MCHAKATO WA URAIS 2015 :MBUNGE WA JIMBO LA NZEGA DR.KHAMIS KINGWANGALLAH ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA URAIS 2015 - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


8 Sept 2014

MCHAKATO WA URAIS 2015 :MBUNGE WA JIMBO LA NZEGA DR.KHAMIS KINGWANGALLAH ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA URAIS 2015



1Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya serikali za Mitaa na Mbunge wa jimbo la Nzega Dr. Khamis Kigwangallah akitangaza nia yake ya kugombea urais waJamhuri ya Muungano ya Tanzania wakati alipokutana na waandishi wa habari kwenye ambapo amesema hajasukumwa na mtu yeyote ila ni yeye mwenyewe ameamua kwa moyo wake. 02Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya serikali za Mitaa na Mbunge wa jimbo la Nzega Dr. Khamis Kigwangallah akimtambulisha mke wake Dr Bayoum Awadh wakati wa mkutano huo. 4Mzee Nasser SAid Mussa baba mzazi wa Dr. Khamis Kigwangallah na mama yake mzazi Mama Bagaile Lumola. na watoto wake Sheila kulia ni Hawa. 8Mchungaji Patrick Saso akifanya maombi kabla ya kuanza kwa mkutano huo. 9Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo. 10Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.DSC_0103Sheikh Abubakary Mwita akiomba dua kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
..............................................................................
Ndugu viongozi mlioko hapa, wageni waalikwa, wanahabari na watanzania wenzangu mnaonisikiliza;
Ni heshima kubwa sana kwangu kupata fursa hii. Ni katika nchi chache sana duniani, mtoto wa maskini kama mimi, aliyewahi kutembea mitaani akiuza karanga, Big G, maandazi, jerebi na samaki ili kusaidia wazazi kupata chochote kwa ajili ya kulisha familia anaweza kuota kuwa Rais wa nchi yake. Kwamba, mtoto aliyeenda shule bila viatu anaweza kuwa Daktari. Hii inamaanisha misingi ya haki na usawa kwa wote iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili haikuwa ndoto za alinacha, bali ukweli na uhalisia, na inafanya kazi. Kwamba, siyo lazima uwe mtoto wa tajiri ndiyo uoneshe kipaji chako.
Hili peke yake linanipa sababu ya ziada ya kwa nini nitamani kuota kuwa Rais – nataka niwe mfano hai wa mafanikio ya Ndoto ya waasisi wa Taifa letu, kuwa sote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuna haki na fursa sawa bila kujali nani anatokea familia ipi. Hii ni Tanzania ya ndoto za waliotutangulia. Ni lazima atokee kiongozi wa kizazi hiki anayetamani kuiongoza Tanzania itakayodumu kwenye misingi hii: kwamba sisi sote ni ndugu, na tuna fursa sawa. Kwamba, kuendelea kimaisha na kibinafsi ni haki ya binadamu na si hisani. Kwamba, mtoto wa mama ntilie kama nilivyokuwa mimi hapa, ana haki na fursa ya kuwa mbunge ama Rais wa nchi, sawa kabisa na mtoto wa Mbunge.
Kwa namna ya kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza waasisi wa Taifa letu kwa kusimamia tunu hizi. Niwashukuru pia viongozi wote walionitangulia kwa kuzilinda, na niahidi nitakuwa wa mwisho kuisaliti nchi yangu kwenye mambo haya.
Leo nimefika hapa kwa sababu chama change kina mfumo mzuri ulioasisiwa na Mwl. Nyerere na umelindwa na Wenyeviti waliomfuatia mpaka na sisi tumeukuta. Leo nimefika hapa kwa sababu Rais Jakaya Kikwete na wajumbe wenzake wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu walitumia misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Chama changu kuamua kuwa nami nina haki ya kuwa Mbunge. Leo nazungumza hapa nikiamini kuwa ni misingi hiyo hiyo itatoa uongozi wa Taifa letu katika awamu ijayo.
Babu yangu Kizaa Baba aliishi Kijijini Goweko, Mlimani, na alikuwa mfugaji mkubwa wa ng’ombe na mrina asali mashuhuri. Yeye na mkewe waliishi maisha ya heshima sana pale kijijini. Hawakuwahi kusoma wala kuajiriwa japokuwa Babu yangu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama Cha TANU na baadaye CCM katika ngazi ya Kata.
Babu yangu na Bibi yangu kizaa mama waliishi Nzega, na ndiyo walionilea baada ya ndoa ya mama yangu na baba yangu kuvunjika. Walinifundisha mambo mengi, kubwa likiwa ni kujiamini, pia kufanya mambo yangu kwa bidii, uadilifu, umakini na kwa nidhamu ya hali ya juu. Bibi yangu huyu hakusoma shule ya kizungu japokuwa alijifunza kusoma na kuandika. Babu yangu alikuwa mjukuu wa Chifu na hivyo alipata fursa ya kusoma Tabora School miaka miwili mbele ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Alifanya kazi mbalimbali chini ya serikali ya wakoloni, na alishiriki harakati za kuanzishwa na kusambaa kwa chama cha TAA na baadaye TANU. Babu yangu aliamini kuwa “binadamu wote ni sawa na kwamba kila mtu anastahili kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”, na kwamba ukoloni haukuwa kitu cha sawa, na hivyo kujitawala wenyewe dhidi ya wazungu ilikuwa ni haki yetu; pia aliamini katika elimu, na hivyo alifanya juhudi kusomesha mabinti zake watatu, mama yangu aliishia kwenye ualimu kabla ya kuingia kwenye ndoa. Babu aliamini kuwa Tanzania ya mabinti zake itahitaji wasomi, ndoto ambayo ninaishi kuitekeleza kwa ajili ya mabinti zangu wawili na Kaka yao, HK Jr.
Japokuwa bibi na babu yangu wameishatangulia mbele ya haki, naamini wananitazama na kutabasamu huko waliko.
Ninaishi nikiamini kuwa hadithi ya maisha yangu ni mfano hai kwa maisha ya watanzania wengi. Na kwamba, nina deni la kulipa kwa vizazi vijavyo kwa kuwa mimi ninafaidi matunda ya mti uliopandwa na vizazi vilivyonitangulia. Naliona jukumu la kuhakikisha vizazi vijavyo vinafaidi urithi wa Tanzania kuwa ni la kwangu na wenzangu wa kizazi hiki.
Kazi yangu imenifikisha sehemu nyingi sana za nchi yetu – vijijini na kwenye majiji, imenikutanisha na watu wa kila aina – matajiri kwa maskini, wazee kwa vijana – hakuna hata mmoja kati ya watu hawa anayetegemea Serikali itamtatulia kero zake zote. Wanajua wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili wasonge mbele – na wana nia ya kufanya hivyo.
Nenda kwa wafanyabiashara wakubwa kule Pugu Road viwandani, kwa watumishi pale hospitali ya Taifa Muhimbili, ama pale sokoni Kariakoo kwa wafanyabiashara, wote watakuambia hawapendi kuona kodi zao zikitafunwa na wachache pale TRA, ama kulipa posho za bure kwa wabunge na mawaziri kule Bungeni, kulipia mashangingi ya viongozi na watendaji, kulipia tiketi za ndege daraja la kwanza kwa ajili ya safari za viongozi na wataalamu wetu kwenda kujifunza kupambana na umaskini wakati wakirudi wanauacha uzoefu uwanja wa ndege, ama kulipia semina, warsha na makongamano ya wataalamu ya kuandika sera za MKUKUTA, MKURABITA na kuandaa bajeti zisizotekelezwa kila mwaka.
Watanzania wanataka kupata huduma bora za afya, elimu, maji, miundombinu.
Nenda kule kwa watani zangu, Nanyumbu, ama Tandahimba, ama kwa ndugu zangu kule Nduli, Kyela, wazee kule watakuambia hawategemei Serikali itawaletea ubwabwa kwenye sahani za fedha, wanajua Serikali haitowafanyia kila kitu, lakini wanajua kabisa kuwa wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na wamekuwa wakifanya hivyo siku zote. Wanachohitaji wao ni kujengewa mazingira wezeshi kushiriki shughuli zao za kilimo ama biashara, waelekezwe namna ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia njia za kisasa za kilimo chenye tija na ufanisi, waelekezwe wanapataje pembejeo, wanapataje mikopo yenye riba nafuu, wanahitaji, mwisho wa siku, wajue wapi watauza mazao yao kwa uhakika na bila kudhulumiwa wala kucheleweshewa malipo.
Watu hawatarajii serikali itabeba mizigo yao yote. Lakini wanaamini kabisa, kwamba tukibadili kidogo tu vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha serikali, tukibadili kidogo namna tunavyoendesha uchumi wetu, tutaweza, kwa kiasi kikubwa, kubadili muelekeo mzima wa maisha ya baadaye ya watoto na wajukuu zetu. Tutatoa uhakika wa kuiondoa nchi yetu kutoka miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani.
Na mimi, kama watanzania wenzangu wengi, nina imani kubwa kabisa, kwamba tunaweza kubadili mustakabali wa Taifa letu. Tunaweza kufungua milango ya maisha bora zaidi kwa watanzania. Tutatoa fursa sawa kwa kila mtanzania kuishi kwa matumaini, kwamba atabadili maisha yake wakati wowote ule kuanzia leo. Tutaweza kuamsha ari ya kila mtanzania kuongeza bidii kwenye kazi akitumaini na kuamini kuwa kesho yake itakuwa bora kuliko jana yake, kuwa naye ataishi kwa heshima, raha na starehe ndani ya nyumba yake.
Ninaamini, kutokea ndani kabisa ya mifupa yangu, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha serikali yetu, haya ninayoyasema si ndoto za mchana. Ni mambo yanayowezekana.
Watanzania wengi wanaamini, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu, mabadiliko makubwa, na ya haraka yatatokea kwenye uchumi wetu. Wanaamini tukichagua kiongozi sahihi mwakani, anayejua mahitaji ya nchi yetu kwa sasa na baadaye, tutafanikiwa.
Nyote mliopo hapa na wanaotusikiliza kutokea nje ya hapa mna jukumu la kututazama kwa ukaribu sana, kututathmini na kutupima sote; tuliojitokeza hadharani, walioanza safari za matumaini, wanaotajwa tajwa, na wale wanaosubiri kuoteshwa ili wakati muafaka ukifika muwape taarifa sahihi watanzania, kuwa kati yetu sote, ni nani anafaa kutuongoza kuelekea Tanzania ya ndoto zetu!
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuwa Amiri-jeshi-mkuu, siyo kwa uanajeshi wake bali kwa uwezo na utayari wake wa kuwashirikisha wataalamu wa majeshi na kuamua kwa busara kutumia nguvu za kijeshi pale inapolazimika baada ya kupima na kuchambua aina nyingine zote za kutafuta suluhu za migogoro kabla ya kuamua vita.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika uhuru, haki na usawa na wajibu wa watu wote, kama unavyolindwa na Katiba, anayeamini katika haki ya kuabudu lakini asiyekuwa tayari kuitumia haki hiyo kuwagawa watanzania kutokana na dini zao.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika Haki ya kupata huduma bora za afya, elimu, maji, kama wanavyopata wabunge na mawaziri wetu, kama wanavyopata mahakimu na majaji wetu, kama wanavyopata wafanyabiashara na wakurugenzi wetu.
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuhakikisha kuwa watanzania wote wanapata haki hizi bila kutazama hali zao kiuchumi ama daraja zao kijamii.
Kuwa, ni nani kati yetu anaamini zaidi katika uhuru na kujitegemea kwenye masoko na malighafi ili kudhibiti uchumi wetu mpana wa ndani, kujitegemea kwenye masoko ya pamba na nguo, kwenye mafuta ya kula, kwenye chakula cha uhakika kwa ajili ya watu wetu, kwenye mafuta na gesi ili tukwepe mtego wa kuwa sehemu ya uchumi, masoko na biashara za hasara na faida za makampuni makubwa ya kimataifa nje ya mipaka yetu. Ili tulinde thamani ya fedha yetu, ili tuwe na uhakika wa ustawi wa maisha ya watu wetu ndani ya nchi bila athari kubwa kutoka nje ya nchi yetu.
Kuwa, ni nani miongoni mwetu anaakisi taswira sahihi zaidi ya watanzania walio wengi, historia yake, rekodi yake, wajihi wake, mtazamo wake, ndoto zake, zinaakisi ‘utanzania’ halisi. Kuwa, yeye ni hitaji sahihi la watanzania.
Wakati ukifika, muwaeleze watanzania ukweli, wafanye uamuzi unaotokana na taarifa sahihi, wachague mtu sahihi.
Mimi, Ndugu zangu, natangaza rasmi sasa, kuwa ninatia nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Na nimefikia uamuzi huu bila kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa, kupangiwa ama kupanga na mtu ama na kikundi cha watu, bali kwa utashi na utayari wangu. Na ninayasema haya, haswa baada ya kutafakari mambo mengi kwa kina: mahitaji ya sasa na baadaye ya Tanzania ya ndoto zangu, uwepo wa fursa ya kugombea na kushinda uchaguzi ujao, uwezo wangu wa kuchambua mambo, kutafakari, kufanya maamuzi sahihi, kuchukua hatua za utekelezaji na kusimamia utekelezaji, uadilifu na uzalendo wangu, na zaidi nia yangu ya kuwa sehemu ya watanzania wengi tunaotaka kuona mapinduzi ya kifikra katika nchi yetu – mapinduzi ambayo yatatia chachu ya mabadiliko ya namna tunavyochagua vipaumbele vyetu kama Taifa na namna tunavyosimamia utekelezaji wa mambo mazuri tunayojipangia kama Taifa.
Ninatangaza nia ya kugombea Urais nikiwapa fursa watanzania wanipime na kunitazama mwenendo na uwezo wangu, nikiamini kabisa nitapimwa na kuungwa mkono ama kutoungwa mkono si kwa rangi ya ngozi yangu, si kwa jinsi yangu, si kwa umri wangu, na wala si kwa daraja langu kwenye jamii, dini yangu, ama kabila langu. Ninaamini nitapimwa kwa sifa na uwezo wangu, kama mtanzania.
Watanzania tuna sifa moja kubwa; kwenye mambo ya msingi ya kitaifa, tunakubaliana kuwa maslahi ya Tanzania hupanda juu ya maslahi yetu binafsi. Tudumishe utanzania wetu.
Ninaamini katika Ndoto ya Tanzania. Kuwa leo miaka 50 ya kuwa Jamhuri ya Tanzania tuna kila sababu ya kuwa Taifa la dunia ya kwanza, viongozi waliotutangulia wameandaa misingi ya kuifikisha Tanzania kwenye matamanio yetu. Kizazi chetu cha kina jukumu na wajibu wa kuikimbiza Tanzania kufikia kwenye ahadi inayotokana na ndoto za wazee na waasisi wa Taifa letu. Binafsi, niko tayari kulibeba jukumu hilo bila woga wala wasiwasi, maana naamini tusipojitokeza watu kama mimi, tutajikuta tunaongozwa na watu wasiostahili. Nina suluhu ya changamoto kubwa za leo na kesho: kupigana na njaa na kuhakikisha usalama wa chakula kwa watu wetu, tatizo la ajira kwa vijana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa mambo ambayo kizazi chetu kitapaswa kuyafanyia kazi kwa haraka na umakini wa hali ya juu.
Mimi ninaamini kwamba, kama hata mimi nimefika hapa, basi kila mtanzania anaweza, na ana haki ya kufika hapa na kwenda mbele zaidi yangu. Mafanikio siyo haki ya wachache, ni tunu ya Mwenyezimungu kwa kila mtu. Ninaamini ni haki ya kila mtanzania kuota ndoto yake, kuifanyia kazi na kuifikia. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina wajibu wa kutoa fursa kwa watu wake kuota ndoto zao na kufikia mafanikio bila kukwama.
Na ndugu watanzania wenzangu, amini nawaambia, kuwa, mbele yetu tuna kazi ya ziada ya kufanya. Kazi ambayo ninaamini tunaiweza tukiamua; uwezo tunao, sababu tunazo na nia tunayo – sema tuna mapungufu makubwa kwenye kuchukua hatua za kutenda.
Mimi naamini kwamba; E Pluribus unum. Baina ya wengi, mmoja!
Kwamba; Mimi ni mmoja kati ya uwingi wetu. Siwezi kuwa salama kama wengine hawako salama, siwezi kuwa na raha kama wengine wanateseka. Ninaongozwa na ile dhana kwamba, matatizo ya mwenzangu, ni ya kwangu, na si yangu peke yangu, ni yetu sote kama jamii moja.
Hivyo:
- kitisho cha njaa ya familia fulani maskini kule Sakasaka, wilayani Meatu, ni kitisho changu na familia yangu, hata kama siyo familia yangu.
- Kucheleweshewa haki ya kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kule Sombetini, ni kitisho kwangu pia, hata kama kesi siyo yangu.
- Mzee Makame wa kule Wete, Pemba, aliyefiwa na watoto wake akakosa msaada na yeye hana nguvu za kuzalisha tena, anavyokula mlo mmoja kwa siku ili asukume siku, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye siyo babu yangu.
- Mama John ni mpishi mzuri wa wali nazi kwa maharage, na ana wateja wengi mtaani kwake maeneo ya Mtaa wa Sikukuu, Sokoni Kariakoo; akifukuzwa, akapigwa virungu, akanyang’anywa pesa zake, akadhalilishwa na kumwagiwa chakula chake na mgambo wa jiji la Dar es salaam kwa kuwa anafanya biashara mahala pasiporuhusiwa, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye si mama yangu.
- Kama kuna mtoto asiyejua kusoma na kuandika kule Mrijo Chini kwa watani zangu warangi, hiyo inaniuma na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mwanangu.
- Bwana Kalumanzila ni mmachinga nguo za mitumba mitaani. Yeye huchukua nguo zake kumi kwa kuaminiwa na mwenye belo kutokea soko la Karume, akiuza anachukua kifaida kidogo cha juu kinachozidi hapo juu na kurudisha pesa ya mwenye mali Karume jioni ya siku hiyo. Elfu mbili ama tatu anayopata inamfanya aishi yeye na mkewe na watoto wake. Akifukuzwa barabarani na akanyang’anywa mali, anakosa kazi ya kufanya na analazimika kumtumikia bosi mwenye mali mpaka atakapofidia mali iliyopotea bila kupata cha juu. Shida na madhila anayoyapata bwana Kalumanzila zinaniumiza na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mjomba wangu.
Tarehe 4, Agosti 2014, Rais Kikwete akihutubia kwenye Kituo cha kimataifa cha maendeleo (Center for Global Development) alisema: “…Nataka na natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi masikini. Raslimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri…” Mimi nasema hivi: nataka na natamani kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kuongoza nchi Tajiri. Kama nitafanikiwa kuwa Rais, nitatumia miaka ya awali ya uongozi wangu kuikimbiza Tanzania kuelekea kwenye ndoto hii.
Mungu awabariki. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad