UTAWALA BORA :UMUHIMU WA APRM KATIKA KUIMARISHA UTAWALA BORA NA UCHUMI TANZANIA - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Thursday, 3 April 2014

UTAWALA BORA :UMUHIMU WA APRM KATIKA KUIMARISHA UTAWALA BORA NA UCHUMI TANZANIA

 Viongozi wa Nchi za Kiafrika katika Makao Makuu ya AU.  Jumla ya nchi 34 kati ya 54 wanachama hai wa AU ni wanachama Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
Wajumbe wa Bodi na Sekretarieti ya APRM (Tanzania) wakiwa katika picha ya pamoja na Rais Dkt. Jakaya Kikwete. Kushoto kwa Rais ni Mwenyekiti wa APRM, Prof. Hassa Mlawa na kulia ni Katibu Mtendaji wa APRM, Bibi Rehema Twalib.



Na Saidi Mkabakuli

Tanzania, kama zilivyo nchi nyingi duniani kwa miaka mingi imekuwa mfuasi wa dhana ya usawa na haki ili  kuwa msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ili kutimiza matakwa ya demokrasia.
Hali hii imeifanya Serikali kufanya jitihada nyingi za kuboresha dhana hii licha ya changamoto nyingi zinazokinzana na juhudi hizi za serikali.
Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ufuasi wake kwa demokrasia na hasa suala zima la utawala bora, sio tu ilianzisha wizara maalum kwa ajili ya kusimamia utawala bora pia ilijiunga na Mpango wa Kujipima kwa kutumia vigezo vya Utawala Bora (APRM) kwa kuwasilisha rasmi maombi ya kujiunga na mpango huu tarehe 26 Mei, 2004 na kukubaliwa rasmi tarehe 8 Julai 2004, wakati wa Kikao cha Tano cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika.
APRM ni mpango wa hiari, uliobuniwa na viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika, kuziwezesha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, kujitathmini katika utendaji wa shughuli za serikali na shughuli zao nyingine kwa ujumla. Aidha mpango huu unalenga kuzipa nchi wanachama, fursa ya kujifunza kutokana na uzoefu na mafanikio ya nchi zingine za Kiafrika, na hivyo kuziwezesha nchi husika kuiga sera na mbinu muafaka zilizoleta mafanikio hayo kwa manufaa ya nchi zao. Kwa ujumla, ombi la kufanyiwa tathmini linapofanywa, linaashiria nchi husika kukubali kufuata misingi ya utawala bora katika uendeshaji wa siasa na shughuli za kiuchumi na wakati huohuo, kukubali kufanyiwa tathmini na Viongozi Wenza wa nchi za Kiafrika.
Hadi sasa nchi 34 kati ya 54 wanachama wa Umoja wa Afrika zimejiunga na mpango wa APRM. Mpango huo unahusisha uhakiki katika vipindi mbalimbali (periodic reviews) wa sera, kanuni na taratibu za utendaji zilizozoeleka (practice) ili kubaini maendeleo yaliyopatikana katika kutekeleza malengo yaliyokubaliwa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na utawala wa pamoja wa kibiashara kama ilivyoainishwa kwenye Tamko la Demokrasia, Siasa, Uchumi na Utawala wa Pamoja.
Chimbuko la APRM ni Mpango Mpya wa Maendeleo ya Afrika (New Partnership for Africa’s Development-NEPAD), ambao unalenga kuliondoa bara la Afrika kutoka kwenye lindi la umaskini, na kuleta maendeleo. NEPAD imeunganisha mipango ya maendeleo iliyobuniwa chini ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika, (OAU), na kuainisha ukosekanaji wa utawala bora kama mojawapo ya vikwazo dhidi ya maendeleo yanayolikabili bara la Afrika. Hivyo, ili kukabiliana na kikwazo hiki, viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika (UA) walitoa Tamko Kuhusu Demokrasia, Siasa, Uchumi na Uongozi Bora katika nyanja za uchumi na mashirika ya kibiashara. Tamko hilo pia linaainisha mkakati wa kufanikisha azma hii, kupitia demokrasia na utawala bora.
Lengo la msingi la APRM ni kuhimiza utumiaji wa sera, viwango na miendeno inayokubalika kitaalamu ili kujenga utengamano wa kisiasa, ukuaji chanya wa uchumi, maendeleo endelevu na kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda na hatimaye bara zima.
Pia, APRM inatoa fursa ya kuchangia katika kudumisha utengamano, kuleta maendeleo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kikanda kwa njia ya kubadilishana uzoefu na kuiga mifano bora ikiwa ni pamoja na kutambua udhaifu na kutathmini mahitaji ya kuongeza uwezo wa serikali na nchi.
Kwa kutambua umuhimu wa utawala bora, Mipango na mikakati mingi ya kimaendeleo na ile ya kupambana na umaskini imekuwa ikijumuisha kipengele cha utawala bora kama moja ya misingi ya kufikia malengo. Kwa mfano, moja ya misingi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo (TDV) 2025, kati ya misingi minne ya utekelezaji, unahimiza uimarishaji wa utawala bora na uongozi wa haki na kisheria ikiwa ni pamoja na jamii kukataa rushwa, kuimarisha mifumo ya uongozi na utawala ili kuweza kufikia malengo makuu ya Dira hiyo.
Pia, kwa upande wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA) I&II, sifa na misingi yake ni pamoja na Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini wa Mapato; Kuboresha maisha ya watu na Ustawi wa Jamii; na Utawala bora na uwajibikaji.
Suala kuu la msingi linalojitokeza katika kila Mkakati ni Utawala bora na uwajibikaji. Dhana hii ni msingi madhubuti katika kutekeleza mikakati hii yenye mkondo wa kiuchumi na mingine mingi inayotekelezwa na Serikali. Hivyo basi, umuhimu wa APRM katika mustakabali wa ustawi wa jamii ni chanya, kwa kuwa nchi inapata faida ya kujitathmini pale inapokosea. Hivi karibuni Katibu Mtendaji wa Mpango huu (APRM) nchini Tanzania, Bibi Rehema Twalib alitoa taarifa kuwa Tanzania ni moja ya nchi zinazofanya vizuri katika utawala bora Barani Afrika.
Akizungumzia umuhimu wa APRM katika kufikia lengo la msingi la mikakati hii, Bibi Twalib anasema kuwa ni muhimu kudumisha utengamano, ili kuleta maendeleo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kikanda kama njia ya kubadilishana uzoefu ili kuiga mifano mizuri kutoka nchi zilizopiga hatua kiuchumi.
Kwa mujibu wa Bibi Twalib, Tanzania imepata mafanikio katika maeneo ya Usimamizi wa Uchumi, Maendeleo ya Uchumi-Jamii Demokrasia na Utawala Bora, Siasa, Uendeshaji wa Kampuni na Masuala Mtambuka kama Afya.
Bibi Twalib alisema kuwa Tanzania kupitia APRM, imefanya tathmini yake katika maeneo hayo na kuwasilisha ripoti yake mbele ya wakuu wa nchi wanachama na kujadiliwa. Akizungumzia mikakati iliyopo katika kuhakikisha kuwa malengo ya APRM yanakuwa chachu ya kukuza uchumi wa nchi na kuleta maendeleo kwa jamii ya Kitanzania.
Bibi Twalib aliongeza kuwa APRM kupitia Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania inaendelea kuendesha tathmini ya utendaji wake na vyombo vyake kwa uwazi, ukweli na umakini, kulingana na vigezo vilivyowekwa kwenye Mpango wa Kujipima kwa kutumia Vigezo vya Utawala Bora.
“Kwa kutambua umuhimu katika kuimarisha utawala bora, Sekretarieti inaendelea kutekeleza Mpango kazi wa kitaifa wa kujitathmini katika masuala ya utawala bora (African Peer Review Mechanism - National Plan of Action, APRM-NPoA),” aliongeza Bibi Twalib.
Kwa mujibu wa APRM-NpoA, moja kati ya manufaa ya ya utekelezaji wa Mpango huu ni kubaini mambo mazuri juu ya utawala bora nchini Tanzania hali inayoongezea imani (confidence) wawekezaji toka nje ya nchi na wabia wa maendeleo. Hili moja ya mafanikio ya APRM, maana kwa mujibu wa takwimu kutoka Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) mpaka kufikia mwezi Desemba, 2013 kilifanikiwa kusajili miradi 9,442.
Hatahivyo, suala la kushirikisha wananchi ni suala lisiloepukika, ambapo, Bibi Twalib anahimiza suala la nafasi ya wananchi katika Mchakato huu. Bibi Twalib anasema kuwa, kwa kuwa APRM ina njema ya kupanua wigo wa demokrasia, na kuwapa wananchi kauli katika maamuzi yanayohusu mustakabali ya nchi yao.
“APRM Tanzania inategemea kuwa wananchi watatumia kikamilifu, nafasi inayotolewa ili kutoa tathmini yao ya kweli, kuhusu yale wanayoyaona kuwa ni mapungufu ya utendaji serikalini na mapungufu ya utawala bora nchini kwa ujumla, ili kuiwezesha serikali nayo kuyabaini mapungufu hayo na kuyachukulia hatua muafaka” anasihi Bibi Twalib.
Anaongeza kuwa ikiwa wananchi watatumia vyema fursa hizi vizuri, ndipo malengo ya kuanzishwa kwa Mchakato huu yatakapotekelezwa na kuwezesha kutimia malengo na misingi ya mikakati ya Serikali ya kuivusha Tanzania kutoka dimbwi la umaskini.

No comments:

Post a Comment