SIASA : MHE. RIDHIWANI KIKWETE ATAJA 11 WATAKAOFAA KUGOMBEA KWENYE URAIS 2015 - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Monday, 14 July 2014

SIASA : MHE. RIDHIWANI KIKWETE ATAJA 11 WATAKAOFAA KUGOMBEA KWENYE URAIS 2015

Mbunge Wa Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete akiomba kura wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kuzindua kampeni za CCM uliofanyika kwenye Uwanja wa Miembe saba, Chalinze mkoa wa Pwani. Picha / Maktaba

Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ametaja majina 11 ya wanachama wa CCM wanaofaa kuwania urais kurithi kiti cha baba yake, Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake mwakani.
Ridhiwani (35), ambaye alishinda kiti cha ubunge wa Jimbo la Chalinze Aprili mwaka huu, alitaja majina hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.
Miongoni mwa aliowataja kuwa wana sifa ni makada watano walio chini ya uangalizi wa CCM wa mwaka mmoja baada ya kubainika kuanza kampeni za urais mapema, mawaziri wawili waliopoteza nyadhifa zao katika kashfa ya Operesheni Tokomeza, mwanamke mmoja na Rais wa Zanzibar.
“Kutaja majina tu, naweza kuorodhesha wengi tu. Naweza kuorodhesha hata watu 500, kwa sababu tunaona wengi sana,” alisema mtoto huyo wa Rais Kikwete ambaye amekuwa ndani ya CCM kwa muda mrefu akitokea umoja wa vijana wa chama hicho, UVCCM. “Kwa mfano, kwa upande wa Bara tunao Emmanuel Nchimbi, William Ngeleja, January Makamba, Bernard Membe, Steven Wassira, Edward Lowassa na Asha-Rose Migiro,” alisema.
Aliongeza: “Hawa ni kwa uchache zaidi… ni baadhi ya watu ambao wanatajwa kwa upande wa Bara, lakini jambo la msingi ni nani mwenye sifa za kuwa rais.”
Alisema pamoja na kwamba wanasiasa hao wote wanazo sifa za kuiwania nafasi hiyo ya juu, vikao vya chama ndivyo vitakuwa na nafasi ya kuwachuja ili kupata wanaotosha. “Kama wanatosha au la, vikao vya chama vitakaa kuamua licha ya kuwa hao wote niliowataja, kwa sifa za kugombea urais wote wanajitosheleza. Wana sifa, wana uwezo wa kugombea na wana uwezo wa kushinda, hao ni kwa upande wa Bara,” alisema.
Alipoulizwa hali ikoje kwa upande wa Zanzibar, Ridhiwani alisema, “Sisi chama chetu kina utajiri wa watu kwa upande wa Zanzibar kuna Shamsi Vuai Nahodha, Hussein Ali Mwinyi, Dk Seif Ally Iddi (Makamu wa pili wa Rais Zanzibar) na Dk Mohammed Ali Shein, Rais wa Zanzibar. Hawa ni watu ambao wana uwezo na hata wakipewa jukumu la kuongoza nchi hii wanaweza. Tunao wengi sana.”
Membe, Wassira, Lowassa, Ngeleja na Makamba walipewa adhabu na Kamati ya Maadili ya CCM ya kutogombea nafasi yoyote ndani ya chama wala kufanya kampeni baada ya kudaiwa kukiuka taratibu za chama hicho, wakati Nchimbi na Nahodha walilazimika kujiuzulu nyadhifa zao za uwaziri kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza ambayo ililenga kushughulikia majangili, lakini ikahusishwa na vitendo vya ukiukaji haki za binadamu.
Ridhiwani hakumtaja Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye ambaye pia anatumikia adhabu hiyo ya Kamati ya Maadili ya CCM.
Baadhi kukwama
Hata hivyo, Ridhiwani alidokeza kuwa wapo baadhi ya wanasiasa watakaokwama kufikia lengo hilo kutokana na kukabiliwa na kesi ndani ya chama, ambazo hakuzitaja wala kutaja wahusika.
“Kuna watakaopungua kutokana na kesi zinazowakabili katika chama ambazo zinawafanya wapungukiwe sifa. Kwa maana hiyo kuna watu kama wanne hivi (wa Bara) unawatoa na ukiwatoa unabakiwa na watatu, sasa unaweza kujiuliza hao watakaobaki watatu, je, wanatosha?”
Alipotakiwa kueleza iwapo angepewa nafasi ya kuteua mgombea mmoja wa CCM atakayepambana na vyama vingine katika uchaguzi mkuu mwakani, Ridhiwani alijibu kwa ufupi kuwa akisema, “Hilo siwezi kujibu.”
Amsaidia Membe
Ridhiwani pia alizungumzia uchaguzi wa ndani ya CCM akikiri kuwa alimsaidia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Membe kushinda ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
“Ni kweli katika uchaguzi wa NEC nilimsaidia Bernard Membe. Nilimsaidia si kwa sababu ya kuwa katika kundi lolote, ila nilimwona kuwa ana sifa ya kuingia kwenye NEC, hili jambo lazima watu waelewe,” alisema Ridhiwani.
Hata hivyo, Ridhiwani alieleza kukerwa na kitendo cha baadhi ya wajumbe ambao katika uchaguzi wa ndani badala ya kufanya kampeni kwa mtu wanayemtaka, wanafanya kampeni dhidi ya yule wasiyemtaka. “Hili ni jambo la ovyo ambalo nimewahi kuliona katika chama chetu… na tangu nimezaliwa sijawahi kuliona. Kwa mara ya kwanza nimekuja kuliona kwenye NEC,” alisema Ridhiwani ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
“Pale tunagombea nafasi kumi halafu kibaya zaidi ni kwamba watu wanakampeni ili mtu asipite. Ndiyo maana mimi nikasimama kuwaomba watu wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani tumsaidie Membe. Walionyesha ushirikiano wa kutosha na wakamchagua kwa kura nyingi na akaingia NEC. Mambo ya makundi mimi sina wala siasa yangu haiangalii kundi,” alisema.
Je, atamuunga mkono pia kwenye urais? Ridhiwani anasema: “Hapana. Hiyo siyo tafsiri sahihi. Naomba niseme jambo moja. Mmoja wa watu walionipigia kura Chalinze ni baba yangu, japo alisema amempigia kura mgombea wake, lakini nafahamu kuwa mgombea wake ni mimi kwa sababu ninatoka katika chama chake, hiyo ni tafsiri ya kawaida kulingana na maneno yake aliyoyasema.
“Baba yangu aliponipigia kura kuwa mbunge, kesho nitakapogombea nafasi ya uenyekiti wa CCM wa mkoa, mfano Mkoa wa Pwani halafu akanikataa, tafsiri haiwezi kuwa baba kamkataa mwanaye.”
Alisema jambo la msingi ni kuwa mtu anatosha katika nafasi gani, hivyo ikitokea Membe akawa katika nafasi hiyo na ana sifa kuliko wengine waliojitokeza, atamsaidia katika kuhakikisha anafanikiwa.
“Lakini ikitokea kwamba kuna watu wana sifa zaidi yake hatuwezi tukakubali kuipeleka hii nchi katika misingi ya kujuana. Tutaangalia mwenye sifa ni nani,” alisema kwa kujiamini.
Sifa za rais ajaye
Akizungumzia sifa za mtu atakayerithi kiti hicho, Ridhiwani alisema: “Matamanio yangu ni kumwona rais atakayefuata awe mtu mwenye uwezo wa kuendeleza pale Bwana Jakaya Kikwete alipoachia. Siyo rafiki yangu, mchumba wangu wala si mshikaji wangu wala mshiriki wangu katika baishara. La msingi ni mtu ambaye anaweza.”
Ridhiwani alisema ndani ya CCM kuna watu wengine ambao wana sifa na uzuri wa CCM haiangalii ni nani amejitokeza bali pia wanaangalia watu ambao wapo nje ya utaratibu wao, lakini ni makada wazuri ambao hata wakiletwa, wana sifa za kutosha.
“Ndiyo maana siwezi kujiingiza katika suala la kushabikia nani awe rais. Tutaangalia ni nani mwenye sifa atajitokeza na nani ambaye tukimuunga mkono anaweza kututoa hapa tulipo na kutupeleka kuzuri zaidi. Hakuna urafiki katika suala la nchi, tunaangalia masilahi ya nchi. Siyo masilahi ya nchi tu, ila masilahi makubwa ya nchi,” alisisitiza Ridhiwani.
Alisema pamoja na kwamba kwenye vitabu vya mwongozo zimetajwa sifa za mgombea urais, yeye binafsi akiulizwa sifa za rais anayetakiwa ni kuwa lazima awe mtu ambaye atakuwa sehemu ya kupata ufumbuzi wa matatizo na siyo sehemu ya walalamishi.
Alisema mgombea lazima awe mtu ambaye ukimwambia kwamba wananchi hawana chakula, atakuja na suluhisho ya nini kifanyike, ukimwambia shilingi imeshuka atakuja na ufumbuzi, akiambiwa kuhusu suala la ajira, atatafuta ufumbuzi na siyo na yeye kuwa sehemu ya walalamishi.
“Tunamtaka rais ambaye atatambua anaongoza watu gani kwa sababu tuna tatizo kubwa ambalo ni tishio kwa nchi yetu sasa, mgawanyiko wa madaraja katika maisha ya watu. Rais lazima ajue anaongoza watu wa namna gani. Wakati mwingine unakuwa na mtu ambaye anaangalia kundi la watu wake wanaomzunguka tu, akidhani kuwa ndiyo nchi, rais wa namna hiyo hapana,” alisema.
Aliongeza: “Rais ninayemtaka anapaswa awe mtu ambaye anaweza kushughulikia mambo yanayogusa maisha ya watu wote.”
“Pia, rais ninayemtaka lazima ajue misingi ya chama chetu. Tuna tatizo kubwa kwa wanasiasa wetu wa leo wengi hawafahamu nini umuhimu wa chama…Tuna wabunge wa CCM ndani ya Bunge ambao tangu wameingia bungeni ni miaka mitano, hawajawahi kuchangia chama.
Alisema katika hali hiyo, anahitajika rais anayefahamu kuwa chama kinatakiwa kisemewe na demokrasia ya chama lazima iwe kubwa. “Mfano watu wa CCM wanatakiwa kupewa uhuru wa kusema katika yale ambayo yanawafurahisha na yale ambayo wanaona hayafurahishi ili ituwezeshe sisi wanachama kubadilika. Mojawapo ya sifa ya chama ni kubadilika kutokana na wakati na mazingira ambayo ndiyo moja ya sifa ya chama na chama chetu sisi kimethibitisha hilo,” alisema.
Ridhiwani alisema ni vizuri apatikane rais ambaye ni muwazi katika demokrasia na atakayeweza kulinda usalama wa nchi hii kwa sababu nchi iko katika kipindi kigumu na kiongozi huyo awahakikishie wananchi kuwa anaweza kutengeneza nyanja mpya za watu kupata ajira.
Ajira 1,000,000 za JK
Ridhiwani, ambaye mwaka 2010 alikuwa mmoja wa wanachama wa CCM waliopewa jukumu la kuzunguka nchini kutafuta watu wa kumdhamini baba yake ili apitishwe kugombea tena kiti cha urais, pia alizungumzia ahadi ya Rais Kikwete ya ajira milioni moja, akisema kuwa imetimia lakini wapo watu wengine milioni tatu wasiokuwa na ajira.
“Tumeona hapa Rais Kikwete alipokuwa anaingia madarakani alituahidi ajira milioni moja, lakini mipango ya Serikali ikafungua vyuo vingi, leo hii ukihesabu ajira milioni moja kwa Serikali zimefika, lakini tuna wengine milioni tatu bado wapo benchi wanasubiri ajira,” alisema.
Aliongeza kusema: “Sasa tunafanyaje, huyu rais anayekuja lazima atupe ufumbuzi wa hilo. Siyo ufumbuzi wa kuangalia nyuma kwamba watu wanaohitaji chakula ni watu kumi, lakini huangalii kumi hao ambao baada ya kula watazaa, kwa hiyo kesho haitakuwa watu kumi, watakuwa zaidi ya watu 20.
“Hili ni jambo ambalo kwangu naona ni changamoto ambayo rais anayekuja lazima alitambue hilo. Pamoja na hilo rais anatakiwa pia awe na uwezo wa kutambua michango ya wenzake waliotangulia. Siyo shughuli kubwa ya rais atakayekuja iwe ni kuanza kukosoa wenzake kwamba huyu alifanya jambo la ovyo; hapana. Afanye kama vile ambavyo waliotangulia wamefanya,” alisisitiza.
Alitoa mfano wa jinsi marais walivyosahau ya nyuma na kusonga mbele.
“Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipomaliza muda wake alipokuja Mwinyi hakuangalia Nyerere alikosea wapi, alichoangalia ni kuwa nchi inakabiliwa na changamoto gani na tunakwendaje mbele.
“Ametoka Rais Mwinyi, akaja Mkapa ambaye pia aliangalia nchi inakwenda wapi, amekwenda mbele.
Akaja Rais Kikwete ameangalia nchi inakwenda wapi na akaendelea mbele. Hivyo rais anayefuatia lazima awe na uwezo huo. Aangalie mwenzake ameishia wapi na aendeje mbele. Yamefanyika mambo mengi nchini, ni vipaumbele vipi alivyonavyo. Lazima uwe na rais wa namna hiyo.
“Rais ajaye atambue watu katika matabaka yote. Tunao wafanyabiashara, wacheza muziki, waigizaji wa filamu hivyo lazima rais awatambue na lazima awe tayari kuwasaidia, atumie nafasi yake kuhakikisha kwamba watu hawa wanapatiwa haki zao.
“Rais ambaye anakuja lazima atambue watu katika kada mbalimbali. Mfano, waandishi wa habari wana malalamiko yao, lazima afungue mlango kwa kukutana nao na azungumze nao ili waseme shida zao kama suala la sheria. Hapa tunazungumzia muswada wa kuletwa bungeni, hiyo sheria tunafanyaje? Rais lazima atambue hayo.
“Rais lazima atambue juhudi zinazofanywa na wanamichezo wetu. Jinsi gani yeye anaweza kushiriki na kusaidia kunyanyua kile kiwango ambacho michezo yetu imefikia kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya michezo.”
Kuhusu jimbo lake la Chalinze, Ridhiwani alisema limekaa kwa miaka mitatu bila mtu wa kuwasemea kwa sababu mbunge wao, Said Bwanamdogo alikuwa mgonjwa na baadaye kufariki dunia. Hivyo anahitaji kutumia muda uliosalia kufidia pengo hilo.
“Mimi nimekuja humu ndani (bungeni) lazima nifidie ile miaka mitatu ya nyuma. Lazima tuikumbushe Serikali kwamba ilikuwa na mipango kadhaa kwa ajili ya jimbo la Chalinze na kwa nini haijatekelezwa hadi sasa.
Ile ya kuipa nguvu, tunaipa nguvu, zile za kushirikiana tunaangalia jinsi gani tunashirikiana,” alisema. 
Ridhiwani ana mpango wa kugombea urais? Je anamiliki mali gani usikose mfululizo wa habari hii. Itaendelea kesho. CHANZO MWANANCHI

KUELEKEA UCHAGUZI 2015...Ridhiwani ataja 11 wanaotosha kugombea Urais

Miongoni mwa aliowataja kuwa wana sifa ni makada watano walio chini ya uangalizi wa CCM wa mwaka mmoja baada ya kubainika kuanza kampeni za urais mapema, mawaziri wawili waliopoteza nyadhifa zao katika kashfa ya Operesheni Tokomeza, mwanamke mmoja na Rais wa Zanzibar.
“Kutaja majina tu, naweza kuorodhesha wengi tu. Naweza kuorodhesha hata watu 500, kwa sababu tunaona wengi sana,” alisema mtoto huyo wa Rais Kikwete ambaye amekuwa ndani ya CCM kwa muda mrefu akitokea umoja wa vijana wa chama hicho, UVCCM. “Kwa mfano, kwa upande wa Bara tunao Emmanuel Nchimbi, William Ngeleja, January Makamba, Bernard Membe, Steven Wassira, Edward Lowassa na Asha-Rose Migiro,” alisema.
Aliongeza: “Hawa ni kwa uchache zaidi… ni baadhi ya watu ambao wanatajwa kwa upande wa Bara, lakini jambo la msingi ni nani mwenye sifa za kuwa rais.”
Alisema pamoja na kwamba wanasiasa hao wote wanazo sifa za kuiwania nafasi hiyo ya juu, vikao vya chama ndivyo vitakuwa na nafasi ya kuwachuja ili kupata wanaotosha. “Kama wanatosha au la, vikao vya chama vitakaa kuamua licha ya kuwa hao wote niliowataja, kwa sifa za kugombea urais wote wanajitosheleza. Wana sifa, wana uwezo wa kugombea na wana uwezo wa kushinda, hao ni kwa upande wa Bara,” alisema.Hata hivyo, Ridhiwani alidokeza kuwa wapo baadhi ya wanasiasa watakaokwama kufikia lengo hilo kutokana na kukabiliwa na kesi ndani ya chama, ambazo hakuzitaja wala kutaja wahusika. CHANZO MWANANCHI
- See more at: http://adeladallykavishe.blogspot.com/2014/07/kuelekea-uchaguzi-2015ridhiwani-ataja.html#sthash.4rd2HIAt.dpuf

No comments:

Post a Comment