Nishati na Madini :TMAA Yapiga Mnada Madini Yaliyokamatwa Yakitoroshwa Nje ya Nchi, Jijini Arusha - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


21 Nov 2014

Nishati na Madini :TMAA Yapiga Mnada Madini Yaliyokamatwa Yakitoroshwa Nje ya Nchi, Jijini Arusha



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eng. Ngosi Mwihava akizungumza kabla ya kuanza kwa mnada wa kwanza wa madini yaliyokamatwa yakisafirishwa nje ya nchi kinyume cha sheria.Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Bruno Mteta (wa kwanza kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Madini Tanzania, Richard Kasesera (wa pili kulia), Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Uchumi na Biashara, Salim Salim (wa tatu kushoto), Meneja Usafirishaji Madini wa TMAA, George Kaseza (wa pili kushoto), na maafisa wengine kutoka TMAA, Eng. Charles Shamika (wa nne kushoto) na Flora Kisena (wa kwanza kushoto).
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Bruno Mteta (wa nne kulia), akisoma moja ya zabuni (bid) ya ununuzi wa madini yaliyokuwa yakipigwa mnada jijini Arusha. Wengine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eng. Ngosi Mwihava (wa tano kulia), Zabibu Napacho, Afisa Mfawidhi Ofisi ya TMAA-Arusha (wa kwanza kulia), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari TMAA, Eng.Yisambi Shiwa (wa pili kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Madini Tanzania, Richard Kasesera (wa tatu kulia), Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Uchumi na Biashara, Salim Salim (wa tatu kushoto), Meneja Usafirishaji Madini wa TMAA, George Kaseza (wa pili kushoto), na Eng. Charles Shamika (wa nne kushoto), Flora Kisena (wa kwanza kushoto) kutoka TMAA.
wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi waliohudhuria Maonesho ya Tatu ya Kimataifa ya Vito ya Arusha, wakishuhudia mnada wa kwanza wa madini yaliyokamatwa yakisafirishwa nje ya nchi bila kuwa na vibali husika.Aliyenyanyua karatasi ya maombi ya zabuni (bid) ya madini hayo ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala katika Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Bruno Mteta.
Meneja Usafirishaji Madini kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), George Kaseza (katikati),akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha, mara baada ya kumalizika kwa mnada wa kwanza wa madini yaliyokamatwa yakisafirishwa nje ya nchi kinyume cha sheria.

NaTeresia Mhagama

Madini yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 yaliyokamatwa wakati yakisafirishwa nje ya nchi bila kufuata taratibu za nchi za usafirishaji madini yamepigwa mnada na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA).

Madini hayo yamepigwa mnada jijini Arusha katika Maonesho ya Tatu ya Kimataifa ya Vito yaliyofanyika katika hoteli ya Mount Meru ambapo mnada   huo wa kwanza kufanyika nchini ulishuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eng.Ngosi Mwihava, Mwenyekii wa Bodi ya Ushauri wa Madini, Richard Kasesera, Makamishna Wasaidizi wa Madini nchini na wananchi waliohudhuria maonesho hayo.

Meneja Usafirishaji Madini wa TMAA, George Kaseza amesema kukamatwa kwa madini husika ni matokeo ya juhudi za Serikali za kufanya kaguzi katika viwanja vikubwa vya ndege vya Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro na kueleza kuwa huo ni utekelezaji wa sheria ya madini ya mwaka 2010 inayoeleza kuwa usafirishaji madini kinyume na taratibu na kanuni zilizowekwa ni kosa la jinai hivyo watoroshaji wa madini hayo walikamatwa na kufikishwa katika Jeshi la Polisi.

"Udhibiti hufanyika ili kuhakikisha kwamba madini yote yanasafirishwa kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni zinazosimamia biashara na uchimbaji unaofanyika kwenye Sekta ya Madini.Moja ya taratibu hizo ni ulipaji wa mrabaha kabla ya kusafirishwa nje ya nchi na kuwa na vibali maalum ambavyo madini husika yanatakiwa kuambatana navyo kabla ya kusafirishwa nje nchi", alisema Kaseza.

Alieleza kuwa madini hayo yaliyopigwa mnada jijini Arusha yalikamatwa yakiwa yanasafirishwa kinyume na taratibu ikiwemo kutokuwa na vibali vya usafirishaji ama kutokuwa na vithibitisho vya ulipaji wa malipo ya mrabaha.

"Adhabu za waliokamatwa na madini haya zilishatolewa na Mahakama ambapo wengi walishatumikia adhabu zao ikiwamo kifungo ama kulipa faini   na madini yao kutaifishwa na kuwa mali ya serikali, hivyo serikali imeamua kufanya mnada wa kwanza kupitia maonesho haya ili kuhakikisha kwamba fedha zinazopatikana katika mnada huo zinaingia katika mfuko wa Serikali na kulinufaisha Taifa", alisema Kaseza.

Alieleza kuwa upigaji mnada wa madini husika pia utapelekea watu kufuata sheria zinazosimamia Sekta ya Madini na kusisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watoroshaji, wanaofanya biashara haramu ya madini na kumiliki madini kinyume cha sheria.

Akifungua mnada huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eng. Ngosi Mwihava alieleza kuwa serikali inaendelea kuisimamia Sekta ya Madini ipasavyo ili kuhakikisha kwamba madini yaliyopo Tanzania yanawanufaisha watanzania na kusisitiza kuwa kupitia utaifishaji madini yanayotoroshwa, serikali itakuwa ikipata fedha zitakazosaidia katika shughuli za maendeleo.

Alieleza kuwa minada husika itakuwa ikifanyika kwa uwazi na haki na kwamba mshindi wa zabuni husika atakuwa ni yule aliyetimiza vigezo vilivyowekwa ikiwemo kutokuwa chini ya bei iliyowekwa na serikali ambayo   imezingatia thamani ya madini husika.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Madini nchini, Richard Kasesera alisema kuwa kufanyika kwa mnada huo kunaonesha jinsi serikali inavyotekeleza kwa vitendo mpango wake wa kuwakamata wale wote wanaotaka kuvusha madini nje ya nchi bila kufuata taratibu, kukwepa ushuru na kufanya biashara ya madini bila vibali.

Alitoa onyo kuwa hakutakuwa na msamaha kwa wale wote wanaokamatwa wakisafirisha madini kinyume na taratibu na kwamba Serikali itaendelea kukamata, kutaifisha na kupiga mnada madini hayo hivyo aliwataka wadau wote katika Sekta ya Madini ndani na nje ya nchi kuhakikisha wanafuata taratibu na sheria zinazosimamia sekta husika ili kujiepusha na kadhia hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad