Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema vita inayoendeshwa na Serikali ya awamu ya
tano dhidi ya wala rushwa na wale wanaofanya ufisadi siyo nguvu ya soda
kama wengi wanavyofikiri.
“Serikali
ya awamu ya tano imedhamiria kupambana na wala rushwa na mafisadi. Wala
hatutanii. Hawa tutacheza nao na wala wasidhani vita hii ni nguvu ya
soda. Tutaendelea kuwasaka hadi tufike mwisho,” alisema Waziri Mkuu
wakati akizungumza na Watanzania waishio Zambia katika mkutano
uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini Lusaka, Zambia juzi jioni
(Jumanne, Mei 24, 2016).
“Hatutaki
tabia iliyokuwepo ya mwananchi anakuja ofisini kutaka huduma lakini
hasikilizwi hadi atoe chochote, sisi hiyo tabia hatutaki kuisikia
kabisa. Tumedhamiria kurudisha heshima kwenye utumishi wa umma na
nimeanza kupata faraja kwani sasa hivi (nimeambiwa) katika baadhi ya
taasisi unasikia mtu akiulizwa una shida gani, nenda pale, jambo ambalo
zamani halikuwepo,” alisema.
Alisema
Serikali imeamua kupigia debe dhana ya utumishi wenye uadilifu kwa
sababu huo ni utamaduni mpya. “Ni kipindi kigumu kidogo cha mabadiliko
lakini tumesimamia mabadiliko haya na ndiyo maana watumishi wote
tumewasisitizia kuwa suala la uaminifu, uadilifu na uwajibikaji ni
muhimu,” alisema na kuongeza:
“Hatutamvumilia
mtumishi yeyote ambaye hatakuwa tayari kuwatumikia Watanzania au
atakayeendekeza uzembe lakini pia hatutamuonea mtu yeyote. Hapa
tunasisitiza usawa na hatutaki kutengeneza gap kati ya mwananchi
mtumishi na wa mwananchi wa kawaida, tunataka kila mwananchi aione
Tanzania ni nchi yake na kila kinachozalishwa ni sehemu yake. Tukifika
hapo, tunaamini kila mmoja ataweza kuisemea nchi yake.”
Akizungumzia
kuhusu ubadhirifu wa fedha za umma, Waziri Mkuu alionya kwamba Serikali
imelipa kipaumbele suala la uaminifu na uadilifu kwenye fedha za
Serikali na kwamba haitakuwa tayari kuona fedha hizo zikifujwa.
“Hivi
sasa Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na
fedha hizo zitaenda vijijini. Tunataka zikafanye kazi iliyokusudiwa, na
wale wadokozi wajue kuwa wamekalia kaa la moto,” alisema huku
akishangiliwa.
Alisema
watumishi wa umma wana wajibu wa kusimamia kazi zilizopangwa na
kuhakikisha miradi iliyolengwa inakamilika. “Kama fedha zimeletwa
kujenga zahanati simamia zahanati ijengwe na ni lazima zahanati hiyo
ionekane,” alisema.
Alisema
bajeti ya mwaka huu imeongezeka kutoka sh. trilioni 21 hadi trilioni 29
lengo kuu likiwa ni kuleta maendeleo kwa wananchi. “Ndiyo maana
tumepandisha bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 27 hadi asilimia 40.
Ole wake atakayepokea fedha hizi halafu zisifanye kazi yake, ukiipoteza
wewe utafute njia ya kwenda,” alisema huku akishangiliwa.
Akifafanua
zaidi, Waziri Mkuu alisema vita inayoendeshwa imelenga kuifanya
Tanzania ibadilike na itoke kwenye uchumi wa chini na kuingia uchumi wa
kati. “Swali la msingi ni je tunafikaje hapo? Jibu ni kupitia uzalishaji
wa bidhaa viwandani,” alisema.
“Nyote
ni mashahidi wa jinsi ambavyo shilingi yetu imekuwa ikishuka thamani
kulinganisha na dola ya Marekani. Tulitoka sh. 1,600/-, tukapanda hadi
sh. 1,900/- na sasa tumefikia sh. 2,180/-. Hii ni kwa sababu tunaagiza
zaidi bidhaa kutoka nje ya nchi badala ya kuzalisha, hatuwezi kuendelea
hivi na ndiyo maana tumeamua kuwa nchi ya viwanda. Leteni mitaji
nyumbani muwekeze,” alisisitiza.
Akijibu
swali kuhusu Serikali kutafuta njia ya kutoa mikopo kwa Watanzania
waishio nje ya nchi, Waziri Mkuu alisema mkopo ni mkataba kati ya
taasisi ya kifedha na mkopaji kwa hiyo Serikali haiwezi kubeba dhamana
hiyo. “Benki wanataka ijue taarifa zako mkopaji, wanataka wajua dhamana
zako ni zipi, wajiridhishe na shughuli unazofanya. Je panakopesheka
hapo?,” alihoji.
Hata
hivyo, aliwaeleza kwamba wakitaka kuwekeza nyumbani wanaweza kupata
mikopo kutoka benki ya maendeleo ya kilimo (TADB), Benki ya Rasilmali
(TIB Corporate na TIB Development). “Hizi benki ni za wakulima na
wajasiriamali, na zina masharti yake, kwa hiyo ni lazima wakakague eneo
lako au mahali unapofanyia biashara au wakague leseni yako na ukweli wa
maombi uliyopelekea. Sasa ukiwa Zambia watawezaje kukukopesha? Kwa hiyo
ukitaka fedha uwe nyumbani,” alisema.
Akijibu
swali ni vipi Serikali itawasaidia wanadiaspora kupiga kura kwenye
uchaguzi mkuu wakiwa nje ya nchi, Waziri Mkuu alisema Serikali haijawahi
kujaribu jambo hilo licha ya kuwa ilikwishapokea mapendekezo kadhaa
kutoka nchi mbalimbali lakini kwa vile wameliuliza, yeye analibeba na
kwenda kulifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment