Matukio: SAGCOT Yawataka wanaomaliza vyuo vikuu Kuchangamkia Ajira - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


25 May 2015

Matukio: SAGCOT Yawataka wanaomaliza vyuo vikuu Kuchangamkia Ajira

 Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mh. Dk. Rehema Nchimbi akifungua kikao kazi cha biashara ya kilimo kwa kongani ya Ihemi iliyoandaliwa na SAGCOT (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania) kwa ushirikiano na UONGOZI Institute (Taasisi ya Uongozi Afrika kwa Maendeleo Endelevu) mapema leo Iringa mjini. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Kilimo wa TCCIA Bi. Magadalena Mkocha, Mwenyikiti wa Bodi ya Agricultural Council of Tanzania Dk. Sinare Y. Sinare, DC wa Iringa Mh. Angeline Mabula, DC wa Mufindi Mh. Mboni Mhita na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Philemon Luhanjo.
Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT Bw. Geoffrey Kirenga akitoa utangulizi wa mada ya biashara ya kilimo kwa nyanda za juu kusini. Mkutano huo wa siku mbili ulikutanisha  viongozi wa serikali, sekta binafsi, mashirika ya kimataifa pamoja na wakulima kwa ajili ya kujadili kuhusu kuboresha biashara ya kilimo nchini kwa nyanda za juu kusini hususan kongani mwa Ihemi Iringa na Njombe.

                                >>>>>>>>>>>>>>>>> <<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<


SAGCOT yashika kasi kongani mwa Ihemi – Iringa na Njombe

Iringa, Tanzania: SERIKALI imewataka vijana wa mikoa wa Iringa na Njombe, wakiwemo wale wanaomaliza vyuo vikuu kuitumia kongani ya Ihemi katika Ukanda wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), kujiajiri.

Hayo yalielezwa juzi mjini Iringa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi wakati akifungua kikao cha kazi; cha biashara ya kilimo kilichoshirikisha viongozi wa serikali wa mikoa ya Iringa na Njombe, wakulima na wafugaji, wawekezaji na washirika wa mpango wa SAGCOT.

“Kongani ya Ihemi katika mpango huu wa SAGCOT inahusisha mikoa ya Iringa na Njombe, ina ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na ufugaji, tuazimie kuwashawishi vijana wanaodai kukosa ajira, kujiajiri katika kongani hii,” alisema.

Alisema vijana wanaweza kuitumia kongani hiyo kuwekeza katika kilimo na ili wafikie hatua hiyo ni muhimu viongozi wa kisiasa wa ngazi zote bila kujali vyama vya kisiasa wanavyotoka wakaelimishwa kuhusiana na mpango huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Bw. Geoffrey Kirenga alisema; “katika kikao hicho SAGCOT kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, wameangalia changamoto na yale yote yanayotakiwa kufanyika ili kuendeleza kilimo na ufugaji katika kongani ya Ihemi.”

Alisema mpango huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2011 unahusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Njombe na Katavi na umegawanywa katika kongani sita za Ihemi, Rufiji, Kilombero, Mbarali, Ludewa na Sumbawanga.

“Lengo ni kuona ifikapo mwaka 2030 zaidi ya Dola za Marekeni Bilioni 3.5 ziwe zimewekezwa katika ukanda huo na kati yake Dola Bilioni 2.4 zitokane na uwekezaji wa sekta binafsi na zinazobaki ziwekezwe na sekta ya umma katika miundombinu, mawasiliano na huduma za jamii,” alisema.

Alisema katika ukanda huo kuna zaidi ya watu milioni 12, wakiwemo wale wanaojishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara.

“Tangu tuanze uhamasishaji kuna ahadi ya Dola Bilioni Moja hadi sasa imeahidiwa kuwekezwa na sekta binafsi za ndani na nje; na mpaka sasa asilimia 30 ya fedha hizo uwekezaji wake unaendelea na serikali imeanza kutoa kipaumbele katika eneo hilo,” alisema.

Mbali na kuongeza ajira, alisema utekelezaji wa mpango  huo utawatoa wakulima katika kilimo cha kienyeji na kuwaingiza katika kilimo cha kisasa ili kufikia mahitaji ya soko.

“Kwa mfano katika soko la ndani kuna mahitaji makubwa ya viazi mviringo, matunda na mboga kama matofaa, maharage, shayiri na ngano na maziwa. Haya yote tunaagiza kutoka nje wakati yanaweza kuzalishwa kwa wingi katika Kongani ya Ihemi kwasababu ya hali yake ya hewa ya baridi,” alisema.

Akizungumzia mahitaji ya kiwanda chake, Meneja Masoko wa Kampuni ya Maziwa ya Asas ya mjini Iringa Bw. Roy Omolo alisema wanahitaji asilimia 80 ya maziwa kutoka kwa wafugaji wadogo ili kiwanda chao kifanye kazi kwa ufanisi lakini kiasi hicho hakifikiwi na hivyo kulazimika kuagiza kutoka mikoa nje ya Iringa na Njombe.

“Unaweza kuona jinsi ajira ilinavyoweza kupatikana katika sekta hii ya kilimo na ufugaji; viwanda vipo lakini havipati malighafi. Matarajio yetu ni kuona SAGCOT inawahamasisha wakulima kulima kisasa na kufuga kwasababu soko la bidhaa zitokanazo na mifugo lipo,” alisema.

Taarifa iliyotolewa katika kikao hicho inaonesha ifikapo mwaka 2030, zaidi ya hekta 350,000 zitakuwa zimeendelezwa katika ukanda mzima wa SAGCOT na matarajio yake ni kuajiri zaidi ya watu 420,000, wakiwemo vijana wanaomaliza vyuo vikuu.

Mbali na wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa ya Iringa na Njombe, wengine waliohudhuria kikao hicho kilichoshirikisha sekta ya umma na binafsi toka ndani na nje ya nchi ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo aliyeamua kujikita katika kilimo baada ya kustaafu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad