Zanzibar : Risala ya Rais wa Zanzibar , Dk. Shein Akiukaribisha Mwaka Mpya 2017 - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


31 Dec 2016

Zanzibar : Risala ya Rais wa Zanzibar , Dk. Shein Akiukaribisha Mwaka Mpya 2017





Assalamu Aleikum Warahmatullah Wabarakatuh


Ndugu Wananchi,
Tuna wajibu mkubwa wa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Muweza wa kila jambo kwa kuturuzuku neema ya uhai tukaweza kuifikia siku hii tunapouaga mwaka 2016 Miladiya na kuukaribisha mwaka mpya wa 2017. Hapana shaka, kwamba tuliuanza mwaka 2016 tukiwa na wenzetu ambao kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, wameshatangulia mbele ya haki. Tumuombe Mola wetu awape malazi mema peponi na sisi tulio hai atujaalie kila la kheri katika maisha yetu hapa duniani na atupe hatma njema. Amin!


Ndugu Wananchi,
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu; Subhana Wataala kwa kutuwezesha kuyakabili kwa mafanikio makubwa masuala mbali mbali tuliyoyatekeleza katika mwaka 2016, ambao sasa tunaouaga. Mtakumbuka kwamba miongoni mwa matukio makubwa ya mwaka 2016, ni kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 ambao ulifutwa na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar pamoja na matokeo yake. Uchaguzi huu ukarudiwa tena tarehe 20 Machi, 2016. Katika uchaguzi huo wananchi walishiriki kupiga kura kwa amani na kuitumia vyema haki ya kidemokrasia na kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka. Kwa mara nyengine wananchi mlionesha imani yenu kwa Chama cha Mapinduzi na mimi mkanichagua kwa asilimia 91.4 na vile vile, mmewachagua wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM. Uamuzi wenu huo mmeiwezesha CCM kuunda Serikali, pamoja na kupata idadi kubwa ya Wajumbe wa Baraza la Tisa la Wawakilishi na Baraza hilo nililizindua tarehe 05 Aprili, 2016. Kwa niaba ya viongozi wenzangu wote kwa mara nyengine tunatoa shukurani zetu kwenu na kuahidi kukutumikieni kwa uwezo wetu wote.
Ndugu Wananchi,
Katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja, wa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba, kwenye kipindi hiki cha pili, nchi yetu imepata mafanikio ya kuridhisha katika utekelezaji wa mipango yetu mikuu ya maendeleo ikiwemo Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020, MKUZA, Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 pamoja na mipango mingine ya kisekta. Tathmini tuliyoifanya hadi tunapouaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2017, inaonesha tumeweza kupiga hatua katika malengo yetu ya kuinua uchumi na kuimarisha huduma za jamii, zikiwemo afya, elimu na huduma za maji safi na salama na nyenginezo.
Ndugu Wananchi,
Uchumi wetu umeendelea kuimarika. Kwa mwaka 2015, Pato Halisi la Taifa lilikua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 6.6. Hadi kufikia robo mwaka ya pili (Aprili - Juni) mwaka 2016 uchumi umekua kwa kasi ya asilimia 6.2. Kadhalika, tumefanikiwa kuongeza kiwango cha kukusanya kodi. Kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, 2016 Serikali imeweza kukusanya jumla ya TZS bilioni 441.3 kutokana na vyanzo vyetu vya ndani. Kwa kipindi kama hicho mwaka jana (2015) tulimudu kukusanya TZS bilioni 336.6. Hii ina maana kwamba kwa miezi kumi ya mwanzo ya mwaka 2016, mapato yetu yameongezeka kwa TZS bilioni 104.7 sawa na ukuaji wa asilimia 31.1. Sambamba na mafanikio hayo, washirika wetu wa maendeleo wameithamini sana kazi nzuri tunayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi. Katika kuthibitisha imani yao kwetu, Serikali imepokea jumla ya TZS bilioni 54.53 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kati ya mwezi wa Januari hadi Oktoba, 2016. Kipindi kama hicho kwa mwaka 2015 tulipokea TZS bilioni 47.47, sawa na ongezeko la asilimia 14.9. Huu ndio ukweli halisi na hio ndiyo hali halisi ambayo ni vyema wananchi mkaifahamu kuwa ni nzuri; kinyume na maelezo yanayotolewa na baadhi ya watu ambao hawana taarifa sahihi na takwimu za uhakika za Serikali yetu. Tutajidhatiti zaidi katika mwaka ujao na Mwenyezi Mungu akipenda mambo yatakuwa bora zaidi.
Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa huduma za jamii mwaka unaomalizika, utakumbukwa kwa hatua za mafanikio tuliyoyapata katika kuimarisha huduma za afya nchini. Tarehe 11 Novemba, 2016 tulizindua majengo ya wodi mpya ya watoto na wodi ya wazazi katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja. Wodi hizo zimetiwa vifaa vya kisasa vya kutolea huduma, na kuwa na nafasi ya kutosha kwa wagonjwa watakaofika kuhudumiwa. Hii ni hatua muhimu katika utekelezaji wa lengo la Serikali la kuifanya Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa hospitali ya rufaa kamili na kuimarishwa kwa huduma zake.
Kadhalika, tarehe 26 Novemba, 2016 tulifanya uzinduzi mwengine nao ni wa Hospitali ya Abdalla Mzee, Mkoani Pemba baada ya kujengwa upya kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Kufunguliwa kwa hospitali ya Abdalla Mzee ambayo sasa imefikia hadhi ya Hospitali ya Mkoa kutawawezesha wananchi wa Pemba kupata huduma mbali mbali za afya ambazo mwanzoni walilazimika kuzifuata nje ya Kisiwa cha Pemba. Dhamira ya Serikali ni kuyaendeleza mafanikio hayo katika mwaka ujao, kwa kuzidi kuchukua hatua ili huduma za afya nchini ziimarike zaidi na ziwe za viwango bora. Maelekezo ya kina ya mafanikio tuliyoyapata kwa kila sekta, penye majaaliwa nitayatoa katika hotuba yangu ya kilele cha maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ifikapo tarehe 12 Januari, 2017.
Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la kuwaenzi wazee wetu na kuthamini mchango wao katika maendeleo ya nchi yetu, Serikali, katika mwaka unaomalizika, ilianza utekelezaji wa Mpango wa Pencheni ya Jamii. Kupitia mpango huu wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 na kuendelea waliosajiliwa, wameanza kupewa posho la TZS 20,000 kwa mwezi. Kuanzia mwezi Aprili 2016, tulipoanza utaratibu huu, idadi yao imeongezeka kutoka watu 21,263 waliosajiliwa mwaka 2015, hadi kufikia watu 26,603 mwezi wa Novemba, 2016.
Hivi sasa Serikali inaendelea kuwasajili watu wengine waliotimiza sifa za kuwemo katika mpango huo ambao hapo mwanzo hawakusajiliwa. Vile vile tutazifanyia kazi changamoto zilizojitokeza kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mpango huo. Kadhalika, Serikali inazingatia haja ya uwezekano wa kuongeza idadi ya wazee wanaopaswa kuwemo kwenye mpango huu, kwa kupunguza umri hadi kufikia miaka 65 badala ya miaka 70 kama ilivyo hivi sasa. Vile vile, tunazingatia haja ya kuwaandalia wazee huduma za afya kwa dhamira ile ile ya kuwatunza na kuwaenzi wazee wetu.
Ndugu Wananchi,
Tukio jengine mahususi katika mwaka tunaoumaliza lilikuwa ni kutiwa saini kwa Sheria Namba 6 ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016 inayoipa Zanzibar uwezo wa kisheria wa kushughulikia utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia. Hili ni tukio kubwa, ambalo kwa umuhimu wake tuliamua kulifanya hadharani hapo tarehe 15 Novemba, 2016, kwenye ukumbi wa Ikulu, mbele ya viongozi mbali mbali, wafanyakazi, wananchi na wafanyakazi wa vyombo vya habari. Kufuatia hatua hii, Zanzibar imepata uwezo wa kisheria wa kushughulikia utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizi muhimu ili nazo ziweze kuchangia pato la uchumi wetu. Hadi sasa mipango yetu katika suala hili inaendelea vizuri. Tunaendelea na mazungumzo na baadhi ya wawekezaji wenye uwezo mkubwa na uzoefu wa masuala ya mafuta na gesi asilia ambao wana nia ya kuwekeza nchini kwetu.
Ndugu Wananchi,
Katika mwaka tunaoumaliza, Serikali iliendelea kufanya jitihada katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini kama ilivyo kwa mataifa mengine duniani. Katika jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia Mfuko wa Uwezeshaji kwa kutoa mikopo kwa wananchi wanaojishughulisha na biashara, kilimo, uvuvi, ufugaji na nyenginezo, vile vile, Serikali iliandaa Kongamano na maonesho ya Wajasiriamali tarehe 03 Disemba, 2016 na tarehe 04 Disemba, 2016 ambapo maonyesho hayo yalifanyika katika jengo la zamani la Baraza la Wawakilishi Kikwajuni.
Lengo la kongamano na maonesho hayo lilikuwa ni kutoa fursa kwa wajasiriamali kujifunza mbinu bora za kufanya shughuli zao ili kuongeza tija. Aidha, shughuli hiyo ilikuwa na lengo la kuongeza hamasa na taaluma, hasa kwa vijana ili waweze kuzifahamu fursa ziliopo katika ujasiriamali, kwa lengo la kujiajiri wenyewe na kuondokana na hisia za kutegemea ajira chache zinazopatikana Serikalini. Katika mwaka ujao, Serikali itaendeleza jitihada za kuwasaidia wajasiriamali kwa kuwapatia fursa zaidi za mikopo, kutafuta masoko ya bidhaa zao na kuwapa mafunzo kwa njia ya mafunzo mbali mbali, zikiwemo semina na makongamano pamoja na kukiendeleza kituo cha kukuza na kulelea Wajasiriamali, kilichopo Mbweni.
Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha Maadili ya Viongozi na utawala bora, Serikali katika mwaka 2016 ilikamilisha uundaji wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo tayari imeshaanza kufanya kazi zake. Madhumuni ya kuchukua hatua hizo ni katika utekelezaji wa matakwa ya kisheria kwa mujibu wa sheria ya Maadili Namba 4 ya mwaka 2015. Miongoni mwa majukumu ya Tume ya Maadili ni kuhakikisha kwamba viongozi wa umma na wale wote waliotajwa katika sheria ya Maadili, wanajaza fomu ya tamko la rasilimali na madeni ambazo tayari zimekwishatolewa kwa wahusika na kutakiwa kuzirejesha Tume fomu hizo, si zaidi ya tarehe 31 Disemba, 2016.
Napenda nisisitize kauli yangu niliyoitoa tarehe 10 Disemba, 2016 katika maadhimisho ya siku ya Maadili kwenye viwanja vya bustani ya Victoria, ya kuwataka wanaohusika wote wazingatie maelekezo yaliyotolewa kwenye fomu hio na waepuke kutoa taarifa zisizo za kweli, kwani kufanya hivyo ni kitendo cha kuvunja maadili ya uongozi. Aidha, nahimiza kuwa kila mmoja wetu azingatie kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya maadili isemeyo:“Imarisha utawala bora kwa kukuza uadilifu, uwajibikaji, haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa.” Huo ni ujumbe muhimu wa kuuzingatia wakati tunapouanza mwaka mpya wa 2017. Sote tuazimie kuitekeleza kauli hii kwa vitendo, kwani nchi yetu inaongozwa kwa kufuata sheria na misingi hiyo muhimu ya utawala bora.
Ndugu Wananchi,
Katika kusherehekea kumalizika kwa mwaka huu na kuja kwa mwaka mpya, wapo baadhi ya watu ambao husherehekea kwa vitendo ambavyo huweza kuharibu amani na utulivu na kusababisha usumbufu kwa watu wengine. Ni vyema sote tuzingatie umuhimu wa kuitunza amani, umoja na mshikamano wetu kwani ndiyo msingi wa mafanikio tunayoendelea kuyapata katika nyanja za uchumi, siasa na ustawi wa jamii. Kwa hivyo, kila mmoja wetu ana jukumu la kudumisha amani kwani Serikali haitosita kumchukulia hatua mtu yeyote au kikundi chochote kitakachofanya vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa wananchi na mali zao pamoja na wageni wanaoitembelea nchi yetu.
Ndugu Wananchi,
Wakati tunauaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka 2017, nchi yetu bado inakabiliwa na changamoto mbali mbali, zikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi, zinazoathiri ufanisi katika utekelezaji wa mipango yetu ya kiuchumi na maendeleo. Tuna changamoto ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana na tatizo la kuendelea kuwepo kwa vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto. Taarifa kutoka katika Jeshi la Polisi Zanzibar zinaonesha kuwa idadi ya makosa ya udhalilishaji wa kijinsia, yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi, yameongezeka kutoka makosa 169 mwaka 2015 hadi kufikia makosa 512, kati ya Januari hadi wiki ya pili ya Disemba, 2016 sawa na ongezeko la asilimia 203. Hii si taarifa nzuri. Natoa wito kwa wananchi wote tushirikiane katika kuvikomesha vitendo vya udhalilishaji. Ni dhahiri kuwa ufumbuzi wa changamoto hizi unahitaji mchango wa kila mmoja wetu na sio Serikali peke yake.
Sote tuna wajibu wa kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo pamoja na kutii sheria bila ya kushurutishwa. Mafanikio yetu ya sasa na yale ya baadae yanategemea sana ushirikiano na umoja wetu, katika kujenga nchi yetu. Mambo hayo muhimu yawe ndiyo dira yetu. Ni jukumu letu sote kwa pamoja na lazima tutimize wajibu wetu huo.
Ndugu Wananchi,
Kwa kumalizia risala yangu hii, napenda nikukumbusheni kwamba tarehe 12 Januari, 2017, tunaadhimisha Miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Sote tuna wajibu wa kuyasherehekea na kuyadumisha Mapinduzi kwani ndiyo yaliyotukomboa. Wito wangu kwenu ni kwamba kila mmoja wetu ajitahidi kushiriki katika maadhimisho yetu hayo yanayotanguliwa na shamra shamra mbali mbali za uzinduzi wa miradi ya maendeleo kwa uwekaji wa mawe ya msingi. Aidha, jambo hili litaongeza chachu ya sherehe zetu tutakaposhiriki katika siku ya kilele kwenye Uwanja wa Amaan ili kuzifanikisha sherehe hizi adhimu na muhimu.
Namalizia risala yangu kwa kutoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wote wa Zanzibar, Tanzania Bara, ndugu na marafiki wote popote walipo. Kadhalika, natoa salamu kwa viongozi wa nchi marafiki, Taasisi za kimataifa na washirika wetu mbali mbali wa maendeleo. Mola wetu aujalie kheri na baraka nyingi mwaka mpya wa 2017. Aiongezee nchi yetu amani, umoja, mshikamano na mapenzi baina yetu. Mwenyezi Mungu atupe uwezo wa kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.




No comments:

Post a Comment

Post Top Ad