Matukio : RC Gambo atoa pikipiki 200 kwa waendesha Bodaboda Jijini Arusha - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Monday, 28 November 2016

Matukio : RC Gambo atoa pikipiki 200 kwa waendesha Bodaboda Jijini Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo (aliyesimama) akiongea na madereva wa boda boda kuwaelezea mpango wa Serikali wa kuwapatia Pikipiki 200.

Nteghenjwa Hosseah

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo amekutana na waendesha bodaboda wa Jiji la Arusha na kuwajulisha kuhusu mpango wa Serikali wa kuwakwamua kiuchumi kwa kuwawezesha kupata Pikipiki bila Riba wala dhamana.

Rc Gambo amekuja na Mpango huu wa Kuinua uchumi wa Vijana kwa kuwapatia Pikipiki baada ya kukutana na kundi hili la waendesha boda boda kwa mara na kusikiliza malalamiko yao huku miongoni mwa kero yao kubwa ni kutozwa fedha nyingi na wamiliki wa boda boda hizo.

Akiongea na waendesha boda boda Rc Gambo alisema ninaona jinsi mnavyojituma katika kujitafutia riziki lakini hamthaminiki na kazi hii imekua ikidharaulika, sasa muda umefika kwa kazi hii kuwa ya heshima mbele ya Jamii, kila kijana aliyepo katika biashara hii ataweza kumiliki Pikipiki yake na sio kuendesha Pikipiki za watu ambao wamekuwa wakiwanyonya kila siku kwa kuwatoza Fedha nyingi na wao kuzidi kuneemeka wakati ninyi mnazidi kuwa masikini.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (Katikati) akiwasili kwenye Kikao na waendesha bodaboda wa Jiji la Arusha.

“Kundi hili limekuwa likitumiwa kwa maslahi ya watu wachache kwa kuwa wamekuwa wakipewa Pikipiki hizo kwa faidi kubwa na mmiliki anapokea Fedha zaidi yya mara mbili ya bei ya kununulia Pikipiki hiyo ndipo aamue kummilikisha kijana pikipiki hiyo au aamue kuendelea kupokea Fedha kwa kipindi chote wakati ninyi mnapata tabu barabarani huko na mnaambulia Fedha kidogo kiasi ambacho hamuwezi fikia hatua ya kumiliki Pikipiki zenu” Alisema Gambo.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mkoa wa Arusha imeona ni vyema ikawajengea uwezo vijana waliopo katika kazi hii kwa kuwapa mafunzo na kuwapatia Pikipiki ambazo mtatakiwa kurejesha kiasi cha Fedha halali iliyonunuliwa Pikipiki hiyo kisha kumilikishwa chombo bila ya riba yeyote wala dhamana.
Lucas Malusu ni dereva wa boda boda Kutoka Kata ya Elerai (aliyesimama katikati) akitoa maoni yake katika kikao chao na Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Aliendelea kusema utoaji wa Pikipiki hizi utazingatia Kata zote zilizopo katika Jiji la Arusha ili Pikipiki ziweze kuwafikia walengwa na zoezi hili litaendelea kwa vijana wengine kadiri ya mahitaji; Tutaongeza usimamizi kwa wote watakaopata Pikipiki hizi ili waweze kurejesha Fedha kama inavyotakiwa na tuweze kuwanunulia vijana wengine hatimaye tuwafikie vijana wote wenye uhitaji wa kumiliki na kufanya biashara ya bodaboda.

Serafini Shirima ni dereva wa boda boda Kata ya Levolosi akizungumza katika Kikao hicho alisema kwa mara ya kwanza Katika Mkoa huu wamepata mlezi anayetambua na kuthamini kazi ya boda boda na aliyethubutu kuwatafutia Pikipiki za bei nafuu ili kuongeza kipato cha vijana wa Arusha.

Shirima alishauri kuundwa kwa kamati ya mpito itakayosimamia na kuratibu mchakato mzima wa vijana watakaoanza kupewa Pikipiki hizo na kukamilisha taratibu zote za uanzishaji wa umoja wa wandesha Boda boda utakaofahamika kwa jina la (UBOJA) chini ya Mlezi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Gambo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (aliyesimama mbele) akihitimisha kikao chake na waendesha boda boda wa Wilaya ya Arusha.

RC Gambo alikamilisha Kikao hicho kwa kusimamia uchaguzi wa viongozi wa mpito kutoka katika Kila Kata na hatimaye kupatikana viongozi watano watakaoratibu mpango wa awali wa utoaji wa Pikipiki kwa vijana.

Pikipiki zitakazotolewa katika awamu ya kwanza ni 200 zikiwa na thamani ya Tsh Mil 400 na zitatolewa sanjari na Bima kubwa(Comprehensive Insurance) kwa vijana 200 ambapo kila Kata itatakiwa kutoa vijana 8.

Vijana wa Arusha watakabidhiwa Pikipiki hizi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassimu Majaliwa tarehe 03/12/2016 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Baadhi ya waendesha boda boda wakifuatilia kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya Ndg. Polycarp Nkuyumba(aliyesimama) akiwakaribisha viongozi na wadau kwenye Kikao na waendesha boda boda wa Wilaya ya Arusha.
Serafini Shirima(aliyesimama) ni dereva wa boda boda kutoka Kata ya Levolosi akichangia uanzishwaji wa umoja wa wandesha boda boda Wilaya ya Arusha (UBOJA).
Viongozi wa mpito waliochanguliwa kusimamia taratibu za uanzishjwaji wa Umoja huo pamoja na utoaji wa Pikipiki wa vijana nane wa Kila Kata.