Mwl. Samwel Tupa akitoa hoja |
KOCHA maarufu wa riadha, Samwel Tupa, ameulalamikia uongozi wa Riadha Tanzania (RT), kwa kutumia jina lake kama kocha aliyeondoka na wanariadha waliokwenda nchini New Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya Jumuiya ya Madola yanayotarajia kufanyika Glasgow, Scotland, Julai mwaka huu.
Akizungumza na Tanzania Daima
kwa njia ya simu akiwa jijini Arusha, Tupa alisema hajui sababu iliyofanya
uongozi huo kufanya hivyo, na kwamba mara ya mwisho aliwasiliana na Katibu Mkuu
wa RT, Suleiman Nyambui, ambaye alimtaka wabaki ili waandae mashindano ya taifa
yanayotarajiwa kufanyika Juni.
“Nyambui aliponiambia hivyo,
nilimwambia mimi kama kocha siwezi nikabaki wakati wanariadha wangu wanakwenda,
huko watafundishwa na nani, akadai watakuwa na kocha wa China, lakini mimi
sikuafiki hilo na nikajua watakuwa wamebadilisha jina la kocha anayeenda, ila
cha kushangaza naona kwenye vyombo vya habari kwamba nimeenda huko,” alisema.
Alisema mbali na yeye kuachwa, pia
wamemuacha mwanariadha mwingine, Michael Damson, ambaye naye alikuwepo katika
orodha ya kwenda na aliambiwa apeleke pasipoti, ila kaachwa bila taarifa
yoyote.
“Baniani mbaya kiatu chake dawa na
kidole kidogo kinashika mpini wa jembe, lakini hakiingii kwenye bakuli ya
mboga, mimi siwezi kulalamika sana, lakini ninachohoji kwanini watangaze jina
langu kwamba nimekwenda wakati nimeachwa bila kupewa taarifa yoyote?” alihoji
kocha huyo wa kimataifa ambaye ni mkufunzi pekee Tanzania wa mchezo huo
aliyethibitishwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF).
Alisema kwa kuonyesha kwamba uongozi
huo unakubali kazi zake, waliamua kuondoka na mwanariadha wake, Michael Gwandu
bila kumpa taarifa na kuamua kuwasiliana na kocha msaidizi.
Alipotafutwa Rais wa RT, Anthony
Mtaka, alitaka atafutwe makamu wake, William Kallaghe, ambaye alidai
ahusiki na benchi la ufundi, hivyo atafutwe Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Ombeni
Zavalla, ambaye pia alisema anayejua utaratibu wa safari hiyo ni Nyambui, yeye
hajui lolote.
CHANZO: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment