Miundombinu : Naibu Waziri, Kwandikwa Amwagiza CHICO Kujenga kiwanja cha Ndege, Shinyanga. - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


19 Oct 2017

Miundombinu : Naibu Waziri, Kwandikwa Amwagiza CHICO Kujenga kiwanja cha Ndege, Shinyanga.



Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Bi. Josephine Matiro (Watatu kushoto), alipofika mkoani humo kukagua maendeleo ya kiwanja cha ndege cha Shinyanga kilichopo eneo la Ibadakuli.

Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga, Bw. Julius Misollow akitoa taarifa ya maendeleo ya kiwanja hicho kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa, alipofika kiwanjani hapo kujionea maendeleo yake.

Muonekano wa kiwanja cha Ndege cha Shinyanga ambacho kinatatrajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami na Mkandarasi wa Kampuni ya ujenzi ya kichina ya CHICO.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa akizungumza na wananchi wa Mwigumbi mkoani Shinyanga, alipofanya ziara ya kukagua barabara ya Mwigumbi – Maswa (KM 50.3), inayounganisha mkoa wa Shinyanga na Simiyu.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani Simiyu, Mhandisi Albert Kent, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa kazi za ujenzi zinazoendelea katika barabara ya Mwigumbi – Maswa (KM 50.3).

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya kichina ya CHICO alipokuwa akikagua barabara ya Mwigumbi – Maswa (KM 50.3) inayounganisha mkoa wa Shinyanga na Simiyu.

Muonekano wa Barabara ya Mwigumbi – Maswa (KM 50.3), inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi CHICO kutoka nchini China. Barabara hii inaunganisha mkoa wa Shinyanga na Simiyu.Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mheshimiwa Elius Kwandikwa, amemtaka Mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya kichina ya CHICO aliyepewa zabuni ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Shinyanga kufika eneo la mradi na kuanza ujenzi wa kiwanja hicho haraka iwezekanavyo.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya kiwanja hicho katika eneo la Ibadakuli leo, mkoani Shinyanga, Naibu Waziri Kwandikwa, amesema kuwa haoni sababu ya mkandarasi huyo kuchelewa kuleta vifaa vyake katika eneo la mradi hadi sasa wakati tayari mkataba wa kuanza kazi hiyo umeshasainiwa.
"Mkandarasi hana sababu ya kuchelewa kuanza kazi wakati fedha zipo na zimeshatengwa kwa ajili ya mradi huu na mkataba umeshasainiwa, sasa namwagiza mkandarasi huyu kuleta vifaa vyake na kuanza kazi mara moja", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.


Aidha, Naibu Waziri huyo amemtaka Meneja wa kiwanja hicho kuhakikisha anatoa ushirikiano na kumsimamia mkandarasi huyo ili kuhakikisha kiwanja hicho kinakamilika mapema nakwa viwango vinavyotakiwa.
"Naamini tukimsimamia vizuri mkandarasi huyu tutapata kiwanja kizuri na imara hapa Shinyanga na tutafungua fursa mbalimbali za kiuchumi katika mkoa huu", amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.
Kwa upande wake, Meneja wa kiwanja cha ndege cha Shinyanga, Julius Misollow, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kutoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo atakapowasili eneo la mradi.
Amefafanua kuwa mradi huo unatarajiwa kuhusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, jengo la abiria, maeneo ya maegesho ya ndege na mnara wa kuongozea ndege.


Ameongeza kuwa ujenzi wa kiwanja hicho kwa kiwango cha lami chenye urefu wa kilomita mbili unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni 49.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa, amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mwigumbi - Maswa (KM 50.3), mkoani Simiyu na kumsisitiza mkandarasi anayejenga barabara hiyo kuikamilisha kwa wakati na kwa viwango.


Amesisitiza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo ambayo ni kiungo kwa wananchi wa Maswa, Bariadi, Lamadi na Mwanza, kutarahisisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo katika maeneo hayo.


Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani Simiyu, Mhandisi Albert Kent, amesema kuwa mradi upo katika hatua nzuri na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili kutoka sasa.
Naibu Waziri Kwandikwa amefanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Shinyanga na Simiyu ambapo amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad