Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Musa Iyombe (kushoto), akimkabidhi zawadi
Mwakilishi Mkuu mpya wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) Toshio
Nagase (kulia) Ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Musa Iyombe akifurahi jambo na Ujumbe
kutoka wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) wakati ugeni huo
ulipotembelea ofisini kwake kwa lengo la kutoa pongezi za JICA kwa
Wizara ya Ujenzi kutokana na utekelezaji mzuri wa miundombinu ya
barabara.Picha na Habari kwa Hisani ya Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini-Wizara ya Ujenzi.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Musa Iyombe amelipongeza Shirika la
Misaada ya Maendeleo la Japan (JICA) kwa ufadhili wa miradi mingi ya
ujenzi wa miundombinu ya barabara iliyokamilika na inayoendelea nchini.
Eng.
Iyombe ametoa pongezi hizo leo jijini Dar es Salaam wakati akiagana na
Mwakilishi Mkuu wa JICA nchini Bw. Yasunori Onishi, ambae amemaliza muda
wake na kumpisha Mwakilishi Mkuu mwingine Bw. Toshio Nagase.
“Nafikiri
ninyi ni wa kwanza kufadhili miradi mingi ya ujenzi wa miundombinu ya
barabara nchini kwetu, kwani mmekuwa mkiahidi kufanya mambo mazuri na
kuyatekeleza kwa kipindi kifupi, hivyo sina budi kuwashukuru kwa
jitihada hizi”, alisema Eng. Iyombe.
Katibu
Mkuu ameongeza kuwa miradi mingi ya barabara ambayo inafadhiliwa na
JICA inaonekana kukamilika kwa wakati hivyo kutoa fursa za kimaendeleo
nchini.
Aidha,
Eng. Iyombe amefafanua kuwa Wizara ya Ujenzi itaendelea kushirikiana
kwa karibu na Shirika la JICA ili kuhakikisha miradi yote ambayo
wameiahidi kuitekeleza inafanyika na kumalizika kwa wakati. Awali,
akimkaribisha Mwakilishi Mkuu Mpya wa JICA nchini Bw. Toshio Nagase,
Katibu Mkuu ameahidi kuwa Wizara ya Ujenzi itatoa ushirikiano wa karibu
kwake kama ilivyokuwa inafanya kwa mtangulizi wake.
Kwa
upande wake Mwakilishi Mkuu wa JICA nchini aliyemaliza muda wake
Yasunori Onishi, amesema kuwa furaha yake ni kuona Tanzania inakuwa na
miundombinu bora katika ya sekta ya barabara ambapo amesisitiza kuwa
Shirika hilo linajikita katika kuhakikisha kuwa inajenga na kukarabati
barabara za miji, mikoa na zile zinazounganisha nchi.
Zaidi
ya miradi 26 ya barabara nchini imefadhiliwa na Shirika la maendeleo la
Japan (JICA) tangu mwaka 1980 hadi sasa, lengo likiwa ni kupunguza
msongamano na kuhuisha fursa za kiuchumi.
Baadhi
ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa daraja la Selander, ukarabati wa
barabara ya Makuyuni – Ngorongoro pamoja na ukarabati wa barabara ya
TANZAM katika eneo la Kitonga, ujenzi wa barabara ya Masasi- Mangaka,
Upanuzi wa barabara ya Bagamoyo eneo la Mwenge – Tegeta, ujenzi wa
daraja la Rusumo ambayo yote imekamilika.
Miradi
mingine inayotarajiwa kuanza kujengwa muda wowote ni upanuzi wa
barabara ya Gerezani, ujenzi wa barabara za juu (Tazara flyovers), na
ujenzi wa barabara ya Morocco- Mwenge itakayojengwa kwa njia nne.
No comments:
Post a Comment