Balozi
Mpya wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Japan Balozi Batilda
Buriani akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alipofika kuaga rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na
Rais wa Jakaya Mrisho Kikwete.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkaribisha Balozi
Mpya wa Malawi Nchini Tanzania Bibi Hawa Ndolowe aliyefika Ofisini kwake
kujitambulisha rasmi.
Balozi
Seif akisalimiana na Gavana Mkuu wa Jimbo la Siustan na Balachestan
Nchini Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran Bwana Ali Osat Hashemi wakati
alipofika na ujumbe wake kwa mazungumzo ya uhusiano kati ya nchi hizo
mbili. Wa mwanzo kushoto ni Balozi Wa Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran
Bwana Mehdi Aghasafari na wa mwanzo kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya
Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Nd. Issa Ibrahim Mahmoud.
Balozi
Seif akibadilishana mawazo na Gavana Mkuu wa Jimbo la Siustan na
Balachestan Nchini Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran Bwana Ali Osat Hashemi
ambae yupo Zanzibar na Ujumbe wake kwa ziara ya siku mbili.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Jamuhuri
ya Kiislamu ya Iran ina wajibu wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar
katika harakati za maendeleo kutokana na Historia ndefu iliyopo ya
muingiliano wa kibiashara baina ya baadhi ya Wananchi wa pande hizo
mbili.
Gavana Mkuu wa Jimbo la Sistan na Balachestan Nchini Jamuhuri ya
Kiislamu ya Iran Bwana Ali Osat Hashemi akiuongoza Ujumbe wa Viongozi
saba wa Jimbo hilo alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar.
Gavana Ali Osat Hashemi alisema muingiliano huo wa biashara kati ya
Irani na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla umepelekea watu wa pande hizo
mbili pia kuwa karibu zaidi kwa kuchanganya damu.
Alisema wiki chache zijazo pande hizi mbili zinatarajia kusaini Mkataba
wa ushirikiano katika kuendeleza mradi wa mafunzo ya amali ambao
utagharimiwa na Iran kwa kiasi cha Dola za Kimarekani Laki 500,000
zitakazotumika katika ununuzi wa vifaa vya kufundishia.
Gavana huyo wa Jimbo la Sistan na Balachestan Nchini Jamuhuri ya
Kiislamu ya Iran alifahamisha kwamba sekta binafsi hasa miradi ya amali
inafaa kuungwa mkono kwa vile inasaidia kutoa ajira kubwa kwa Jamii hasa
Vijana.
Alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Iran
itaendelea kutoa fursa za masomo ya Elimu ya juu kwa Wanafunzi wa
Tanzania na Zanzibar katika vyuo vikuu mbali mbali vilivyomo nchini
humo.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alisema miradi ya Amali na Sekta ya Afya inayofadhiliwa na Iran
kwa Zanzibar ni uthibitisho wa uimarishaji wa uhusiano uliopo kati ya
pande hizo mbili.
Balozi Seif aliiomba Jamuhuri ya Kiislamu ya Irani kuendelea kuongeza
fursa za mafunzo kwa Vijana wa Zanzibar ili elimu watayoipata hasa
katika miradi ya amali iweze kusaidia kupunguza wimbi kubwa la ukosefu
wa ajira hapa Nchini.
Alieleza kwamba fursa za ajira bado zinaendelea kuwa changamoto kubwa
kwa Mataifa mbali mbali Duniani zikiwemo pia zile Nchi ishirini
zilizoendelea kiviwanda Ulimwenguni { yaani G 20 }.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikutana kwa
mazungumzo na Balozi Mpya wa Malawi Nchini Tanzania Bibi Hawa O.
Ndilole aliyefika kujitambulisha rasmi Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar.
Katika mazungumzo yao Balozi huyo Mpya wa Malawi Bibi Hawa Ndilole
alisema Historia kubwa ya Utamaduni na Elimu inayofanana kati ya Malawi
na Tanzania inafaa kuendelezwa zaidi kwa maslahi ya mataifa hayo mawili
jirani.
Bibi Hawa alifahamisha kwamba muingiliano wa mafunzo ya elimu ya juu
ambao unatoa fursa kwa wanafunzi wengi wa Malawi kupata elimu ya vyuo
vikuu nchini Tanzania ni moja kati ya uthibitisho huo wa uhusiano
mwema.
Naye Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa wataalamu wa kilimo wa Malawi na
Zanzibar kufanya utafiti wa pamoja kwenye sekta hiyo ili kusaidia kutoa
matunda bora yatakayoimarisha ustawi wa Wananchi wa pande hizo mbili.
Balozi Seif alisema Mataifa ya Bara la Afrika yamebarikiwa kuwa na
Utajiri mkubwa wa rasilmali tofauti zinazopaswa kufanyiwa utafiti wa
pamoja na wataalamu wazalendo wa Bara hili ili ziendelee kufaidisha Bara
hili.
Akizungumza na Balozi Mpya wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini
Japani Balozi Batilda Buriani aliyefika Ofisini kwake Vuga kumuaga rasmi
baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo Balozi Seif alimuomba Balozi
Batilda kuhakikisha kwamba Tanzania inafaidika kutokana na ushirikiano
wake wa Kidiplomasia ya Japan.
Balozi Seif alisema ipo miradi kadhaa ya maendeleo kama huduma za Umeme,
Maji pamoja na masuala ya kukabiliana na maafa na majanga
inayoendelezwa na Zanzibar ambayo imekuwa ikipata nguvu na ufadhili
katika utekelezaji wake kutoka Japan suala ambalo Balozi Batilda
atapaswa kulifuatilia ili kuona utekelezaji wake unafikia ufanisi
uliokusudiwa.
Alifahamisha kwamba kazi kubwa ya Balozi Batilda Buriani ambayo
amekabidhiwa na Taifa katika kusimamia Diplomasia ya Tanzania Nchini
Japan ni kuchangamkia fursa zote za Maendeleo ambazo zinaweza kuisaidia
Tanzania kupitia taasisi na mashirkia yote yatayokuwa ytayri kujitolewa
kusaidia nguvu zao.
Balozi Mpya wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Batilda Buriani amepata
uteuzi huo aliokabidhiwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Dr. Jakaya Mrisho Kikwete wadhifa ambao aliwahi kuutumikia kabla Nchini
Jamuhuri ya Watu wa Kenya.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment