Makala : Kustaafu kwa Bi. Arianna Huffington kuna maana gani kwa Issa Michuzi ? - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


14 Aug 2016

Makala : Kustaafu kwa Bi. Arianna Huffington kuna maana gani kwa Issa Michuzi ?


Na Ankal
Nilipopata tarifa kuwa  Blogger mkongwe Bi. Arianna Huffington (pichani) anastaafu kutoka Mtandao wa Jamii   ama blog ya Huffington Post
 (BOFYA HAPA)   ili kuanzisha mtandao wa Thrive Global unaohusiana na staili za maisha na afya (BOFYA HAPA), nilistuka sio kidogo maana daima amekuwa kichocheo changu kikubwa katika tasnia hii ya habari za mtandaoni.
Bi. Huffington alianzisha mtandao wake huo wa  Huffington Post mwaka 2004 (Globu ya Jamii ilianza mwaka 2005) baada ya Rais George W. Bush kuchaguliwa kuongoza Marekani kwa mara ya pili, na wakati huo huo vita ya Iraq ilikuwa ikiendelea. 
Blog hiyo ilianza kiutani-utani kwa taarifa za kawaida na michango hii na ile kutoka kwa marafiki zake, kabla ya sio tu kuwa moja ya blog kubwa duniani bali pia kampuni  kubwa ya habari mtandao duniani yenye matawi  katika nchi 15 kwa jina la Huffington Post Media Group.
Kampuni hiyo hivi sasa inaajiri watu 850 kila pembe ya dunia na imeendelea kuwekeza katika kusaka na kutoa habari mtandao kwa picha, maandishi na video na kujizolea tuzo kibao ikiwemo ya Pulitzer Prize ambayo ni kubwa kuliko zote.
Japokuwa  Bi. Huffington  amekuwa akijihusisha na maswala ya siasa muda wote, ikiwemo kumpinga  waziwazi  mgombe urais Donald Trump tokea atangaze azma yake hiyo ,  pia amekuwa akitumia muda wake mwingi katika maswala ya afya na maisha kwa kuandika kitabu  kuhusiana na mambo hayo mwaka 2014 kiitwacho Thrive na mwaka huu kuandika kingine kiitwacho The Sleep Revolution.  Mnamo mwezi wa June mwaka huu akatangaza kuanzisha mtandao wa Thrive Global.
Katika mahojiano, Bi. Huffington  anaripotiwa kusema kuwa hawezi kujenga kampuni mpya kama kazi ya pembeni, hasa katika wakati huu ambapo wawekezaji wameshaanza kuwekeza mamilioni ya dola kwenye  kampuni ya Thrive Global.
Majukumu yake yamewahi kubadilika mara moja huko nyuma, hususan pale kampuni ya AOL  kuinunua blog ya Huffington Post mwaka 2011 kwa dola milioni 315.  Katika makubaliano hayo  Bi. Huffington alibakia kuwa Mhariri Mkuu na wakati huo huo Rais wa Huffington Post Media Group.
Kuondoka kwake katika kampuni hiyo kumekuja wakati kampuni ya Verizion ilipoinunua kampuni ya AOL  kwa dola bilioni 4.4, na kutangaza pia kutaka kuinunua Yahoo kwa dola bilioni 4.8. Ila yeye alikana kuwa kuondoka kwake kunahusiana na manunuzi hayo, bali alisema muda ni muafaka wa kuanza mambo mengine.
Nilipata bahati ya kukutana ana kwa ana na Bi. Arianna Huffington huko  Davos, Uswisi, mnamo  Januari 26 mwaka 2012 (BOFYA HAPA) na kubadilishana naye mawazo pembezoni mwa  mkutano wa dunia wa uchumi. Nilifarijika sana pale mama huyo nguli wa habari za mitandaoni aliposema anaifahamu Michuzi Blog nami  nikamfurahisha kwa kumwambia nafuatilia kila hatua anayopitia.
Nikikumbuka kukutana kwetu huko Davos na kuifikiria kauli hiyo, mie pia  sasa nimeanza kujiuliza endapo  kama sasa ni muda  muafaka wa kuachana na  Globu ya Jamii na kuendeleza Libeneke kwa njia zingine? 
Jibu nitalitoa ifikapo Septemba 8, mwaka  huu wakati wa maadhimisho ya miaka 11 ya Globu ya Jamii.Kitabu hiki nilipewa kama zawadi na dada Emelda Mwamanga wa jariba maarufu la BANG! ambaye alitembelea ofisi za Huffington Post huko Marekani mwaka 2009. Naye akaniambia baada ya kupewa kitabu hicho akanikumbuka mara moja na kuamua kuja kunizawadia.  Asante sana Emelda. Still touched by the gesture...Nami nimeanza kuandika changu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad