Maendeleo :Tume ya Mipango Yatembelea Meli ya Kihistoria ya MV Liemba - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


13 Dec 2014

Maendeleo :Tume ya Mipango Yatembelea Meli ya Kihistoria ya MV Liemba

Wakaguzi wa Miradi ya Maendeleo toka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wamepata fursa adhimu ya kutembelea meli kongwe kupita zote nchini, MV Liemba iliyo kwenye Ziwa Tanganyika, mkoani Kigoma.
Wakizungumza mara walipofika katika meli hiyo baadhi ya wakaguzi hao hawakuficha bashasha waliyokuwa nayo mara baada ya kuingia ndani ya meli hiyo kongwe iliyo na umri zaidi ya miaka 100.
Mmoja wa wakaguzi hao Bibi Zena Hussein, alisema kuwa anajisikia furaha sana kuingia na kushuhudia mandhari ya meli hiyo ya kihistoria nchini Tanzania.
“Nimefurahi sana kufika leo hii kwenye meli hii yenye miaka zaidi ya 100, licha ya ukongwe wake bado inaonekana imara na yenye uwezo wa kufanya kazi miaka mingi zaidi,” alisema.
MV Liemba ni meli ya Kitanzania inayohudumia pwani za Ziwa Tanganyika. Ni chombo cha usafiri wa majini chenye umri mkubwa kuliko kingine chochote nchini na kipo tangu mwaka 1914. Meli hii kama zilivyo meli ningine inasukumwa na injini ya diseli na ina urefu wake ni mita 67, upana mita 10 na uzito wa tani 1500.
Kwa mujibu wa Nahodha wa meli hiyo, Kapteni Mathew Mwanjisi, meli hiyo ina uwezzo wa kubeba abiria 600 na tani za mizigo 200.
“Katika daraja la kwanza meli ina uwezo wa kubeba abiria 20, daraja la pili abiria 30 na daraja la tatu abiria 550,” alisema. 
Meli ya MV. Liemba inamilikiwa na Kampuni ya MSCL na kusajiliwa na Mamlaka ya Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kwa namba ya usajili KP/P001. Meli hiyo ilijengwa katika Bandari ya Kigoma mwaka 1913 na mjenzi kutoka Ujerumani kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo na abiria.
Mv. Liemba ilitengenezwa nchini Ujerumani mwaka 1913 ikiwa ikiitwa kwa Kijerumani "Graf von Goetzen" kwenye kiwanda cha meli cha Meyer huko Papenburg.
Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ikiwa ndani ya MV Liemba mara walipofika kujionea mandhari ya meli hiyo kongwe duniani.
Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kushoto) akisaini kitabu cha wageni ndani ya MV Liemba. Kulia ni Nahodha wa Meli hiyo, Kapteni Mathew Mwanjisi.
Nahodha wa MV Liemba, Kapteni Mathew Mwanjisi (Watatu kushoto) akitoa maelezo kwa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.
Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Wapili Kulia) akiiongoza Timu yake kusikiliza kwa umakini namna ya kusoma radar inayotumika ndani ya Meli ya MV Liemba. Anayewapa maelezo ni Nahodha wa Meli hiyo, Kapteni Mathew Mwanjisi.
Nahodha wa Meli ya MV Liemba, Kapteni Mathew Mwanjisi (Kulia) akitoa maelezo ya namna ya kutumia chombo cha kuokolea kwa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango. Wanaomsikiliza ni Kiongozi wa Timu hiyo, Bibi Florence Mwanri (Kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji (Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango), Bw. Omary Abdallah.
Mhandisi Mkuu wa Meli ya MV Liemba, Eng. Justine Joachim (Mwenye fulana nyeusi) akiwapa maelezo Wakaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango walipongia kujionea mitambo ya kuendeshea meli hiyo.
Kazi inaendelea! Watumishi wa Meli ya MV Liemba wakiendelea na kazi ya kushusha shehena ya mahindi kutoka kwenye meli hiyo. PICHA NA SAIDI MKABAKULI

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad