Pichani
juu na chini ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu
akizungumza na katika mkutano uliohusisha wadau wa mashirika ya
Kimataifa na asasi za kijamii ukiwa na lengo la ushirikishaji wa jamii
katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori uliofanyika jana katika ukumbi
wa mikutano wa Mpingo House uliopo Wizara ya Maliasili na Utalii jijini
Dar es Salaam.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewji blog).
Na Modewji blog team
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema kama watanzania
wasiposhirikiana katika kudhibiti ujangili wa Tembo waliopo watatoweka
kabisa katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
Kauli
hiyo ameitoa jana kwenye mkutano wa ushirikishwaji wa jamii katika
masuala ya uhifadhi wa wanyamapori uliofanyika wizarani kwake.
“Uhifadhi kama tunavyoujua, hautaweza kufanikiwa kama kila mtu kwenye nchi hii atafikiria ni kazi ya serikali kuu peke yake.Na vilevile kama kila mtu atafikiria ni kazi ya wahifadhi peke yao”. alisema Nyalandu kwenye mkutano huo.
Nyalandu
alibainisha kuwa, majadiliano hayo, yatakuwa chachu kubwa ya maendeleo
katika wizara hiyo huku akiwashukuru wadau hao mbalimbali wakiwemo
wanahabari kwa kufika kwao, ili kuangalia suala la uhifadhi kwa mapana
yake.
Alisema
wakati ujangili wa Tembo nchini umeshamiri sana, wakati umefika kwa
watanzania kuhakikisha kwamba wanakomesha hali hiyo ili taifa kuendelea
kuwa na wanyama wake.
Alisema
mathalani Tembo katika hifadhi ya Selous wamepungua kutoka Tembo 38,975
katika sensa ya mwaka 2009 hadi Tembo 1,384 kwa sensa ya mwaka 2014 na
akasema kwa kasi hiyo katika miaka 10 ijayo Tembo Tanzania wataisha
kabisa.
“Hili
ni muhimu watu wakafahamu, upana wa hivi vita ni mkubwa kiasi gani na
watu wanaohusika ni wengi kiasi gani ndani na nje ya nchi," alisema
Nyalandu akiongeza kuwa mitandao ya kihalifu imetanda ulimwenguni kote.
Alisema suala la hifadhi halipo kwa wanyama pekee bali lipo katika upana wote na hata katika misitu.
Alisema
ili kukabiliana na ukatwaji hovyo wa miti kutoka katika misitu ya
miombo wanajipanga kuhakikisha kwamba miombo inayodaiwa kuingizwa nchini
kutoka Zambia inakamatwa ili kulinda miombo iliyopo magharibi ya nchi.
Akizungumzia
suala la mifugo na mbuga zinazopakana nazo amesema kwamba wanaanda
rasimu ya kuhakikisha kwamba kuna mahusiano mazuri kati ya wenye mifugo
na hifadhi wakiwa tayari kuyaachia baadhi ya maeneo kwa lengo la
kuhakikisha kwamba wafugaji hawaingizi mifugo yao katika hifadhi.
Aidha
amesema kwamba wanajipanga namna ya kuhakikisha kwamba hakuna mgongano
wa maeneo kati ya wanyama na binadamu na kwamba wanavijiji wanafundishwa
namna ya kuishi na wanyama katika maeneo yenye mwingiliano mkubwa.
Aidha
alisema kwamba meno ya Tembo kilo 1,763 yalikamatwa mwaka jana na
jitihada zinaendelea za kukabiliana na majangili kwa kutanua mtandao wa
kiintelejensia ndani na nje.
Alisema
kwa sasa wanamsaka raia wa China anayeshutumiwa kutorosha nyara za
serikali kwa kushirikiana na jeshi la Polisi la Kimataifa (Interpol).
Kwa nje ya nchi, meno ya Tembo yaliyokamatwa, Kilo 40 katika miji ya Hong Kong, China.
Aidha
alisema watuhumiwa 1,711, walikamatwa kuanzia Januari hadi Desemba
mwaka jana na kesi zao zinaendelea katika mahakama mbalimbali hapa
nchini. Pia silaha 85 zimekamatwa ikiwemo silaha za kivita ambazo
walikuwa wakizitumia mbugani.
Alisema ukichanganya na silaha zilizokamatwa kwenye operesheni tokomeza, jumla silaha 1,199 zimekamatwa.
Kwa
upande wake, Ali Said Mosee aliyehudhuria mkutano huo kutoka Tanzania
Association on Climate Change, alishauri ushirikishaji wa wadau
mbalimbali kutatua migogoro kwenye mipaka ya mbuga na pia mgongano wa
kimaslahi kati ya hifadhi na wanadamu.
Aidha
wadau walishauri Wizara kuhakikisha inapunguza misafara ya wanyama ya
kuhamahama kutoka sehemu moja hadi nyingine ikiwemo kwa kuzalisha miti
na mazao yanayopendwa na wanyama hao.
“Wanyama
wetu wanatakiwa wafanyiwe utafiti na kujua nini Nyati anapendelea kula
porini, basi wapande hiyo miti na vyakula vyake kwa ujumla hata kwa
Tembo hivyo hivyo.Wapande hiyo miti hapa hapa kwani hata siye binadamu
tunavyovyakula tunavyovipenda, naamini hata kwa wanyama ni hivyo hivyo,
rai yangu ni kuwa tufanye utafiti na kujua ili kuzuia misafara hii”
alisema Ali Said Mosee.
Tanzania
inahifadhi za taifa 16 na asilimia 40 ya ardhi ya nchi ni maeneo
yaliyohifadhiwa. Kati ya maeneo hayo yaliyohifadhiwa hadi mwezi uliopita
mwaka huu 2015, maeneo 19 yanamilikiwa na wananchi na yameshasajiliwa.
Pia alisema kwamba kuna mapori ya akiba, 28 nchi nzima.
“Watu
wengi wanadhani kwamba misitu yote inamilikiwa na serikali kuu. Ukweli
ni kwamba serikali kuu inamiliki asilimia 35 tu ya misitu ya nchi
yetu, misitu mingine yote inamilikiwa na vijiji, wilaya na watu
binafsi asilimia 7. " alibainisha waziri huyo.
Aliwataka
watendaji wa Serikali za mitaa kukabiliana na changamoto ya kutoweka
kwa kasi kwa misitu ili taifa lisitumbukie katika jangwa.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu akifafanua mazungumzo na
wadau wa mashirika ya kimataifa na asasi za kijamii ukiwa na lengo la
ushirikishaji wa jamii katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori
uliofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Mpingo House uliopo Wizara
ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam.
Naibu
Waziri wa Maliaisli na Utalii, Mahmoud Mgimwa akitoa salamu kwa wadau
wa taasisi za kirai. Kushoto Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro
Nyalandu.
Mratibu
wa Uhakiki wa Ubora kutoka Haki Elimu, Robert Mihayo akitoa maoni kwa
Waziri Mh. Nyalandu ambapo amemuomba kushirikisha wadau wa elimu katika
kutoa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori kuanzia ngazi ya elimu ya msingi
ili kuwaanda vijana ambao ni taifa la kesho.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Foundation for Civil Society, Francis Kiwanga akishiriki
kutoa maoni katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori pamoja na
kutokemeza ujangili wa Tembo.
Mwandishi wa gazeti la Daily News, Diriham Kimathi akiuliza swali kwa Waziri Nyalandu (hayupo pichani).
Pichani
juu na chini ni baadhi ya wadau kutoka asasi za kijamii na mashirika ya
kimataifa waliohudhuria mkutano ulioitishwa na Waziri Nyalandu ambao
umefanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Mpingo House uliopo ndani
ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
No comments:
Post a Comment