Maisha na Dini : Rais Kikwete Asema " Waislamu Anzisheni Mahakama ya Kadhi, Serikali Imegoma na Haitawaingilia" - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


30 Mar 2015

Maisha na Dini : Rais Kikwete Asema " Waislamu Anzisheni Mahakama ya Kadhi, Serikali Imegoma na Haitawaingilia"


Rais Dkt.Jakaya mrisho Kikwete akifungua mkutano wa Viongozi wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere(JNICC) jijini Dar es Salaam leo. Baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali wakimsikiliza kwa makini Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akiwahutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Viongozi wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam leo.(picha na Freddy Maro).
<<<<<<<<<<<<<<<< >>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>
RAIS Jakaya Kikwete amefafanua msimamo wa Serikali katika mjadala unaoendelea wa Mahakama ya Kadhi, na kuweka wazi kuwa Serikali haina mpango wa kuianzisha, wala kuiendesha.


Mbali na hiyo, Rais Kikwete ambaye jana alizungumza na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Dar es Salaam, pia alielezea kusikitishwa kwake na tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania, lililowaelekeza waumini wao kupigia Katiba Inayopendekezwa kura ya Hapana.
Mahakama ya Kadhi
Akifafanua suala la Mahakama ya Kadhi, Rais Kikwete alisema Serikali ina msimamo wa mambo mawili katika mahakama hiyo.
Kwanza, alisema Serikali haina mpango wa kuianzisha na kuiweka katika Katiba na pili, haihusiki kuiendesha na badala yake, Waislamu wenyewe ndio watakaoiendesha.
Alisema kimsingi, mahakama hiyo ilikuwepo kabla ya Uhuru na kinachotakiwa kuzungumzwa ndani ya Bunge, ni Sheria ya Kutambua Uamuzi Unaofanywa na Kadhi.




Alifafanua zaidi kuwa Mahakama hiyo ya Kadhi, haihusiki na mambo ya jinai, isipokuwa mambo ya kijamii ikiwemo talaka, mirathi na mengine ya aina hiyo.
Alitoa mfano wa Sheria ya Kiislamu, iliyokuwepo tangu zamani, ambayo inatambua chombo hicho na kusisitiza kuwa kinazungumzwa, ni uamuzi unaofanywa na Kadhi utambulike tu.
Katika mfano huo, alisema Muislamu ukigombana na mke wake, kuna mabaraza ya usuluhishi ambayo huyo mwanamke atapaswa kwenda, ila wakishindwa na ataomba talaka ambayo inaidhinishwa na Kadhi, ambaye ndiye msajili wa vyeti vya ndoa kwa Waislmau.
Baada ya kutoa ufafanuzi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Shehe Alhad Musa, alimshukuru Rais Kikwete kwa ufafanuzi alioutoa na kusema Wakristo na Waislamu siku zote ni wamoja na wataendelea kuishi kwa amani, furaha na ushirikiano.
Katika hilo, Shehe Alhad alinukuu Biblia katika Kitabu cha Mathayo tano, mstari wa 25, ambao unasema; “Patana na mshitaki wako, mngali njiani, asije akakupeleka kwa Kadhi na Kadhi akakukabidhi kwa Polisi na Polisi akakutupa korokoroni.”
Katiba Pendekezwa
Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, ambayo inasubiri kupigiwa kura na wananchi, Rais Kikwete alisema Katiba hiyo imewakilisha vitu vingi kuliko Katiba iliyopo.
Alifafanua kwamba Katiba Inayopendekezwa, imeweka haki za makundi mbalimbali ya jamii, kuliko iliyopo na kuongeza kuwa yeye binafsi ameisoma na kurudia kuisoma, lakini hajaona mahali popote ambapo ina kasoro.
Alisema isingekuwa rahisi kuweka maoni ya kila mtu katika Katiba, na kufafanua kuwa yale ambayo hayajawekwa sasa hivi, utafika wakati wake na yatawekwa.
Alibainisha kuwa haikuwa rahisi kwa maoni ya kila mtu kuingia katika Katiba Inayopendekezwa, kwani hata CCM ilikuwa na mambo 60 waliyopendekeza, lakini kati ya hayo ni 12 tu yaliyoingia.
Rais Kikwete alisema Katiba sio Msahafu au Kurani, ambayo haiwezekani kubadilishwa hata nukta. Alitoa mfano wa Zanzibar, kwamba wakati kuunda Muungano, yapo mambo yalionekana ni muhimu kubakia katika Muungano, lakini kadri muda ulivyokwenda yameondoka.
Jukwaa la Wakristo
Akizungumzia tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania, Rais Kikwete alisema amehuzunishwa na kufadhaishwa na tamko hilo la viongozi wa dini la kutaka waumini wao wajiandikishe kwa wingi, lakini wapige kura ya Hapana kwa Katiba Inayopendekezwa.
Tamko hilo lilitolewa na jukwaa hilo linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT).
Rais Kikwete alisema, tamko hilo litakuwa pia limekwaza waumini, kwa kuwawekea mipaka ya kidemokrasia na kukwaza hata viongozi wenyewe.
Alitoa mfano kwamba kwa tamko hilo, muumini hataweza kusimama na kumwambia kiongozi wa dini asiwaingilie katika uamuzi, kwa kuwa kupiga kura ni haki ya kikatiba ya kila mtu, na ikitokea hivyo, hata kiongozi husika atakwazika.
Subira kwa NEC
Kuhusu uwezekano wa Kura ya Maoni kufanyika Aprili 30 kama ilivyotangazwa na Serikali, huku kazi ya kuandikisha wapigakura ikiendelea kusuasua, Rais Kikwete alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inayoratibu uandikishaji wa wapigakura, itazungumza kuhusu walipofikia wakati muafaka ukifika.
Amani
Kuhusu amani ya nchi, Rais Kikwete alisema viongozi wa dini pia wa jukumu kubwa la kuimarisha amani ya nchi.
Katika utekelezaji wa jukumu hilo, Rais Kikwete aliwataka viongozi hao wajaribu kuepuka kutumiwa na watu wenye nia mbaya, kwa sababu wanafahamu kuwa viongozi wa dini wana ushawishi katika jamii na wana watu wengi nyuma yao.
Alisema machafuko yatakayotokana na mvurugano wa kidini, hakuna mtu atakayeweza kuyazuia, hivyo ni vyema viongozi hao waendeleze mshikamano.
Alitoa mwito kwa mikoa mingine nchini, kuunda kamati za amani kama ilivyo Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad