Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Khalid Salum Mohamed ameeleza hayo wakati akisoma Mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kuhusu Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016-2017 katika Baraza la Wawakilishi Chukwani Nje kidogo wa Mji wa Zanzibar .
Alisema serikali imekusudia kutekeleza ahadi yake ya kuimarisha maslahi ya wafanyakazi hususan wa kipato cha chini ili waweze kumudu vyema maisha yao na kuhamasika kufanya kazi kwa bidii.
Aidha alisema kuwa serikali imekusudia kupunguza kodi katika kipato cha mshahara wa wafanyakazi na kuweka viwango vyake sawa na Tanzania Bara ili kwenda sambamba na hatua ya kupandisha kima cha chini cha mshahara
Pia aliwataka wafanyakazi kujituma zaidi kwa ufanisi ili kuongeza tija na kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kukuza kwa haraka uchumi wa nchi na kuongeza wigo wa mapato ya serikali na kupunguza mzigo mkubwa wa matumizi yasiyo ya msingi.
Dkt Khalid alisema kwa kuzingatia malengo makuu ya Serikali na mustakabali wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha katika kila shilingi inayotumika senti 58.7 ziende katika sekta tano zinazobeba malengo makuu ya serikali .
Akizitaja sekta hizo ni Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji ,Elimu na Mafunzo ya Amali ,Afya ,Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira na Kilimo ,Maliasili , Mifugo na Uvuvi ambapo zinatarajiwa kutumia jumla ya shilingi TZS 494.2 bilioni kati ya TZS841.5 bilioni za matumizi ya Serikali .
Aidha Waziri huyo alisema Serikali haikusudii kupandisha kodi yoyote katika vianzio vyake vya mapato ya ndani zaidi na kurekebisha viwango vya ada mbali mbali vilivyopitwa na wakati na badala yake inatajia kupanua wigo wa kodi kwa kuimarisha ufanisi katika ukusanyaji na kuongeza uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato.
Aidha alifahamisha kuwa kutokana na hali ya muelekeo wa fedha sera kuu ya matumizi inahitaji kubana zaidi matumizi kulingana na vianzio vya mapato vilivyopo kwa kupunguza madeni hasa ya kiinua mgongo, walimu, wazabuni na Dhamana za hazina .
Hata hivyo waziri Khalid alieleza serikali itaendelea na jitihada zake za kuwaenzi wazee kwa kuendelea kutoa pencheni maalum kwa wazee waliofikia umri wa miaka sabini na zaidi kwa kiwango cha TZS 20,000 kwa kila mwezi kwa wazee wote wa Unguja na Pemba.
Katika kutekeleza malengo Waziri Khalid ameliomba Baraza hilo liidhinishe Mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa fedha 2016/2017 yenye mapato ya jumla TZS 841.5 bilioni zikiwemo TZS 482.4 bilioni za mapato ya ndani, TZS 324.8 bilioni kutokana na Ruzuku na Mikopo ya nje, TZS 1.3 bilioni kutokana na misamaha ya madeni na bilioni 33.0 bilioni za mikopo ya ndani.
Pia ameomba kuidhinishwa matumizi ya 841.5 bilioni ikiwa TZS445.6 bilioni kwa matumizi ya kawaida na TZS 395.9 bilioni kwa kugharamia Mpango wa Maendeleo.
Khadija Khamis na Mariyam Kidiko – Maelezo Zanzibar
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dk.Khalid Salum Mohammed akionesha mkoba wenye Bajeti ya Serikali ya Zanzibar ya mwaka wa Fedha 2016/2017 wakati alipokuwa akiingia Baraza la Wawakilishi kwa kuiwasilisha Bajeti hiyo.
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa mwaka wa Fedha 2016/2017 katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Baadhi ya Mabalozi wadogo wanaowakilishi nchi zao Zanzibar wakisikiliza Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dk.Khalid Salum Mohammed kuhusu mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya Serekali kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
Wajumbe wa Baraza la wawakilishi wakifuatilia Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa Fedha 2016/2017 wakati Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Khalid Salum alipokuwa akiwasilisha Hutuba hiyo. Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar. Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar
No comments:
Post a Comment