Na Ferdinand Shayo wa Wazalendo 25 Blog ,Longido
Waziri wa Ardhi nyumba na makazi Wiliam Lukuvi ameiagiza Halmashauri ya wilaya ya Longido kuhakikisha kuwa wanapima ardhi pamoja na kupanga miji ili kuepukana na tatizo la ujenzi holela .
Aidha amesema kuwa miji inayokua inapaswa ipangwe mapema
ili kuepushwa suala la bomoa bomoa ambalo hujitokeza baadae na kuzua
migogoro.
Lukuvi ameyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mradi
nyumba za watu wenye kipato cha chini na cha kati unaotekelezwa na
shirika la nyumba la taifa (NHC) katika
wilaya ya Longido na kugharimu kiasi cha shilingi milioni 921.Lukuvi
amewaasa wakazi wa longido kuchangamkia fursa hiyo ya kununua nyumba
hizo bora kwa makazi ya watu.
Mbunge wa Longido Lekule Laizer amesema kuwa hitaji la
makazi bora kwa jamii ya wafugaji litafikiwa na mradi huo hivyo
amewashauri wafugaji kumiliki nyumba ili kujipatia heshima kwani
haiwezekani kuwa na maisha bila nyumba.
Katika Ziara hiyo Waziri
Lukuvi amewaagiza viongozi wa mila pamoja na viongozi wa kiserikali
kutatua mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Longido ,Monduli na Wilaya ya
Arusha ili kuepuka migogoro mbali mbali inayojitokeza na kuathiri
shughuli za kijamii.
Kwa upande wake Katibu tawala msaidizi ,miundombinu Hamdun
Mansour amesema kuwa migogoro mingi ya ardhi ni kati ya wananchi wenyewe
pamoja na ile inayohusisha wawekezaji na wananchi ,Mkoa umekua ukifanya
juhudi za kutatua migogoro hiyo ambayo wakati mwingine huathiri hali ya
amani.
Mkoa wa Arusha ni moja kati ya mikoa inayokabiliwa na
changamoto ya migogoro ya ardhi ambayo imekua ikiathiri amani na utulivu
pamoja na shughuli za maendeleo,utatuaji wa migogoro hiyo utaleta tija
kwa maendeleo na kudumisha amani.
No comments:
Post a Comment