Kilimo Kwanza : Ujasiriamali ndio njia pekee ya kujikomboa kiuchumi - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


26 May 2015

Kilimo Kwanza : Ujasiriamali ndio njia pekee ya kujikomboa kiuchumi


Mradi wa Kilimo cha Tangawizi wa kikundi cha ujasiriamlai chaushindi kilichopo katika kijiji cha Mkongotema kata ya Mkongotema tarafa ya Madaba Halmashauri ya Songea.

Na Benjamin Sawe.

Katika ulimwengu wa sasa wenye changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira na ushindani wa kila namna ujasiriamali unabaki kuwa dhana pekee inayoweza kuwakomboa vijana kiuchumi na kuwawezesha kutimiza malengo na ndoto walizonazo.

Kutokana na kukithiri kwa idadi kubwa ya vijana wanaohitimu katika ngazi mbali mbali za elimu hasa elimu ya  msingi,sekondari na Chuo  ile hali hawana ajira na kuishia kukaa mitaani kutokana na elimu waliyoipata iliwaandaa kuajiriwa maofisini na sio kujiajiri,ni ukweli usiopingika kwamba elimu ya ujasiriamali inahitajika kwa kiasi kikubwa ili kuleta ukombozi wa kweli wa kiuchumi.

Mafanikio ni shilingi yenye pande mbili kuajiriwa na kujiajiri ,vijana wasifikiri kuwa kuajiriwa ndio njia pekee ya kufanikiwa  pia wajue  kuwa kuna mafanikio ya kiuchumi nje ya ajira na haya ni kwa wale walioamua kujiajiri kwa kuanzisha miradi mbali mbali ama biashara na huo ndio ujasiriamali wenyewe.

Vijana wengi wamekuwa wakihuzunika, kunung’unika na kulalamika kana kwamba waliambiwa maisha ni rahisi. Wakati unapoukubali ukweli ya kuwa maisha ni magumu, ndiyo wakati ambao maisha hayawi magumu tena! Ndiyo! Kwa sababu ukijua maisha ni magumu lazima utaishi kwa nidhamu kubwa, na nidhamu ndiyo msingi namba moja wa kutatua matatizo yote katika maisha.

Ukiona unalalamika kuwa maisha ni magumu, rejea katika fikra zako, huenda bado hakujafanyika mapinduzi! Ukiona unaukubali ukweli kuwa maisha ni magumu na wakati huo huo huna nidhamu, ama una nidhamu chache, basi ujue kuwa hujaukubali ukweli wote kuwa maisha ni magumu!

Ujasiriamali kwa ujumla ni dhana ambayo ili kukubalika kikamilifu, kunahitajika mapinduzi makubwa ya fikra kwa vijana kuliko elimu ya kawaida. Fikra za kuwatazama wajasiriamali waliofanikiwa na kutoa visingizio kuhusu mafanikio yao, ni fikra zenye matege na ukilemaa na hizo kamwe haziwezi kutufanya tukafanikisha kujikwamua kiuchumi.

Kutokana na hali hii, utagundua kuwa tatizo linalowakabili vijana wengi wa Tanzania katika kujikwamua kiuchumi si mitaji wala ukosefu wa elimu, bali ni la kifikra.

 Ili kijana aweze kufanikiwa kubuni na kuanzisha mradi, anatakiwa aamini kuwa kujiajiri kuna tija kubwa sawa na kuajiriwa. Kwa sababu ni mara chache mtu anaweza kuwa tajiri kwa kutegemea mshahara wake pekee!

Ni vema vijana wote wafahamu kuwa “fedha ni mawazo.” Kama fedha ni mawazo basi kujikwamua kiuchumi ni mawazo pia. Kama ni suala la kuwaza, kwa nini asiye na elimu asiwaze? Kama ujasiriamali unaanza na mawazo, kwa nini wenye elimu walilie mitaji? Sikatai kuwa mitaji ni suala la msingi katika ujasiriamali, lakini ifahamike kuwa uthubutu wa kuanza na kujaribu wazo hata kwa sehemu ndogo ndiyo msingi wa mafanikio ya mjasiriamali yeyote.

Nchi ya Tanzania ina ajira na fursa nyingi za kiuchumi za kumtosha hata mtoto atakayezaliwa kesho! Sioni sababu ya mhitimu wa darasa la saba kukosa ajira, kwanini mhitimu wa kidato cha nne na sita wakose kitu cha kufanya chenye kuwakwamua kiuchumi katika nchi tajiri kama Tanzania? Kwa wale ambao ni wahitimu wa vyuo vya kati na vya elimu ya juu, sioni haja ya kuwaandikia kwa sababu inatosha sana kwao kutengeneza ajira kwa wengine.

Tatizo jingine linalowasibu vijana wengi wa Tanzania kiasi cha kushindwa kupoka (seizing) fursa za kijasiriamali na fikra potofu za kutaka kuanza na mafanikio. Kama ni kijana msomi anawaza kuanza na kampuni yenye mtaji wa mamilioni. Yatatoka wapi mamilioni bila kuanza na kidogo? Kwa wale ambao hawana elimu kubwa wengi wamevia kimawazo kwa kuota kuokota fedha ama kuokota elimu!

Kama ulikosa elimu hupaswi kulalamika wala kunung’unika kwa sababu huko ni kupoteza muda, bado unayo nafasi kubwa ya kufanikiwa. Fikra za kupata vya bure bila kuhangaika ndiyo zinazosababisha Watanzania wengi kujiingiza katika michezo mingi ya bahati nasibu kwa matarajio kuwa watatoka! Cha ajabu ni kuwa michezo hiyo, ama mingineyo inawapotezea fedha badala ya kuwasaidia, hapa yanahitajika mapinduzi ya kifikra.

Maisha bora na ya uhakika kwa vijana yanawezekana ikiwa kutafanyika mageuzi makubwa katika sekta binafsi, ujasiriamali. Ili ujasiriamali ufanikiwe na kufanywa na vijana kwa uhakika, lazima vijana wote wakubali kufanya mapinduzi ya fikra zao za kitegemezi.

Tukisema ujasiriamali hatumaanishi ujasiriamali wa kujikwamua wewe kijana peke yako, bali tunagusa pia katika utanuzi wa fikra za kuanzisha kampuni, huduma na bidhaa mbalimbali zenye ubunifu mpya kwa kuvitumia vipaji kikamilifu.

Vijana wengi wamekuwa wakilalamikia ugumu wa maisha na kuacha kujishughulisha na ujasiriamali hivyo kupelekea kukabiliana na ugumu wa maisha.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Ester Riwa akitoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana wa mkoa wa Ruvuma anasema vijana wengi nchini wamekuwa wakitaka kupatiwa pesa bila kuzingatia mafunzo ya elimu ya ujasiriamali hivyo kupelekea upotevu na usumbufu katika urejeshaji wa marejesho.

Anasema baadhi ya vikundi vya vijana katika Halmashauri mbalimbali wamekuwa wakigomea mafunzo ya ujasiriamali na kudai posho za mafunzo na kusahau mafunzo wanayapatiwa ni muhimu kuliko hiyo poshowanayodai.

Bi Riwa anasema Serikali haitoi posho za mafunzo ya ujasiriamali bali hutoa elimu na baadae kutoa mikopo kwa vikundi vilivyosajiliwa kisheria.

Kaimu Mkuu wa Mkoa Mh.Norman King anasema Serikali imeamua kutoa mafunzo kwa vikundi vya vijana ya jinsi ya kuandaa maandiko ya miradi mbalimbali, uongozi bora na stadi za maisha ili kuwatoa katika mitazamo hasi kwenda mitazamo chanya kwa kutumia fursa zilizopo.

Anasema vijana wengi wanafursa mbalimbali za kujikwamua na umaskini lakini hawatumii fursa hizo vizuri na kubakia wakikaa vijiweni bila kujishughulisha na kazi yeyote na kuishia kuvuta madawa ya kulevya na kuwa wezi.

Nea Diwani wa kata ya Matimila jimbo la Peramiho Mh. Menesi Komba amesema mafunzo ya kujengewa uwezo ni fursa kwa vijana wa Halmashauri ya Songea kwani watakuwa wamepewa uelewa mkubwa wa jinsi ya kuendesha shughuli zao za ujasiriamali kwa ufanisi na utaalamu
Anawaasa vijana kutekeleza elimu ya ujasiriamalikwa vitendo kwa kuwafundisha vijana wenzao ambao hawakupata bahati ya kuhudhuria katika mafunzo hayo na kuachana na tabia ya kuwa wabinafsi wa kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vingine.

Tubadili mitazamo ya kuwaona ni sehemu ya matatizo katika jamii bali tuwaone kama ni sehemu ya suluhisho la matatizo yaliyopo kwenye jamii kwasababu vijana wana nguvu,vipaji,uwezo wa ajabu,ubunifu .

Nguvu za vijana zikitumika vizuri zinaweza kufukuzisha umasikini,utegemezi na matatizo lukuki yanayoikumba jamii.

Vijana nao wasikae nyuma katika masuala ya kifamilia ,kijamii,wawajibike watumie nguvu walizonazo,ubunifu,uwezo,vipaji na talanta na elimu walizonazo katika kutatua changamoto za jamii badala ya kukaa kama watu wa pembezoni.

Ni vyema kuhamasisha ushiriki mpana wa vijana katika masuala ya kiuchumi,kijamii na kisiasa kwasababu vijana wakiachwa nyuma hali itazidi kuwa mbaya kwa vizazi vijavyo.

“Nusu ya maisha tunayoishi yanatokana na kizazi kilichopita na nusu nyingine inatokana na kizazi kilichopo” Anaeleza Mtunzi mmoja wa kitabu.

Ina maana kuwa vijana wanawajibika kuweka misingi bora ya kiuchumi,kimaadili  na kiuwajibika misingi ambayo itatumiwa na kizazi kijacho iwapo hawatafanya hivyo hali itazidi kuwa mbaya .

“Unapoacha kutimiza wajibu wako duniani,kutumia uwezo ulionao,vipaji  unapokufa unaacha nafasi wazi duniani ambayo ingepaswa uijaze kwa kuacha kitu duniani kizazi kijacho kikija kitakuta nafasi uliyoiacha hukufanya kitu” Anaeleza Mtunzi Mashuri wa vitabu Myles Munroe.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad