweza kuwapa kaya maskini ambazo zinaishi katika maeneo ya hayo.




Kazi hii ya upimaji wa maeneo na kutoa hati kwa wananchi ni katika mpango wa nchi wa matumizi bora ya ardhi,ambapo serikali imechangua Mkoa wa Morogoro kuwa wa Mfano katika upimaji wa ardhi na utahusisha nchi nzima kwa wapimaji wa ardhi kutumia vipimo vya kisasa zaidi ambavyo kwa kiasi kikubwa vipimo hivyo vitaweza kupima ardhi kwa kipindi kifupi na kila mtu kumiliki kipande cha eneo lake.




Lukuvi alisema kuwa wakati wa kampeni mwaka 2015,Rais Dkt. John Magufuli alihaidi wazi kuwa kipindi cha miaka 10 kutakuwa na upimaji katika maeneo yote ya nchi kwa utaratibu wa mpango mzuri na wa kisasa, na kwa miaka mitano takribani vijiji 7,500 vitapimwa kwa kupangwa kila halmashauri 25 ambapo na kila mwaka vitapimwa vijiji 1,500 na kutoa hati. Alisema kuwa zoezi la upimaji linaloendelea hivi sasa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM)kwa wananchi katika kuondoa migogoro inayojitokeza.


Na Hassan Mabuye (Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Wizara ya Ardhi)

Mzee Ali Juma mkazi wa kijiji cha Hembeti wilayani Mvomero mkoani Morogoro akimshukuru Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kumuwezesha kupata hati ya kumuliki ardhi yake ambayo amekuwa nayo kwa miaka mingi bila kupewa hati hiyo, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Dkt. Stephen Nindi anayemsaidia kwa kumshika mkono.

Bi. Zaina Hussein mkazi wa kijiji cha Dihombo wilayani Mvomero mkoani Morogoro akipokea hati ya kumuliki ardhi kutoka kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe.

Bibi. Magret Hamis mkazi wa kijiji cha Hembeti akipokea hati ya kumuliki ardhi kutoka kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe.

Baadhi wa wakazi wa vijiji vya Hembeti na Dihombo wilayani Mvomero mkoani Morogoro wakiwa hati zao za kumuliki ardhi mbele Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiongea na wakazi wa vijiji vya Hembeti na Dihombo na kuwataka wahakikishe wanazitumia hati miliki hizo za kimila kwa kujiletea maendeleo.

Baadhi wa wakazi wa vijiji vya Hembeti na Dihombo wilayani Mvomero mkoani Morogoro wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Hembeti wilayani Mvomero mkoani Morogoro Bwana Limbena Madela akimshukuru Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kuwezesha wakazi wa kijiji chake kupata hati miliki hizo za kimila.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad