Matukio : Waziri Mkuu, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa afungua mkutano wa 'Africa World Heritage' , Jijini Arusha - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


1 Jun 2016

Matukio : Waziri Mkuu, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa afungua mkutano wa 'Africa World Heritage' , Jijini Arusha


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea Vitambu kutoka Rais wa Bermuda Emmissions Control Limited, Bw. Donal Smith katika mkutano wa 'Africa World Heritage' alioufungua kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Mei 31, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe wakati alipomkaribisha kufungua Mkutano wa "Afrca World Heritage' kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Mei 31, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua mkutano wa 'Africa World Heritage' kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Mei 31, 2016. Kulia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumaane Maghembe.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa wa' Africa World Heritage ' wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua mkutano wao kwenye kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Mei 31, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano wa 'Africa World Heritage' baada ya kuufungua kwenye kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Mei 31, 2016. Kulia kwake ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na kushoto ni Mkuu wa Arusha, Felix Tibenda.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wasanii waliojitokeza kumlaki wakati alipowasili kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kufungua mkutano wa 'Africa World Heritage' mjini Arusha Mei 31, 2016. Kulia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wataalamu wa mambo ya malikale na uhifadhi wa urithi asilia (natural heritage) watafute mbinu zitakazoimarisha utunzaji wa rasilmali hizo bila kuathiri mifumo ya uchumi ya nchi zinazoendelea.
Ametoa wito huo leo (Jumanne, Mei 31, 2016), wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa siku nne unaojadili Uhifadhi wa Urithi wa Dunia wa Afrika kama Nyenzo ya kuleta Maendeleo Endelevu ulioanza leo kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Waziri Mkuu amesema kuna baadhi ya nchi ambazo ni maskini sana lakini zimebarikiwa kuwa na rasilmali kama madini na gesi asilia lakini kwa sababu rasilmali hizo ziko karibu sana na vivutio vya urithi asilia wa dunia, watu wa nchi hizo wanazuiwa kuchuma rasilmali zao ili wasiharibu vivutio hivyo.
“Tunatambua umuhimu wa kutunza rasilmali na vivutio vya urithi asilia. Hivi ni kwa nini zisitafutwe teknolojia zinazofaa ambazo zitaruhusu uvunaji wa gesi asilia na madini bila kuathiri uhifadhi wa vivutio vya urithi asilia wa dunia (world heritage sites)?”, alihoji Waziri Mkuu.
“Serikali za nchi za Kiafrika zinahitaji suluhisho kama hili wakati zikiendelea kutafuta njia sahihi za kuwianisha uhifadhi wa vivutio vya urithi wa dunia na changamoto ya kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake,” amesema.
“Sisi viongozi ambao wengi wetu ni wanasiasa, hatukatai ushauri wa wataalamu lakini tunawasihi baadhi yenu ambao mnashiriki mkutano huu muhimu, mtafute njia mbadala za kufumbua tatizo hili badala ya kuendelea kutegemea njia za kizamani za kukabiliana na changamoto kama hizi ili sote tuweze kunufaika na rasilmali zilizopo ikiwa ni pamoja na kutunza vivutio vya urithi asilia wa dunia,” aliongeza.
Amesema kama rasilmali hizo zitachambuliwa vizuri na kwa njia sahihi bila kuathiri vivutio vya urithi wa dunia, ni dhahiri kuwa zitaingiza mapato ambayo kiuchumi yatasaidia kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi ambao pia watasaidia kwenye uhifadhi wa vivutio hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilmali nyingi zikiwemo za ardhini (madini), misitu, wanyama na maeneo ya kihistoria na kusisitiza kuwa Watanzania wana jukumu la kuzilinda ili zilete tija kwa wananchi wote.
“Tukizitunza rasilmali zetu zitasaidia kupata mapato kutokana na utalii Serikali itapeleka sehemu ya mapato haya katika miradi mbalimbali na hivyo kuchangia kwenye pato la Taifa,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na UNESCO hasa katika masuala yanayohusu uhifadhi wa vivutio vya dunia kutokana na umuhimu wake kwenye maendeleo endelevu.
Alisema wizara yake imelenga kusimamia, kuendeleza na kuimarisha utunzaji wa maliasili na uhifadhi wa vivutio asilia na vya kiutamaduni (natural and cultural heritage) kwa kushirikiana na wadau wengine hapa nchini.
Naye Mkurugenzi wa Uhifadhi Malikale wa UNESCO, Dk. Mechtild Rossler aliwataka washiriki wa mkutano huo kutoka nchi mbalimbali duniani wawe tayari kupitia upya shughuli zinazotekelezwa katika eneo la urithi wa dunia na kuangalia wajibu wa nchi za Kiafrika katika kuandaa mwelekeo wa miaka ijayo.
Alisema katika miaka 40 ya utendaji wa UNESCO, idadi ya vivutio vya urithi wa dunia imeongezeka na kufikia 89 ambapo kati ya hivyo viko baadhi vinakavyobiliwa na changamoto ya kufutika kutokana na athari za kigaidi, matukio ya kivita na kazi za kibinadamu.
“Vivutio 16 kati ya 48 viko katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara na hivi vinakabiliwa na tishio la kupotea kutokana na vita, harakati za kigaidi na shughuli za kiuchumi za kibinadamu zikiwemo uchimbaji wa madini na gesi asilia,” alisema.
Aliwataka washiriki wa mkutano huo wakumbuke kuwa vivutio vya urithi wa dunia ni vielelezo vya jamii na pia huchangia uchumi kwa kutoa ajira kwenye jamii husika.
Mkutano huo unaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 150 kutoka nchi mbalimbali duniani, unajumuisha washiriki kutoka nchi 36 zikiwemo nchi 12 ambazo ni za nje ya bara la Afrika.

Waziri Mkuu amerejea mjini Dodoma mchana huu kuendelea na vikao vya Bunge.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad