HAPPY BIRTHDAY TO YOU: MCHEKESHAJI NA MSHEREHESHAJI ,EMMANUEL MATHIAS a.k.a MC PILI PILI - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


1 Oct 2014

HAPPY BIRTHDAY TO YOU: MCHEKESHAJI NA MSHEREHESHAJI ,EMMANUEL MATHIAS a.k.a MC PILI PILI

 
 Wazalendo 25 Blog inakutakia Maisha marefu na Mungu akuzidishie Nguvu, Juhudi na Ubunifu katika maisha yako.
 
 
 
 


 

Emmanuel Mathias almaarufu kama Mc Pilipili mwenye uso wa uchekeshaji kama kazi yake ilivyo, alizaliwa mtaa wa Airport Dodoma mjini mnamo tarehe 1 mwezi wa 10 mwaka 1985 akiwa ni mtoto wa pili wa Bwana Mathias Matebe na Bi Mariam Matebe.
 Emmanuel alianza elimu yake ya shule ya msingi katika shule ya msingi Kiwanja cha Ndege ambapo alisoma mpaka darasa la nne na kuhamia shule ya msingi Ipagala ambako alimalizia elimu yake ya msingi hapo mnamo mwaka 2000.
Akiwa shule ya msingi Emmanuel kijana mdogo na mcheshi alijihusisha na masuala ya uchoraji, uimbaji na hata kucheza muziki ingawa alikua na ndoto za kuwa Muandishi wa habari.
“mimi nilivutiwa saana na kazi za waaandishi wa habari na nikatamani sana siku moja niwe muandishi wa habari kama wao, japo nilikuwa pia natamani kuwa Mchungaji”. Alielezea kwa Emmanuel kwa kukumbuka.
“Nkumbuka nikiwa na umri wa miaka nane, ilikuja bendi ya Afriso iliyokuwa chini ya Super Lovii Longomba, kaka wa Awilo Longomba, daah! Nilitunzwa hela nyingii na ndio ilikuwa hela yangu ya kwanza ambayo pia niliitumia kulipa kodi ya nyumba tuliokuwa tunadaiwa na pia kununulia debe la unga kwani kwa kipindi hicho baba yangu alikuwa muuza mishkaki na mama alikuwa anauza ndizi hospitali hivyo hawakuweza kwa kipindi hicho kulipa kodi hali iliyopelekea kutaka kufukuzwa tulipokuwa tunaishi, ilitusaidia sana”.
Akiwa bado na umri mdogo, aliweza pia kuigiza sauti mbalimbali kama ya mwalimu Nyerere, Mwakasege, Mr. Bean na pia kubadili nyimbo za wasanii mbalimbali wa kizazi  kipya na kuziimba kwa Kigogo. Nyimbo
hizo ni kama Zeze, Mapozi, Seya na hata Zuwena.
Emmanuel aliweza kutunukiwa cheti cha ‘MTOTO WA NURU’ kama mtoto wa mfano na wa kuigwa katika kanisa la Baptist Bible Church ambapo alikuwa akisali na familia yake.  
Baaada ya kumaliza darasa la saba Emmanuel alijiunga na Shule ya sekondari Dodoma (Dodoma sekondari) mwaka 2001 ambapo ndoto zake za kuwa muandishi wa habari zilipoanza kufunikwa taratibu.
Akiwa sekondari kama ilivyo kawaida  huwa kuna masomo ya kuchagua, kutokana na tabia yake, mwalimu Kilela ambaye sasa ni marehemu alinishauri nichukue somo la ‘Theatre arts’ ambalo ni la Sanaa ya jukwaani somo ambalo alilipenda na kufaulu kuliko masomo mengine.
“Ilifikia hatua kila ninachoongea au watu wakiniangalia tu wanacheka, mpaka darasani ilifika hatua nikinyoosha mkono kujibu swali mwalimu hanichagui anajua ntachekesha tu”.
Emmanuel alipendelea masuala ya sanaa hali iliyopelekea kipaji chake cha uchekeshaji kukua na hata kuanza kuwa mshereheshaji (MC) katika matukio mbalimbali kama Birthday, Sendoff, Harusi na hata Vipaimara na baadaye kutunukiwa cheti cha ‘SPECIAL TALENT’ ama kipaji maalum  alipohitimu kidato cha nne.
Aliendelea na kazi ya Ushereheshaji hata alipofika kuanza masomo ya kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari Jubilee mkoani Dodoma.
Baada ya kuhitimu kidato cha Sita, Emmanuel alipata ufadhili kutoka kwa wahisani ambapo alipaswa kwenda kusomea Ualimu.
“nilipata wakati mgumu sana kufanya uamuzi kwani nilipenda kuwa Mwandishi wa habari na wakati huo huo mama yangu alisisitiza niende ualimu kwani hata katika Familia yetu tu hakuna hata mmoja aliyewahi kuwa mwandishi wa habari”.
Emmanuel alikubali kwenda katika Chuo cha Ualimu Eckenforde kilichoko mkoani Tanga.
Alipofika chuoni hapo alipata changamoto ya kusitisha tabia yake ya Uchekeshaji kwani alionywa na familia yake kuwa makini kwani amefadhiliwa hivyo akazane na kitu alichofuata chuoni.
“Kwakweli nilipata shida sana kwani hata nikisimama kimya mbele za watu walikua wanaangua vicheko wengine mpaka wanatoka machozi”. Alihadithia Emmanuel.
Waswahili husema, Maji ukiyavulia nguo sharti Uyaoge. Emmanueli au MC Pilipili alijikuta akiyaoga maji ya Uchekeshaji kwani alijikuta akianza kusherehesha katika Matamasha mbalimbali ya kidini ndani na nje ya Chuo.
“Kila palipotokea matamasha ya kidini kama Joint mass au Graduation walinichagua kuwa MC na watu walikuwa wakisikia ni mimi ntaogoza walifurahi na kujaa kwa wingi. Nilipata fursa ya kutembelea mikoa mbalimbali kwa kazi hii kama Dar es salaam na Morogoro”.
Mnamo mwaka 2009 Emmanuel alihitimu mafunzo yake ya Ualimu chuoni hapo na kupangiwa kufanya kazi Mkoani Manyara.
“Lakini sikupenda mkoa ule kwa sababu hauna sherehe nyingi kwahiyo nikaona kazi yangu ya uchekeshaji na uMC itakuwa ngumu kuifanya, ikabidi niombe kufundisha katika shule niliyosoma kidato cha tano na sita na walinipokea tayari kwa kazi ya ualimu hapo”.
.
Mwaka huo wa 2009 Emmanuel alijikuta ana majukumu makubwa  ya kuhudumia familia kwani kwa kipindi hicho baba yake mzazi alikuwa mgonjwa hivyo mama ambaye kwa wakati huo alikuwa ni mwalimu katika shule moja ya chekechea mjini hapo alikuwa anamuuguza baba nyumbani.
“Kwa bahati mbaya tarehe 30/5/2009 nilimpoteza baba yangu mzee Mathias Mtebe, niliumia sana kwani tulibaki sisi na mama peke yetu. Niliendelea  kutafuta hela nyingi zaidi kwani kwa kipindi hicho familia yangu ilikuwa inanitegemea kwa kila kitu kama baba”.
Aliajiriwa rasmi shuleni Jubilee sekondari mwezi wa 7 mwaka huo huo na kendelea na kazi ya ualimu kama mwalimu wa msomo ya Kiswahili, Historia, Bible knowledge pamoja na Civics.
Emmanuel ambaye kwa kipindi hicho jina la MC Pilipili lilikuwa tayari limeshajulikana zaidi kwa watu, aliendelea na kazi yake ya Uchekeshaji na Ushereheshaji kwa mapana zaidi kwani alikuwa na uwezo wa kusafiri kwenda mikoani.
Mwaka 2013 tarehe 30 mwezi wa 1, Pilipili aliacha rasmi kazi ya ualimu na kujishughulisha moja kwa moja na kazi ya Uchekeshaji na Ushereheshaji kazi ambayo ilimuingizia kipato zaidi akiilinganisha na ualimu.
“Baada ya kuwa nasafiri sana kuja Dar na kurudi Dodoma nilijikuta kwakweli nakuja zaidi ya mara moja kwa wiki na kwa bahati nzuri kipato cha Ushereheshaji kilikuwa kinazidi kabisa kile cha ualimu”. Anaendelea kusema kwamba hakuwa na jinsi zaidi ya kusitisha ualimu.
Mgaagaa na Upwa hali wali mkavu. Pilipili aihamia Dar es salaam  ambapo ssa alifanya kazi hiyo rasmi na kwa ufanisi mzuri.
“Yaani naweza nikapata ‘deal’ nyingi kwa wiki nzima mfululizo ila sio chini ya mara mbili kwa wiki na kila kazi huwa natoza si chini ya Shilingi miliomi mija na laki nne kama mtu atanihitaji kama MC na Mchekeshaji. Ukiniita kama mchekeshaji peke yake una MC wako huwa inakuwa kama Shilingi laki nane hivi ambapo kwa Ushereheshaji peke yake ni kama million moja na laki mbili hivi.
MC Pilipili anaelezea kuwa mafanikio aliyoyapata kutokana na kazi hii ni makubwa sana kwani ameweza kujenga nyumba kubwa mbili nyumbani kwao, anamiliki viwanja vitano pamoja na akiba ya kutosha kwa matumizi yake ambayo iko Benki.
Kwa upande wa changamoto Pilipili anasema “Kwakweli kazi hii ni ya imani, unaweza ukaamka hujui hata utafanya nini wiki nzima lakini zikafululizana simu unapigiwa kuwa unahitajika, unabaki kupanga wewe sasa uende wapi’. Pia anaendelea kusema kuwa sanaa ya uchekeshaji kwa Tanzania bado haijakubalika sana haswa uchekeshaji wima (Stand up Comedy)
Pilipili ameweza kufanya kazi ya Uchekeshaji na Ushereheshaji katika nchi mbalimbali kama Kenya, Rwanda, Uganda pamoja na Afrka ya kusini hali iliyomsaidia kujitangaza ndani nan je ya nchi kwani mashirika na kampuni mbalimbali humwita sana kuongoza sherehe na matukio mbalimbali.
“Matarajio yangu ni kutangaza Stand up comedy Tanzania pamoja na sanaa ya uchekeshaji na pia kuitangaza Tanzania kupitia Stand up comedy”.
Pilipili ambaye bado ni kijana anawasihi vijana wenzake kutumia vipaji vyao na sio kulazimisha usomi. Anasema, “Kipaji kinaweza kukupeleka mbele ya wakuu” akitolea mfano wa watu wa kwenye Biblia kama Mfalme Daudi na Yusuph ambao walitumia vipaji vyao na wakainuliwa na Mungu.
 Pilipili ameweza kualikwa Bungeni ambapo alitambulishwa kama mchekeshaji wa Tanzania, Kualikwa Makanisa mbalimbali kutoa mafunzo na mahubiri na pia alifanya kazi jukwaa moja na Eric Omondi kutoka Kenya mwezi wa 12 mwaka 2013 katika hoteli Golden Tulip kama wachekeshaji.
“Npenda kutumia usemi unaosema ‘Sherehe ni Mc”. Aliyasema hayo akiwasahauri washereheshaji wenzake kufanya kazi hiyo kwa kuhakikisha wanasoma vitabu, kuangalia internet kuona nini wanatakiwa kufanya pamoja na kuwa na Usasa ili wafanye  kazi hiyo katika kiwango kizuri. 
 
USHAURI WA Mc PiliPili kwa Serikali
Pia anaishauri serikali kurudisha masomo ya sanaa na kuweka walimu maalum wanaojua sanaa kufundisha masomo hayo na kuwawekea watoto msingi mzuri wa kitu wanachokipenda kufanya tangu wakiwa wadogo kwani kila mtu ana kipaji chake na anasisitiza kuwa kazi ambayo mtu ataifanya vizuri na kwa ufanisi ni kazi ambayo anaioenda na ataifanya kutoka moyoni.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad