Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari . Kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dkt. Rufaro Chatora
Taarifa kwa umma, kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu hapa nchini ni kama ifuatavyo; Tangu ugonjwa huu uanze, jumla ya watu 13,491 wameugua Kipindupindu, na kati yao jumla ya watu 205 wameshafariki kwa ugonjwa huu.
Katika kipindi cha wiki iliyoanza tarehe 04 hadi 10 Januari 2016, kumekuwa na jumla ya wagonjwa 615 walioripotiwa nchini kote na vifo vitatu (3). Mikoa ambayo bado imeripoti kuwa na ugonjwa huu ndani ya wiki moja iliyopita ni 11 kati ya 21 iliyokuwa imeripoti ugonjwa hapa nchini. Mikoa hiyo ni pamoja na Morogoro, Arusha, Singida, Manyara, Pwani, Dodoma, Geita, Mara, Tanga, Mwanza na Simiyu. Kati ya hiyo, mikoa inayoongoza kwa kuripoti idadi kubwa ya wagonjwa wapya ndani ya wiki moja iliyopita ni pamoja na Morogoro (Manispaa ya Morogoro 87, Halmashauri ya Morogoro 66), ukifuatiwa na Arusha (Arusha Manispaa 50), Singida (Iramba 40) na Manispaa ya Dodoma ( 33).
Aidha, mikoa iliyokuwa na maambukizi lakini kwa muda wa wiki moja iliyopita hakukuwa na mgonjwa yoyote wa kipindupindu ni pamoja na Mbeya, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kagera, Lindi. Vile vile mkoa wa Dar es Salaam ambako ndiko ugonjwa ulianzia na kudumu kwa muda wa miezi minne (4) haujaripoti mgonjwa wa kipindupindu kuanzia tarehe 22/12/2015.
Mikoa ambayo ilikwisha kuwa na ugonjwa huo lakini hapajakuwepo na wagonjwa wowote kwa muda wa zaidi ya miezi miwili iliyopita ni pamoja na Shinyanga, Kilimanjaro na Iringa. Pia mikoa ambayo haijawahi kutoa taarifa ya ugonjwa wa kindupindu tangu mlipuko huu uanze hapa nchini ni Njombe, Ruvuma na Mtwara.
Bado Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaendelea kusisitiza kuwa, ili kudhibiti ugonjwa huo na kuokoa vifo vinavyotokana na ugonjwa huu, wananchi wanasisitizwa kunywa maji yaliyo safi na salama, kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka:-
-kabla na baada ya kula
- baada ya kutoka chooni
-baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia
-baada ya kumhudumia mgonjwa
Aidha, jamii inaaswa kutumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, maziwa na mabwawa.
Hivyo, Mamlaka za Mikoa na Halmashauri pamoja na watendaji wake kote nchini zinaagizwa kuendeleza juhudi za kuzuia kusambaa kwa mlipuko pamoja na kuchukua hatua stahiki za tahadhari kwa kusimamia utekelezaji wa yafuatayo:
*Ushirikishwaji wa viongozi ngazi mbali mbali, hasa ngazi za Halmashauri kwa kushirikisha madiwani na viongozi wa kata, vijiji, na mitaa.
*Mamlaka husika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama ikiwa ni pamoja na uwekaji wa dawa ya klorini kwenye maji na kupima usalama wa maji mara kwa mara.
*Upatikanaji wa dawa za kutibu maji (Water Guard, Aqua Tabs) katika maeneo ya mlipuko.
*Juhudi kubwa ziongezwe kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya vyoo bora kwa kila kaya.
*Uelimishwaji wa Baba na Mama Lishe, na wauzaji wengine wa vyakula kuhusu kanuni za afya.
*Kusimamia utekelezwaji wa Sheria ya Afya ya Mazingira na Sheria ndogo ndogo (By-Laws).
*Uhamasishaji wa Wananchi wanaopata ugonjwa kuwahi kutumia maji ya chumvi chumvi (ORS) na kuripoti mapema katika vituo vya huduma.
*Uboreshwaji wa vituo vya kutolea huduma za afya.
Hitimisho
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inawashukuru wadau wote wanaoshirikiana na Serikali katika harakati za kupambana na ugonjwa huu. Aidha, Wizara inaipongeza mikoa ambayo ilikuwa na ugonjwa na sasa umetoweka au kupungua kwa kiasi kikubwa na pia kuikumbusha mikoa ambayo bado haijaathirika kuchukua hatua za tahadhari za kuzuia ili isipate mgonjwa yeyote wa Kipindupindu.
No comments:
Post a Comment