Matukio : Mahakama Kuu Tanga Yajipanga Kumaliza Kesi - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


25 Apr 2017

Matukio : Mahakama Kuu Tanga Yajipanga Kumaliza Kesi



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga
Mhe. Imani Abood Muonekano wa majengo ya Mahakama Kuu
kanda ya Tanga baada ya kukamilika kwa ukarabati

Na Lydia Churi- Mahakama


Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/16-2019/2020) pamoja na Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama, imepania kuhakikisha kuwa kesi zote za zamani pamoja na zile zinazosajiliwa zinamalizika ili wananchi waweze kuwa na kujenga imani zaidi na chombo hicho muhimu cha utoaji wa haki nchini. Katika kulitekeleza hili, ipo mikakati iliyowekwa na Mahakama kwa ujumla na ile inayowekwa na kila Kanda ya Mahakama Kuu nchini.


Mikakati ya Mahakama ni pamoja na Majaji na Mahakimu kupangiwa idadi ya kesi watakazotakiwa kuzisikiliza na kuzimaliza katika kipindi cha mwaka mmoja. Kila Jaji amepangiwa kumaliza kesi 220 kwa mwaka na kila hakimu anatakiwa kusikiliza kesi 250 kwa mwaka. Mkakati mwingine wa jumla ni kiwango cha muda kilichopangwa kwa kesi kukaa Mahakamani, mathalani, Mahakama ya Tanzania imepanga kuwa kesi zote zilizosajiliwa Mahakama Kuu zisikae Mahakama kwa muda unaozidi miaka miwili wakati katika Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na zile za wilaya imeamuliwa kesi isizidi miezi 12 Mahakamani. Kesi katika Mahakama za Mwanzo inatakiwa kumalizika katika kipindi cha miezi sita.


Aidha, Mahakama imeanzisha utaratibu wa kufanya vikao na wadau wake ili kujadili namna ya kumaliza kesi kwa wakati kama moja ya mikakati yake ya kuhakikisha kesi zote za zamani zinamalizika Mahakama na pia kesi zinazosajiliwa zinamalizika kwa wakati ili kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuwapatia wananchi wa Tanzania Haki sawa na kwa wakati.


Pamoja na kuwepo kwa mikakati ya Mahakama ya kumaliza kesi zilizoko Mahakamani, Mahakama Kuu kanda ya Tanga nayo imejiwekea mikakati yake ili kuhakikisha inaenda sambamba na kasi ya Mhimili huo ya kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati kwa kumaliza kesi zao kwa wakati.



Akizungumzia suala la kumalizika kwa kesi kwa wakati, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga Mheshimiwa Imani Abood alisema kanda yake imepanga kuwanunulia Mahakimu wake wote (68) kompyuta Mpakato (Laptops) zitakazowasaidia katika kurahisisha kazi zao na kuondosha mashauri kwa wakati katika Mahakama mbambali za mkoa wa Tanga. Alisema lengo ni kuhakikisha Mlundikano wa kesi zilizopo Mahakamani unaisha na pia kesi zinazosajiliwa zinamalizika kwa wakati.


Jaji Mfawidhi alifafanua kuwa kompyuta hizo zitawasaidia waheshimiwa Mahakimu katika kuandika hukumu ili wananchi waweze kupati haki kwa wakati. Aliongeza kuwa hivi sasa Mahakimu wa mahakama za Mwanzo huandika hukumu kwa kalamu na baadaye hukumu hizo hupelekwa kwenye mahakama za wilaya ambapo kuna umeme kwa ajili ya kuchapwa na baadaye hurudishwa kwenye kwenye Mahakama za Mwanzo.


Alisema pia kanda yake inakabiliwa na uhaba wa watumishi hasa Makatibu Muhtasi pamoja na vitendea kazi jambo ambalo limekuwa likichelewesha utolewaji wa hukumu pamoja na upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wakati. Aliongeza kuwa kwa Mahakimu kupatiwa kompyuta hizo kutarahisisha upatikanaji wa haki.

Pamoja na kuwapatia Mahakimu Kompyuta, Jaji Abood alisema Mahakama Kuu Kanda ya Tanga inao mpango wa kuhakikisha inazipatia umeme baadhi ya Mahakama za Mwanzo kupitia Mradi wa Umeme vijijini (REA) ili kurahisisha upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wakati. Na hivi sasa tayari Mahakama za Mwanzo tano zimeshapatiwa umeme.




Jaji Abood aliitaja mipango mingine iliyowekwa na Kanda yake katika kuitekeleza nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania ya kuwapatia wananchi haki kwa wakati kuwa ni kuwapeleka Mahakimu wenye kesi chache kwenye Mahakama zenye kesi nyingi na upungufu wa Mahakimu ili kuhakikisha mashauri yote ya muda mrefu yanaondoshwa na yaliyofunguliwa yanamalizika kwa wakati.


Aliitaja mikakati mingine waliyojiwekea ili kuondosha mlundikano wa kesi Mahakamani kuwa ni pamoja na Majaji na Mahakimu kugawana idadi sawa ya Mashauri yaliyopo Mahakamani, kutenga vipindi maalum vya kumaliza kesi zote, Mahakimu wenyewe kufanya kazi ya kuchapa hukumu ili kesi zimalizike kwa wakati na kufanya vikao na wadau ili kuweka mikakati ya kumaliza kesi kwa wakati.


Kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania kwenye kanda ya Tanga, Jaji Mfawidhi alisema kuwa utekelezaji wa Mpango huo unaendelea vizuri baada ya kuwa wamejiwekea mikakati ya utekelezaji. Alisema hivi sasa kuna mageuzi makubwa kwenye Mahakama za Mwanzo hasa zile zenye umeme. Nakala za hukumu zinapatikana kwa wakati (ndani ya siku 21) na, mienendo ya kesi ndani ya siku 90 ikiwa ni pamoja na kesi kumalizika kwa wakati.


Kuhusu maendeleo ya Mradi wa kupambana na Rushwa ndani ya Mahakama (STACA), Jaji Mfawidhi anasema Mradi huu wa Mahakama ya Tanzania umeleta mageuzi makubwa ndani ya Mahakama hasa Kanda ya Tanga kupitia vifaa vilivyosambazwa (pikipiki, baiskeli mabango na simu).


Alisema kuwa suala la mapambano dhidi ya Rushwa ndani ya Mahakama linatiliwa mkazo na Mahakama Kuu kanda ya Tanga. Watumishi wa kanda hii wamekuwa wakikumbushwa mara kwa mara juu ya kufuata maadili katika kazi zao na kuepukana na vitendo vya rushwa. Alisema kufuatia mabango yaliyosambazwa na Mahakama katika Mahakama za Mwanzo zote, Mahakama za wilaya, mahakama ya |Mkoa, mahakama kuu, ofisi za halmashauri na ofisi za wakuu wa wilaya, jamii imeanza kubadilika kimtazamo kuhusu Mahakama akisema hivi sasa malalamiko yamepungua kwa kiasi kikubwa katika kanda yake.


Taarifa ya malalamiko ya mwezi Februari 2017 inaonyesha kulikuwa na malalamiko 3 tu kwa kanda nzima ikilinganishwa na malalamiko 11 yaliyokuwepo kipindi cha mwezi Januari, 2017 na malalamiko 15 katika kipindi cha mwezi Septemba, 2016. Kusambazwa kwa vifaa kama vile Pikipiki na Baiskeli kumesaidia Mahakamu kuweza kutembelea Mahakama za Mwanzo zenye idadi kubwa ya kesi na kuzimaliza hivyo kusaidia kumaliza mlundikano wa kesi.


Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga, Afisa Utumishi wa Kanda hiyo, Farid Mnyamike alisema hivi sasa wanaendelea na ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo ya Magoma iliyoko Korogwe pamoja na ukarabati wa jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Old Korogwe. Alisema kazi hiyo inafanywa na mkandarasi, SUMA JKT ambaye kwa sasa amefikia zaidi ya asilimia 70 ili kukamilisha kazi hiyo. Mkandarasi alikabidhiwa kazi hiyo Februari 2, 2017 na anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu alipokabidhiwa. Aidha, Mradi wa Ukarabati wa majengo ya Mahakama Kuu tayari umekamilika na majengo yalishakabidhiwa kwa Mahakama ya Tanzania.


Mahakama kuu kanda ya Tanga pamoja na kanda nyingine zinakabiliwa na tatizo kubwa la kuwa na miundombinu mibovu hasa kwa upande wa majengo ya Mahakama nyingi za Mwanzo. Mahakama Kuu kanda ya Tanga inayo majengo 68 ya Mahakama ambapo Mahakama 30 ndizo zinazofanya kazi wakati 12 ni zile zinazotembelwa na Mahakama 26 hazifanyi kazi kabisa.


Katika kutatua tatizo la ukosefu na uchakavu wa majengo ya Mahakama nchini, Mahakama ya Tanzania inatarajia kukamilisha miradi ya ukarabati na ujenzi wa majengo 70 ya Mahakama katika kipindi cha miaka miwili ili kusogeza karibu huduma ya utoaji haki kwa wananchi. Majengo tisa ya Mahakama kuu yanatarajiwa kujengwa na kukamilika katika mikoa tisa ndani ya kipindi cha miaka miwili.


Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya siku ya Sheria nchini, Kaimu jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Profesa Ibrahim Juma alisema Mahakama sita za Mikoa zitajengwa ndani ya miezi 6-12 wakati Mahakama za Wilaya 19 na za Mwanzo 36 zinatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2017.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad