Matukio : Mambo Machache Muhimu Kuyajua Baada Ya UK Kuamua Kujitoa Kwenye EU - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


26 Jun 2016

Matukio : Mambo Machache Muhimu Kuyajua Baada Ya UK Kuamua Kujitoa Kwenye EU



Na Jeff Msangi , Canada,
Mapema hii leo dunia imeamka na habari kwamba kutokana na kura za maoni zilizopigwa katika nchi zinazounganisha Ufalme wa Uingereza (United Kingdom-UK) wananchi wameamua kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (European Union-EU) ambao una jumla ya nchi 28. Hakuna nchi ambayo imewahi kujitoa kwenye umoja huo.UK inakuwa ya kwanza.
Swali la kwenye kura hizo za maoni lilikuwa jepesi tu; Tubakie Au Tujitoe? Asilimia 51.9% wamesema Tujitoe na asilimia 48.1% walisema Tubakie. Kwa mujibu wa taratibu za kidemokrasia wengi wanapewa. Hivyo kura ya kujitoa ikashinda.

Kwanini UK wanataka kujitoa EU?
Masuala ambayo yamekuwa mbele katika mjadala huu ni masuala ya Uhamiaji (immigration) na kujitawala (sovereignty). Hivi karibuni pameibuka mfumuko wa wahamiaji kutoka nchi kama Libya,Syria, na mataifa ya kwenye ukanda wa Jangwa wa Sahara ambao wanakimbilia Ulaya kutokana ugumu wa maisha na machafuko yanayoendelea. UK wanasema mfumuko huo wa wakimbizi unaathiri huduma zao za kijamii kama vile afya,makazi nk.
Pia UK wanasema kwa kuendelea kuwa kwenye Umoja wa Ulaya, wanashindwa kujitawala. Wengi wameielezea siku ya jana kama siku ya kupata Uhuru. Kwa hiyo waliokuwa wanaunga mkono hoja ya kujitoa walisisitiza kwenye masuala haya mawili makuu bila kusahau kauli mbiu za “Kulinda Mipaka” kama ambavyo mgombea wa Urais nchini Marekani, Donald Trump, amekuwa akihubiri. Habari za UK kujitoa zimemfurahisha Trump. Anaamini USA nao wataamua kupitia mfumo huo huo wa kujitawala na kulinda maslahi ya nchi yao.

Kwanini Dunia Imeshtuka?
Dunia imeshtuka kwa mambo mawili makuu. Kwanza iliaminika kwamba pamoja kura ya Tubakie itashinda. Wapiga turufu za kisiasa waliamini kwamba ingawa matokeo yatakuwa yamekaribiana sana, Tubakie ingeshinda.
Mawaziri wakuu wote wa Uingereza waliopita waliunga mkono hoja ya kubakia. Pia viongozi kadhaa duniani akiwemo Rais Barack Obama wa Marekani, Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau na wengineo waliwasihi waingereza wabakie. Wachumi waliobobea kama bilionea George Soros walitaka UK ibakie. Superstars kama David Beckham pia. Yote haikusaidia. Polls zilionyesha kwamba Tubakie ingeshinda. Mambo yamekwenda tofauti.
Kingine kilichoipeleka dunia kwenye hali ya mshangao ni masoko ya fedha,hisa na mitaji. Paundi ya Uingereza imeporomoka hivi leo kuliko ambavyo imewahi kutokea kwa miongo kadhaa. Kawaida matukio ya kidunia kama haya husababisha mtikisiko kwenye masoko ya fedha na mitaji. Kutulia au kutotulia hutegemea na jinsi viongozi wa kisiasa na wawekezaji wanavyoitikia kinachotokea.
Ndio Kusema Kuanzia Leo UK Wameshajitoa?
Hapana. Mchakato wa kujitoa unaweza kuchukua hata miaka 5. Kwa hiyo kwenye masuala yanayohusu Umoja wa Ulaya yanabakia hivi yalivyo wakati mchakato huo wa kujitoa unapoendelea. Mojawapo ya hatua ni kwamba nchi inayojitoa kuwaeleza wenzao kwenye umoja huo kwa mujibu wa  kifungu/kipengele  cha 50 cha mkataba uliounda umoja huo kilichoingizwa mwaka 2007 kufuatia Mapatano ya Lisbon.
Wataalam mbalimbali wa masuala ya sheria wanasema kifungu hicho ni kigumu kueleweka (pengine kwa makusudi au kwa sababu hawakuwahi kuwaza habari za nchi mwanachama kutaka kujitoa). Lakini kinaainisha kwamba kujitoa kwa UK kutategemea majadiliano lukuki.Nchi inayotaka kujitoa italijulisha Baraza Kuu la Jumuiya juu ya nia yake na kisha majadiliano yatafuata. Unaweza kukisoma kifungu kizima hapa.
Umoja wa Ulaya umesema mapema hivi leo kwamba ungependa hili suala la UK kujitoa lifanywe haraka iwezekanavyo hata kama kutakuwa na maumivu makali. Ndio mambo ya kutumbua majipu haraka haraka.Kitu kinachofanya mchakato huu kuchukua muda mrefu ni mikataba ya kibiashara, kiutendaji na hususani mambo ya kodi,ushuru na ushirikiano mpya wa soko huria.
Ufaransa imeshasema wataufanya mchakato wa UK kujitoa kuwa mgumu. Hawajafurahi. Kuna hisia kwamba Ujerumani na nchi zingine zitafuata mkondo wa Ufaransa. Jumamosi hii nchi waanzilishi wa umoja huo za  France, Germany, the Netherlands, Luxembourg, Italy na Belgium zinakutana kujadili hiki kinachoendelea.
Waziri Mkuu wa Uingereza,David Cameron ameshatangaza kujiuzulu kufuatia kushinda kwa kura ya maoni iliyotaka UK kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (AP Photo/Matt Dunham)
Waziri Mkuu wa Uingereza,David Cameron ameshatangaza kujiuzulu kufuatia kushinda kwa kura ya maoni iliyotaka UK kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (AP Photo/Matt Dunham)

Kujitoa Kwa UK kuna athari gani za kiuchumi?
Kwa ujumla wachumi wengi wanakubaliana kwamba kujitoa hakutoisaidia UK kama inavyodhania. Leo wanasema kuporomoka kwa paundi na mtetereko kwenye masoko ya hisa ya London hivi leo ni chachu tu ya yanayokuja. Hata hivyo waliosema Tujitoe akiwemo Meya wa zamani wa London, Borris Johnson anasisitiza kwamba rabsha itakuwepo lakini kwa muda mfupi tu. Wanasema UK itakuwa na nguvu zaidi baadae kwa sababu biashara zake na bidhaa zitakuwa hazipitii kwa mtu wa kati (EU) kama ilivyo hivi sasa.
Kingine muhimu kukiongelea ni kwamba kuna hofu kwamba baada ya UK kujitoa, huenda nchi zingine nazo zikaiga. Kuna hofu ya kufa kwa EU…baada ya muda. Binafsi naamini kuna nchi zitajitoa. Lakini pia kuna nchi zitajiunga.

UK ipo salama?
UK inaunda na nchi kadhaa ikiwemo England,Scotland, Wales na Northern Ireland. Kura ya maoni ya kujitoa au kubakia imeonyesha wazi kwamba Scotland walitaka kubakia. Kwa miaka kadhaa Scotland wamekuwa wakitaka kujitoa kwenye UK. Tayari viongozi wa Scotland wameshaanza kuongelea suala la kura nyingine ya maoni ya kujiondoa UK. Kwa hiyo UK kama ilivyo huenda ikakabiliwa na kumomonyoka kutokea ndani. Lakini bila shaka wapigaji kura wa Tujiondoe na viongozi wao tayari wameshalipigia mahesabu hili. La sivyo “dhambi” ya kujitoa itawarudia UK haraka sana. Northern Ireland nao wameshaanza kuzungumzia mkakati wa kura ya maoni ya kujitoa UK na kisha kujiunga tena na EU.

Ilikuwaje Mpaka Wakaamua Kupiga Kura Ya Maoni?
Lilikuwa ni dukuduku la wananchi na baadae likawa ahadi ya kisiasa. Waziri Mkuu David Cameron, ambaye alitaka UK ibakie na ambaye ameshatangaza kwamba ataachia ngazi ndani ya miezi mitatu ijayo, aliliweka kwenye ilani ya uchaguzi ya chama chake cha Conservatives kwenye uchaguzi mkuu uliopita. Ilikuwa ni jitahada yake ya kuwavutia wanachama wa chama cha UKIP ambao ndio walikuwa wanaongoza wazo la kujitoa. Kwa hiyo kimsingi David Cameron aliyataka mwenyewe. Ahadi ni ahadi.

Sasa Waingereza Watahitaji Viza Kutembelea Nchi Zingine za Ulaya?
Kama nilivyosema hapo juu, mchakato wa kujitoa ni mrefu. Bila shaka baada ya kujitoa na kama hakutokuwa na makubaliano ya ziada kati ya UK na nchi zingine, ndio watahitaji viza na kufuata taratibu zingine za kawaida za uhamiaji. Lakini kama ambavyo nchi nyingi hivi sasa zinaweza kutembeleana bila viza(mfano Canada na USA kwa raia), UK itabidi kuingia mikataba mingine ya ziada kwenye suala la uhamiaji.

Waingereza Wataruhusiwa Kufanya Kazi Kwenye Nchi Zingine Za Ulaya?
Inawezekana. Na kama nilivyosema hapo juu, watalazimika kama nchi au muungano kuingia mikataba na mijadala mingine. Bado UK kuna watu wataendelea kufanya kazi kama raia wa kigeni. Ni masuala ya makubaliano kati ya nchi na nchi.

Hali Hii Ina Athari Zipi Kwa Africa?
Athari za kiuchumi ni wazi zitakuwepo. Kujitoa kwa UK kwenye EU kwanza kunamaanisha aliyekuwa akitupigia upatu kwa muda mwingi,hayupo tena. Kihistoria UK alikuwa mtetezi mkubwa wa Africa kama makoloni yake ya pia Umoja wa Nchi Za Madola.
Tayari fedha ya Afrika Kusini,rand ambayo ndio inatumika zaidi kimataifa kutokea barani Afrika imeshakumbwa na msukosuko mapema hivi leo. Nchi nyingi za Afrika zinafanya biashara na UK. Kwa hiyo kama UK itaingia kwenye recession(hata ya muda) mwangwi utasikika kote barani Afrika.
Isitoshe mikataba mingi ya kibiashara kati ya Afrika na UK kimsingi ni mikataba ya EU na Afrika. Yote itaanza mchakato wa kupitiwa upya. Itachukua muda kurekebisha mambo. Tujiandae. Matumaini yaliyopo ni kwamba kupitia Umoja wa Nchi Za Madola, UK itaelekeza nguvu zake huko. Kwa hiyo baadae huenda pakawa na mwanga. Itategemea pia na sisi tunawekaje sera zetu za kiuchumi. Ila ni wazi kwamba kwa wakati huu UK haitoipa Afrika kipaumbele mpaka hapo watakaporekebisha mambo mengine.
Mbali na athari za kiuchumi kuna masuala ya uhamiaji. Kwa sababu UK wamejitoa wakianisha uhamiaji kama mojawapo ya changamoto kubwa walizonazo, ni wazi kwamba waafrika waliopo UK hivi sasa au wanaotaka kutembelea UK watakabiliwa na mshikemshike ya ziada ya aidha kutafuta viza, au vibali vya kufanya kazi nchini humo,kusoma nk.
 Imeandikwa kwa msaada wa tovuti na vyombo mbalimbali vya habari

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad