Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, imejipanga kuanzisha mnada wa madini ya vito ya Tanzanite katika eneo maalumu la kibiashara ili kusaidia kuongeza pato la ushuru wa huduma kwa jamii.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Yefred Myenzi, akizungumza na wakazi wa Mji mdogo wa Mirerani, alisema uimarishaji wa ukusanyaji wa mapato ni moja ya maagizo ya kitaifa ya kusogeza huduma karibu na jamii. Myenzi alisema msukumo wa mbunge wa jimbo hilo James Ole Millya unahitajika kubadili sheria ili ushuru wa huduma uongezeke kutokana na kukosekana kwa mfumo madhubuti wa kuwabana walipa kodi wakubwa kama wa migodi ya madini.
Alisema inasikitisha kuona utajiri mkubwa wa rasilimali zilizopo Simanjiro hauakisi maisha ya wakazi wake, wala miundombinu yake na huduma za kijamii kama elimu, afya, maji umeme na huduma za kifedha na mawasiliano.“Simanjiro ina jina kubwa nchini na duniani kutokana na madini ya vito aina ya Tanzanite yanayopatika eneo la Mirerani pekee duniani na mtu ana matarajio ya kushuhudia maendeleo yanayoshabihiana na utajiri huo,” alisema Myenzi.
Alisema wigo wa eneo la kijiografia haliwiani na idadi ya wataalamu wa halmashauri kukusanya mapato pale wanapotakiwa na ukwepaji kodi unaohusisha ukosefu wa uadilifu wa watumishi, wafanyabiashara na wananchi.“Naamini Simanjiro ya leo siyo ya jana na sivyo itakavyokuwa kesho, wenzetu waliotangualia walifanya walichoweza kwa nafasi yao nasi tumepewa fursa hii tuitumie kuandika historia na tuache urathi usiofutika,” alisema Myenzi.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jackson Sipitieck alisema wanamatarajio makubwa na mkurugenzi huyo mgeni na watahakikisha wanampa ushirikiano wa kutosha kwa ajili ya maslahi ya jamii.
Mbunge wa jimbo hilo Ole Millya alisema kutokana na elimu ya shahada mbili alizonazo Myenzi anatarajia jamii ya Simanjiro kwa namna moja au nyingine watanufaika naye kupitia miradi ya maendeleo ikiwemo elimu, afya, na maji.
Wananchi wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakimsikiliza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Yefred Myenzi akizungumza nao.Diwani wa kata ya Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Philemon Oyogo akizungumza na wananchi wa kata hiyo, baada ya viongozi wa wilaya hiyo kuwatembelea
No comments:
Post a Comment