Teresia Mhagama na Asteria Muhozya
Imeelezwa
kuwa, Wizara ya Nishati na Madini imeendelea kurahisisha utoaji wa
huduma za leseni za madini ambapo sasa wamiliki wa Leseni hizo wanaweza
kupata taarifa za ada ya leseni kwa njia ya ujumbe wa simu (SMS).
Mkuu
wa Kitengo cha TEHAMA katika Wizara ya Nishati na Madini, Francis
Fungameza alisema kuwa ili mteja aweze kupata huduma hiyo anatakiwa
kuandika neno MEM, ache nafasi , kisha aandike Namba ya Leseni na
kutuma kwenda 15341.
Fungameza
alisema kuwa hizo ni habari njema kwa wamiliki wa leseni kwani sasa
wataweza kupata taarifa hizo kwa wakati na hivyo kulipia ada za
leseni hizo kwa wakati.
Aidha
Fungameza alisema kuwa Wizara imekuwa ikibuni njia mbalimbali ili
kuhakikisha kuwa huduma za utoaji wa leseni za madini pamoja na taarifa
mbalimbali kuhusu leseni hizo zinapatikana kwa urahisi na uharaka
tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
“Kwa
mfano kwa sasa tayari kuna mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama
Online Mining Cadastre Transactional Portal (OMCTP) ambao unawawezesha
wateja kufanya masuala mbalimbali ikiwemo kufanya malipo ya leseni na
mrabaha, wateja waliosajiliwa kutuma maombi ya leseni, kuhakiki taarifa
za leseni wanazomiliki na kutuma taarifa za utendaji kazi .
Aliongeza
kuwa Mfumo wa OMCTP pia unawawezesha wateja kupata taarifa mbalimbali
za Sekta ya Madini zikiwamo ramani za kijiolojia na taarifa za migodi
mikubwa.
Fungameza
alieleza kuwa hapo awali, mfumo wa utoaji leseni ulifanyika kwa njia
ya mkono (manually) na ulitegemea utumaji wa karatasi (paperwork based)
na hali hiyo ilichangia kuchelewesha utoaji leseni na kuongeza kuwa
utoaji huo wa leseni ulitegemea hali ya mawasiliano kama ya telegram na
rejesta.
“
Vilevile upimaji na uchoraji ramani za kijiolojia ulifanyika kwa njia
ya mkono na ulitegemea umahiri wa mtu na mara nyingine makosa
yalifanyika na kusababisha migogoro au waombaji kukosa leseni kwa sababu
zisizo za msingi,” aliongeza Fungameza.
Anasema
kuwa mfumo huo wa awali ulileta changamoto kwani Wizara ilikuwa na
wakati mgumu kuhakikisha kuwa kumbukumbu za leseni zinatunzwa vizuri
bila kupotea, pia kulikuwa na kazi ngumu ya kuchambua nyaraka za leseni
kwa njia ya mkono (manually) ili kufuatilia uhai wa leseni, malipo ya
ada na utendaji wa wamiliki wa leseni.
Aliongeza
kuwa leseni nyingi hazikuweza kuchambuliwa na hali hiyo iliathiri ubora
wa utendaji wa Wizara na pia kasi ya kuwahudumia wananchi ilikuwa
ndogo.
Alisema
kuwa mfumo wa kieletroniki unaotumika sasa katika leseni za madini
unakuwa kama kituo kimoja (one-stop-centre) kinakachotumiwa na wadau wa
Sekta ya Madini walio nchini na nje ya nchi kuweza kujipatia huduma za
leseni bila kulazimika kusafiri kwenda kwenye ofisi ya Madini, pindi
wanapokuwa wamesajiliwa ndani ya mfumo huo.
Alisema
kuwa OMCTP ina faida mbalimbali ikiwemo, kuongeza uwazi na kasi ya
utoaji wa leseni za madini na Wateja kuingiza maombi ya leseni wao
wenyewe hivyo kupunguza tatizo la mlundikano wa maombi kwenye ofisi za
madini.
Aliongeza
kuwa Wateja na Serikali watakuwa na uhakika na maombi yote
yatakayowasilishwa (yakiwamo maombi ya sihia (transfer), kuhuisha leseni
na pia kuwa na uhakika na malipo yote yatakayofanywa kupitia mfumo wa
OMCTP.
“
Kupitia mfumo huu, Wateja pia wanapata taarifa za leseni zao kila
wakati na kujua wanapotakiwa kufanya malipo ya leseni au watakapotakiwa
kutuma taarifa za utendaji kazi na pia kurarahisha mawasiliano kati ya
Wizara na wamimiki wa leseni,” alisema Fungameza.
Aidha
alisema kuwa Wateja wataweza kuhuisha taarifa za leseni zao za madini
kama vile anuani na namba za simu kupitia mfumo wa OMCTP pindi taarifa
hizo zitakapobadilishwa.
No comments:
Post a Comment