Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili
kushoto), akipata ufafanuzi kuhusu namna ya kuhifadhi makontena kutoka
kwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Aloyce Matei
(kushoto), mara baada ya kukagua Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Aloyce
Matei (wa tatu kushoto), huku Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Eng.
Edwin Ngonyani (wa pili kulia), akifatilia.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwa na
Naibu wake wakikagua mtambo wa kuchunguza makontena (scanner) katika
eneo la TPA.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua
mtambo wa madai na malipo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania alipotembelea
Mamlaka hiyo.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka
watumishi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufanya kazi kwa
uadilifu na uharaka wenye tija ili kukudhi matarajio ya wananchi katika
wizara hiyo.
Akizungumza
na watumishi wa wizara hiyo mara baada ya kuapishwa, Profesa Mbarawa
amesema kipaumbele chake kwa wafanyakazi hao ni kufanya kazi kwa
uadilifu, weledi na kwa kuzingatia matokeo chanya kwa haraka.
“Tuwe
tayari kubadilika, tufanye kazi ya kuwahudumia watanzania kwa moyo,
tuendeleze taswira nzuri ya Wizara kwani Wizara hii ina sifa nzuri tangu
ilipoanza hadi sasa’, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Profesa
Mbarawa amefafanua kuwa uwazi na uhusiano mzuri kwa wafanyakazi ni ngao
kubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo kati ya watendaji na
watumishi.
Aidha,
amewataka watendaji na watumishi wa Wizara hiyo kushirikiana na
kutokuwa wanyonge kutokana na mfumo wa mabadiliko ya kiutendaji wa
iliyokuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwani Wizara hizo
zina uhusiano mkubwa katika kumhudumia mwananchi hivyo kuungana kwake
kutaleta tija na ufanisi kwa haraka.
“Jambo
la msingi ni kufuata kanuni na sheria katika utendaji wenu pamoja na
kusimamia miongozo iliyopo, utendaji wenu lazima uwe na malengo
yanayotekelezeka kwa haraka”, amesema Prof. Mbarawa.
Akizungumza
na watumishi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Waziri huyo amehimiza
matumizi ya teknolojia katika huduma za bandari ili kuweza kuwahudumia
wateja kwa haraka hata wakiwa mbali.
Amewataka
watumishi wa bandari kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa ushindani ili
kuvutia wadau wengi kupitisha mizigo yao katika bandari za Tanzania.
“Fanyeni
kazi kwa maslahi ya nchi, acheni kufanya kazi kwa maslahi binafsi,
tambueni Serikali na wananchi wanahitaji huduma bora zitakazokuza uchumi
wa taifa kutoka katika bandari zenu”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Naye,
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Eng. Edwin Ngonyani
amewataka watumishi wa bandari kuacha tamaa, kuishi kwa uaminifu ili
kujenga taswira mpya ya taasisi hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa
taifa na jamii kwa ujumla.
Katika
ziara hiyo Waziri Mbarawa na Naibu Waziri Ngonyani waliambatana na
viongozi mbalimbali wa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment