Waziri
wa Nishati na Madini, George Simbachawene (mbele ) akiongoza kikao
kilichokutanisha ujumbe kutoka Benki ya Dunia na watalaam wa Wizara ya
Nishati na Madini ili kujadili maendeleo ya miradi ya nishati nchini
inayofadhiliwa na Benki hiyo, changamoto zake na kupata mapendekezo
ya kuboresha miradi hiyo.
Mkurugenzi
wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi , Philippe
Dongier (kushoto) akimweleza Waziri wa Nishati na Madini, George
Simbachawene (kulia) mikakati ya Benki hiyo katika kuisaidia
Tanzania katika sekta ya nishati kwenye kikao hicho.
Msimamizi
wa Miradi ya Benki ya Dunia Jacques Douzier (kushoto) akisisitiza
jambo katika kikao hicho. Kulia ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa
nchi za Tanzania, Uganda na Burundi , Philippe Dongier.
Waziri
wa Nishati na Madini, George Simbachawene akielezea maendeleo ya
miradi ya nishati nchini na kuiomba Benki ya Dunia kulisaidia Shirika
la Umeme Nchini (Tanesco) ili liweze kutekeleza miradi ya umeme kwa
wakati.
Waziri
wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) akibadilishana
mawazo na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na
Burundi , Philippe Dongier (kushoto) mara baada ya kumalizika kwa
kikao hicho.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri
wa Nishati na Madini, George Simbachawene ameliomba Shirika la Fedha
Duniani (WB) kulisaidia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) ili liweze
kuimarisha miradi ya usambazaji wa umeme nchini hususan vijijini.
Simbachawene
aliyasema hayo wakati alipokutana na ujumbe kutoka Benki ya Dunia na
watalaam wa Wizara ya Nishati na Madini ili kujadili maendeleo ya
miradi ya nishati nchini inayofadhiliwa na Benki hiyo, changamoto zake
na kupata mapendekezo ya kuboresha miradi hiyo.
Alisema
kuwa Tanesco inakabiliwa na changamoto ya fedha katika utekelezaji wa
miradi ya umeme hususan usambazaji wa umeme vijijini na kupelekea
miradi mingi kutokamilika kwa wakati.
Akielezea
maendeleo ya shirika hilo la umeme, Simbachawene alisema kuwa shirika
hilo limeongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato kwa kubuni mikakati
mbalimbali ya ukusanyaji wa mapato hayo na kupunguza hasara zilizokuwa
zikijitokeza mara kwa mara.
Akielezea
kuhusu upunguzaji wa bei ya umeme nchini, Simbachawene alisema kuwa
Serikali imejenga bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara hadi jijini Dar
es Salaam jambo litakalochangia upatikanaji wa nishati ya umeme ya
uhakika na kwa gharama nafuu ambalo ni moja ya utekelezaji wa Mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa.
“ Ili
kuhakikisha wananchi wananufaika na sekta mpya ya gesi, serikali
ilibuni utaratibu wa kusomesha wataalam pamoja na wanafunzi waliofanya
vizuri katika masomo ya sayansi katika vyuo vikuu vinavyotoa fani za
mafuta na gesi ili kuwa na wataalamu watakaosimamia kwa ufanisi sekta
ya gesi na mafuta.,” alisema Simbachawene
Aliongeza
kuwa mara baada ya kuwa na wataalam waliobobea katika masuala ya gesi
na mafuta, serikali itaunda taasisi itakayokuwa na kazi ya kutoa
ushauri katika masuala ya gesi na mafuta hususan wakati wa uingiaji wa
mikataba
“ Kwa
mfano kuna uwekezaji mkubwa unaohitaji mamilioni ya Dola za Marekani,
kwa mfano Ujenzi wa Viwanda vya Gesi ya Kimiminika (LNG), uwekezaji huu
unahitaji timu ya wataalam watakaohakikisha kuwa maslahi ya nchi
yanazingatiwa,” alisisitiza Simbachawene.
Aliongeza
kuwa, mbali na kuzalisha wataalam, serikali kwa sasa inaandaa sheria
kwa ajili ya sekta za gesi na mafuta ambapo mpaka sasa maoni kutoka
kwa wadau mbalimbali yamekusanywa na kujumishwa.
Akielezea
kuhusu uwazi katika mikataba ya gesi na mafuta, Simbachawene alisema
kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kunakuwepo na uwazi katika
shughuli zake, moja ya mikakati hiyo ni pamoja na kujiunga na
Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na Uwazi na Uwajibikaji katika
Tasnia ya Uziduaji (EITI) ambapo taarifa mbalimbali za malipo na
makusanyo katika sekta za madini na gesi zimekuwa zikikusanywa na
kusambazwa kwa wananchi.
Aliendelea kusema kuwa, Serikali inafuata sheria zinazosimamia utoaji wa taarifa za mikataba.
Wakati
huo huo Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na
Burundi, Philippe Dongier alisema kuwa Benki ya Dunia ipo tayari
kushirikiana na Serikali kupitia Shirika la Tanesco ili kuhakikisha
kuwa wananchi wanapata umeme wa uhakika na nchi kutoka katika kundi la
nchi masikini dunaiani na kuwa katika kundi la nchi zenye kipato cha
kati.
Dongier
alisema awali Benki ya Dunia ilijitosa kuisaidia Tanesco ili iweze
kutoka kwenye utegemezi wa chanzo kimoja cha nishati ya umeme yaani
maji na kutumia vyanzo vingi ikiwa ni pamoja na kupelekea ujenzi wa
bomba la gesi kutoka Mtwara hadi jijini Dar es salaam ambalo mara
baada ya ukamilishwaji wake litapunguza gharama ya uzalishaji wa umeme
na wananchi wengi kunufaika na nishati hiyo.
Pia
Dongier alimpongeza Waziri Simbachawene kwa hatua ya serikali kujenga
bomba la gesi na kasi ya uandaaji wa sera kwa ajili ya usimamizi wa
sekta mpya za gesi na mafuta na kusisitiza kuwa Benki ya Dunia ipo
tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa malengo yake
yanatekelezwa.
No comments:
Post a Comment