Mwenyekiti
wa Mtandao wa Mashirika yanayofanya kazi na Watoto Tanzania ambaye pia
ni Mratibu Miradi, Kituo cha Watoto wa Mtaani cha Dogodogo Kigogo
(Dogodogo Centre Street Children Trust), Sabas Masawe.
MCHAKATO wa
kujadili na kuandika Katiba Mpya unaendelea bungeni mjini Dodoma, licha
ya kuwepo kwa mvutano na mgawanyiko wa makundi ya wabunge wa bunge
maalumu wanaojadili Rasimu ya Pili iliyowasilishwa kwao.
Wakati
hayo yakiendelea viongozi, wanaharakati na wadau wa watoto
wanapendekeza masuala ya haki za msingi za watoto yatambulike vizuri
katika katiba ijayo.
Mwenyekiti
wa Mtandao wa Mashirika yanayofanya kazi na Watoto Tanzania ambaye pia
ni Mratibu Miradi, Kituo cha Watoto wa Mtaani cha Dogodogo Kigogo
(Dogodogo Centre Street Children Trust), Sabas Masawe anashauri ibara ya
43 ambayo inataja haki za msingi za watoto iendelee kuwepo mpaka Katiba
inakamilika na iboreshwe zaidi katika mchakato unaoendelea Bungeni.
Nasema
haya maana tayari kuna baadhi ya watu wameanza kuhoji kwamba kwanini
hata watoto wanaingia kwenye katiba ilhali wao ni sehemu ya watu kama
wazazi wao. Anasema pamoja na kuingizwa kipengele cha mtoto kwenye
rasimu ya pili ya katiba bado kuna mambo ambayo wao kama wadau
wangependa yaingizwe tena hivi sasa katika mchakato wa majadiliano
unaoendelea.
Anasema
baadhi ya mambo hayo ni kama umri wa mtoto mwenyewe kutaja wazi kwamba
ni kuanzia umri gani. "...Unaweza ukaangalia hili ni suala la msingi
sana kutaja umri wa mtoto mwenyewe anayezungumziwa...kwa sisi wadau wa
watoto tunashangaa sana kwa maana nyingine tunaona suala hilo ni kama
linaongeza utata, kumuweka mtoto kwenye katiba ilhali umeshindwa
kumtambua (kiumri) mtoto ni yupi ni sawa na vichekesho...tunashauri
mtoto huyu umri utajwe wazi kuondoa utata...," anasema.
Mfano
ukisema wazee wana haki ya kutibiwa bure lazima useme huyu mzee
anaanzia umri gani na kuishia wapi. Huwezi kusema wazee watibiwe bure
alafu unashindwa kuainisha vitu vya muhimu kama umri wao, bila hivyo
utaleta mkanganyiko wa tafsiri...ndiyo maana hata sasa mtoto anayetajwa
tunataka tujue anaanzia umri gani na kuishia umri gani. Sasa hili pekee
linatushangaza watu wasomi wanajadili bila kuliona hili.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Fatma Mwasa akizungumza na mwandishi wa makala haya.
Huyu
mtoto akiingia kwenye mgongano katika sheria anashughulikiwa namna gani
kwasababu hili linaweza kuwa na mgongano kama pia litashindwa kutajwa
kwenye katiba chombo ambacho ni sheria mama ya nchi. Masawe anasema
mambo mengine ambayo yanatakiwa kuainishwa ni pamoja na kuelekeza namna
ya kuwawajibisha wazazi ambao wamekuwa wakikimbia majukumu yao ya kulea
watoto na kuwapeleka katika vituo vya yatima eti kwa madai wamewashinda.
"Hapa
tunataka ijulikane pia hawa wazazi ambao wamekuwa wakikwepa majukumu
yao wanawajibishwa vipi...maana wengine tunawapelekea mtoto wake
anatamka wazi kwamba mimi huyu mtoto amenishinda kabisa, sasa kama
amekushinda nani wa kukulelea? Sasa watu kama hawa lazima ijulikane
namna wanavyowajibishwa kwenye katiba au kama ni jukumu la Serikali
katiba ieleze wazi ili iwe rahisi kumbana mtu kisheria," anasema Masawe.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Jinsia wa Tanzania,
Anna Maembe, anasema Serikali inawapenda watoto na ndiyo maana katika
mchakato mzima wa kukusanya maoni ilizingatia kupata maoni ya kutosha
kutoka kwa watoto wenyewe pamoja na wadau wengine wanaotetea haki za
watoto.
Bi.
Maembe anasema Ibara ya 43 katika Rasimu ya Pili imeweka wazi haki za
watoto pamoja na kufafanua zaidi. "...Ibara ya 43(1) (a) na kuendelea
hadi (g) inaongelea kabisa na kufafanua kwa kina haki ya mtoto...hii ni
pamoja na kulindwa, kuelimishwa, kupatiwa huduma za afya na huduma
zingine zozote muhimu ambazo zitamfanya mtoto akuwe na kufikia utimilifu
ambapo naye awe mzalishaji na mwananchi mwema...," anasema Bi. Maembe
akizungumza na mwandishi wa makala haya.
Anasema
katika mchakato wa kukusanya maoni wadau wamepewa nafasi ya kutosha
katika kutoa maoni kwa ushirikiano na wabunge, wadau wengine wa watoto,
pamoja na mabaraza ya watoto ambayo yapo kila wilaya kutoa sauti za
watoto.
Anasema
anaamini ibara iliyopo sasa inayozungumzia haki za watoto itaboreshwa
zaidi mara baada ya mchakato kufikia mwisho hivyo kutoka na mwongozo
mzuri zaidi wa kutetea haki za kundi hilo la watoto.
"...Binafsi
mi bado naamini kuwa mchakato wa katiba, mi naomba niseme hivi mchakato
wa katiba ni nafasi nzuri sana ya kuweza kutetea haki za watoto wa
Tanzania, kwa kuwa mtoto wa leo ndiyo mbunge wa kesho, kwa hiyo
tusipoweka haki zake vizuri hata wabunge wetu wajao hawatakaa wakatimiza
wajibu wao vizuri...kwa kuwa sisi wote tulianzia utotoni hadi kufikia
hapa, kwa hiyo mchakato wa katiba ufanye mambo yote lakini haki za mtoto
zionekane vizuri ili sheria zote za nchi ziweze kupata mwongozo kutoka
kwenye katiba yetu inayokuja ambayo ni sheria mama kuweza kutoa haki kwa
mtoto. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Jinsia wa Tanzania, Anna Maembe akizungumza na mwandishi wa makala haya.
Hata
hivyo anasema mbali na haki za mtoto kuzingatiwa katika Katiba inayokuja
bado watoto wanapaswa kuzingatia kuwa haki inakwenda sawa na wajibu,
hivyo nao wanapaswa kutimiza wajibu yaani wasome kwa bidii, wakubali
kuelekezwa na sio wafanye mambo yao kinyume kwa kuwa wanajua haki zao
zimezingatiwa. Mkuu wa Mkoa wa Tabora Fatma Mwasa anaipongeza Serikali
kwa kitendo cha kutoa msukumo wa kipekee kwa kuwaingiza watoto katika
Katiba Mpya.
Anaongeza
kuwa Serikali ina kila sababu ya kufanya hivyo maana imeridhia mikataba
ya kimataifa kulinda haki za msingi za watoto, ambapo katika mikataba
hiyo imeainisha mambo ya msingi ya kuzingatia. Haki ya kuishi, haki ya
kupata elimu, haki ya afya haki ya kuudumiwa na kulindwa.
Anasema
kikubwa ambacho tukiweza kukifanya kikapitishwa katika katiba mpya
ambacho kitasaidia kuongeza hatua ambayo Serikali imefikia ni kiongeza
umri wa mtoto wa kike kuolewa. Akifafanua zaidi Mwasa anasema suala hilo
limekuwa na ajenda kwa muda mrefu hasa tunapopigania masuala ya
kijinsia, usawa na haki za watoto.
Anasema
eneo hili la umri wa kuolewa limekuwa likizua mkanganyiko kwa wengi kwa
kile upande mmoja sheria kuruhusu mtoto wa chini ya miaka 18 kuolewa,
licha ya upande mwingine bado sheria nyingine inamtambua mtu chini ya
umri wa miaka 18 ni mtoto.
"...Kimsingi
eneo hili limekuwa likizua utata kwa baadhi ya makundi katika
jamii...hasa baadhi ya viongozi wa dini wao wanasema mtoto wa Tanzania
anamaliza elimu ya msingi akiwa na miaka 14 na hapo kama hakufanikiwa
kuendelea na sekondari hubaki nyumbani bila kuwa na cha kufanya,
wanasema mtoto huyu anaweza kujiingiza katika mchezo mbaya kama atakaa
tu akisubiri umri wa kuolewa wao wanaona kama amepata wa kumuoa ni bora
akaolewa kuliko kujikuta akijiingiza katika mambo yasiofaa," anasema
Mkuu wa Mkoa huyo.
Anasema
hata hivyo anaishukuru Serikali kuleta shule za kata maana idadi kubwa
ya watoto sasa wanapata nafasi za kuendelea na masomo na kujikuta
wakiepukana na hatari za ndoa za utotoni, lakini pamoja na hayo anasema
bado kuna haja ya kujenga mfumo mzuri wa kuhakikisha suala la ndoa za
utotoni linatoweka kabisa. Pamoja na hayo anabainisha kuwa kuna haja ya
Katiba kutamka wazi kuwa mtoto asiruhusiwe kuolewa chini ya umri wa
miaka 18.
Akizungumzia
haki kwa makundi maalum ya watoto wakiwemo walemavu, anawashauri wazazi
wenye imani potofu kubadilika na kumchukulia mtoto mlemavu ana haki
zote kama ilivyo kwa watoto wengine.
Anasema
baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaficha watoto wenye ulemavu ili wasiweze
kupata haki zao ya msingi. "...Kwenye hili changamoto kubwa ilikuwa
wazazi wenyewe kufikiri kuwa kuzaa mtoto mwenye ulemavu ni jambo ambalo
linaleta fedheha, hii imekuwa ikisumbua sana maana wakati mwingine
tunabaini watoto wenye ulemavu wakiwa wamewekwa ndani wakati mwingine
kwa miaka kadhaa...sasa hili tunaamini sio haki maana mtu yeyote anaweza
kuwa mlemavu wakati wowote hata mimi sasa kumbagua juu ya haki kwa kuwa
yuko vile sio sawa hata kidogo," anasema Mwasa.
Bi.
Valerie Msoka ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake
(TAMWA), anasema ili mabadiliko katika jamii yatokee vyombo vya habari
vinahitajika sana na kwa namna yingine vinatoa mchango mkubwa. Anatolea
mfano kuwa kwa sasa matukio ya ndoa za utotoni bado yanashamiri kwa
baadhi ya mikoa kwa kiasi kikubwa.
Anasema
pamoja na vitendo hivyo kuendelea vyombo vya habari ndiyo nyenzo pekee
ambayo inaweza kubadili mtazamo katika jamii na matendo hayo kukoma
kabisa. Anasema mijadala inayoendelea kutoka kwa jamii na vyombo vya
habari kuendelea kuripo inasaidia wajumbe wa Bunge la Katiba kupata
taarifa za kina zaidi juu ya masuala mbalimbali wanayoyajadili hivi sasa
hivyo kuendelea kuboresha zaidi.
"...Mfano
masuala ya ndoa za utotoni yanayozungumzwa hivi sasa, ukeketaji na
masuala mengine ya unyanyasaji wanayofanyiwa watoto na vyombo vya habari
kuandika yanawasaidia wabunge kuwa naufahamu zaidi wanapochangia katika
kamati mbalimbali za Bunge la Katiba...kwa maana hiyo mchango wa vyombo
vya habari unaitajika sana," anasema Bi. Msoka. Bi. Valerie Msoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA).
Anasema
ili kuondoa utata juu ya umri wa mtoto; Katiba ijayo ingemsaidia mtoto
kutamka wazi kuwa mtoto wa kike au wa kiume haruhusiwi kuoa au kuolewa
akiwa chini ya miaka 18.
Anasema
hii ikitamkwa wazi watu wataelewa na hata utoaji elimu kwa jamii juu ya
umri wa mtoto na haki zake hauta kuwa wa mkanganyiko kama ilivyo sasa.
Anasema kwa sasa zipo baadhi ya mila zinashindwa kumlinda mtoto hasa wa
kike hivyo kujikuta wanaozeshwa na kukosa haki zao za msingi ya kupata
elimu, ilhali sheria zinashindwa kuwasaidia kwa kile nayo kuwa wa utata
juu ya umri wa kuolewa kwa mtoto.
Anasema
katiba mpya ikitamka wazi masuala hayo itakuwa rahisi kuwashughulikia
wanaotumia udhaifu wa sheria na kumnyanyasa mtoto. Hata hivyo anafafanua
kuwa pamoja na kuweka sheria ya kumlinda mtoto katika hali zote za
unyanyasaji bado jamii inatakiwa kupewa elimu ya kutosha juu ya kuziacha
mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zimekuwa zikimnyanyasa
mtoto hasa wa kike.
Mwanaharakati
huyu ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba anashauri elimu ya
kuanzia msingi hadi kidato cha nne itolewe bure na kwa watoto wote.
Anasema mtoto atatakiwa kusoma hadi kidato cha nne bure kama ilivyo
darasa la saba sasa kisha kuchujwa kidato cha nne.
"...Nasema
hivyo nikiwa na sababu kwamba ukiangalia mtoto anayemaliza elimu ya
msingi madarasa ambayo ni lazima kila mmoja apitie, wanamaliza wakiwa
wadogo sana, sasa kwa hali hii mi ninashauri kuanzia msingi hadi kidato
cha nne yangekuwa ni madarasa la lazima na bure ili watoto hawa wapate
elimu hadi kidato cha nne angalau hapa watakuwa wameongeza kitu kichwani
na miaka kusogea...," alisema.
Anasema
mtoto anayemaliza katika kidato cha nne angalau atakuwa amepata elimu
kiasi, anajitambua na umri umeongezeka kidogo hivyo kama wengine
wataishia katika darasa hilo wanaweza kujitegemea na hata walioolewa
watajitambua hivyo kujenga familia ambazo zinajielewa kwa kiasi fulani
tofauti na ilivyo kwa sasa.
Kwa
upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Watoto na Jinsia wa Tanzania,
Sophia Simba anasema takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ni kati ya nchi 20
Ulimwenguni ambazo zimekithiri kwa kuwa na ndoa za utotoni. Aidha
anabainisha kuwa takwimu pia zinaeleza katika kila watoto tano, wawili
kati yao wameolewa chini ya miaka 18.
"...Hili
ni tatizo kubwa sana, fikiria kwa kila watoto watano wasichana wawili
kati yao wameolewa chini ya miaka 18, sasa ukiangalia utaona karibuni
kila wakati kuna mtoto anaolewa Tanzania akiwa chini ya miaka 18.
Hili
Serikali haiwezi kukaa kimya ndiyo maana kuna programu mbalimbali
zinafanywa kukabiliana na hali hii...leo tumezinduwa kampeni za
kukabiliana na hali hiyo Mara tutafanya hivi maeneo mengine pia kupinga
suala hili," anasema Bi. Simba.
Pili
Muherisens (13) ni mwanafunzi wa darasa la tano katika moja ya shule za
msingi Wilayani Tarime. Binti huyu alilazimika kutoroka kwao na
kukimbilia eneo lingine akikwepa kukeketwa na wanaukoo kijijini kwao.
Mtoto
huyu wala wazazi wake wote hakupenda kukeketwa baada ya kuhofia madhara
ya tendo hilo lakini ukoo ulishinikiza na ukatishia kama wazazi watazuia
mtoto wao kufanyiwa hivyo wangeliwatenga na mama yake kupigwa. Hapo
ndipo binti alipoamua kukimbia kijiji na kwenda kwenye vituo salama.
Binti
huyu anaomba Serikali iwasaidie watoto kama hawa ambao hulazimishwa
kukeketwa na hata kuozeshwa mapema ikiwa ni vitendo vya unyanyasaji
dhidi yao. Cha kujiuliza ni watoto wangapi Tanzania ambao wanakumbana na
unyanyasaji wa nguvu kama huu. *Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment