ELIMU YETU :VIJANA WEKENI MSISITIZO MASOMO YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA ILI MUWE WAJUZI NA KULETA MAENDELEO NCHINI - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


9 Sept 2014

ELIMU YETU :VIJANA WEKENI MSISITIZO MASOMO YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA ILI MUWE WAJUZI NA KULETA MAENDELEO NCHINI


 Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu, Mhe. Benjamini Wiliam Mkapa akiwahutubia Wajumbe waliohudhuria mkutano wa Jiolojia uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam.
 Baadhi wa Wajumbe waliohudhuria mkutano wa Jiolojia wakifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na mgeni rasmi katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Wanasayansi Vijana wakifuatilia mada wakati wa mkutano wa tatu wa Wanasayansi Vijana Duniani wenye lengo la kuhakikisha kuwa vijana wanashiriki vyema katika rasilimali za duniani kwa ajili ya maendeleo na ukuaji wa uchumi thabiti. (Picha na Makala na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM)
 ========  ======  ========
Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.
 
Vijana nchini hawanabudi kupenda kujifunza masomo ya Sayansi na teknolojia ili waweze kupata ujuzi na mitazamo katika sekta ya gesi ambayo inakuwa kwa kasi kubwa hapa nchini na Duniani kwa ujumla.
 
Kiukweli sayansi na teknolojia inasadikiwa kuwa mihimili mikubwa ya sasa katika kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali kwani mambo mengi yenye kuhitaji haraka hutegemea sayansi na teknolojia kwa kiasi kikubwa.
 
Licha ya kuwepo kwa changamoto zinazozikabili baadhi ya nchi nyingi za Afrika katika kupata maendeleo ikiwa ni pamoja na kutowekeza katika sayansi na teknolojia, hali inayopelekea baadhi ya nchi nyingi kukosa Wataalam wa kutosha katika mambo ya sayansi na teknolojia, hivyo nchi za Afrika zinahitaji kujikwamua na changamoto hiyo kwa kuhakikisha kuwa zinawekeza katika sayansi ili kubadilisha uchumi wa Afrika.
 
Sayansi na teknolojia hapa duniani huleta maendeleo makubwa hivyo Vijana wanatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma katika mambo ya sayansi na teknolojia ili kuweza kuleta uchumi endelevu.
 
Sambamba na hilo, katika Kongamano liloandaliwa hivi karibuni na Wizara ya Nishati na Madini nchini Tanzania ambao ulifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt Mohammed Gharib Bilal ambao ulikuwa ni mkutano wa tatu wa Wanasayansi Vijana Duniani wenye lengo la kuhakikisha kuwa vijana wanashiriki vyema katika rasilimali za duniani kwa ajili ya maendeleo na ukuaji wa uchumi thabiti, Wakala wa Jiolojia nchini, Profesa Mruma alisema kuwa Mkutano huo una lengo la kurithisha taaluma ya jiolojia inayohusisha madini, rasilimali, gesi na mafuta kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
 
Kongamano hilo la Vijana liliwakutanisha vijana toka nchi zaidi ya 42 zikiwemo baadhi ya nchi za Afrika Tanzania ikiwemo na ambaye ndiyo alikuwa mwenyeji wa Kongamano hilo.
 
Katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na madini, Mhe. Masele alisema kuwa Serikali ya Tanzania imewekeza nguvu zake kwa katika kuendeleza sayansi ya mambo ya gesi na mafuta pamoja na afya kwa kuanzisha Vyuo mbalimbali na kuwapeleka baadhi ya Watanzania kwenda kusoma nje ya nchi ili waweze kupata ujuzi na kuwa wataalam na wakaguzi katika sekta ya gesi, mafuta na afya kwa lengo la kuja kuisaidia nchi.
 
Aidha, Mhe. Masele alisisitiza kuwa wajibu wa Serikali kuamua kwa makusudi kusomesha vijana katika nchi mbalimbali ni kuwawezesha vijana waweze kupata elimu juu ya sayansi na teknolojia hasa katika masuala ya gesi ili kupata wataalam na wakaguzi wa kutosha nchini ambao watalisaidia taifa kuinua uchumi wake.
 
“Hivi sasa Serikali imeanzisha vyuo mbalimbali nchini, programu mbalimbali za mafunzo kwa watanzania, imetoa ufadhili wa masomo kwa watanzania na imedhamini makongamano ya vijana ili wapate fursa ya kujiendeleza’, alisema Masele.
 
Mhe. Masele pia aliyataka Makampuni ambayo ndiyo yalikuwa Wadhamini wa kongamano hilo kuendelea kuwekeza nchini pamoja na kuendelea kulipa kodi ili serikali iweze kukusanya mapato na wananchi wapate kunufaika na mapato hayo.
 
Halikadharika, katika mkutano mwingine uliohusiana na mambo ya Jiolojia uliowakutanisha Wataalam mbalimbali wa mambo ya jiolojia ulimwenguni jijini Dar es Salaam, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamini William Mkapa ambaye alikuwa ndiye mgeni rasmi wa mkutano huo aliziasa jamii hizo za Kiafrika kuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na mambo ya sayansi na teknolojia ili ziweze kujikwamua kimaendeleo.
 
Mhe. Mkapa alisema kuwa jamii nyingi za kiafrika hazijaelewa mchango mkubwa wa sayansi na teknolojia katika kuleta maendeleo licha ya ukweli wa kwamba maendeleo daima yanatokana na rasilimaliwatu iliyopo juu ya ardhi na chini ya ardhi, mchango wake huo hauthaminiwi na wengi lakini wanaoweza kufanya hivyo ni Wanasayansi.
 
“Serikali licha ya kudhamini mafunzo mbalimbali na masomo kwa vijana nje na ndani ya nchi, fedha za kutosha bado zinahitajika katika kuhakikisha kuwa kazi hiyo inakuwa endelevu”, alisema Mhe. Mkapa.
 
Bila shaka kuna haja ya kizazi kilichopo na kijacho kurithishwa uelewa mzuri kuhusiana na mambo ya jiolojia ya jamii, jiolojia ya madini, mazingira na mabadiliko ya tabianchi, vyanzo vya nishati, matatizo yanayotokana na milipuko kama jiolojia na kuunganisha elimu ya Tehama na jiolojia kwani hii itawasaidia vijana wengi kuelimika vya kutosha kuhusiana na mambo ya jiolojia na pamoja na maendeleo kwa manufaa yao wenyewe.
 
Naye Mwenyekiti wa Mtandao huo kwa upande wa Tanzania Bw. Stephen Joseph Nyagonde alitaja kauli mbiu ya mkutano huo kuwa ni ”Kuhakikisha ushiriki wa vijana katika rasilimali za duniani kwa ajili ya maendeleo endelevu na ukuaji wa uchumi imara”.
 
Katika mikutano hii yote, wadau mbalimbali wakiwemo Wanasayansi Vijana walipata fursa ya kujadiliana kwa kina na kutoa mapendekezo ya kisayansi ya namna ya dunia inavyotakiwa kupiga hatua za kimaendeleo na kuboresha maisha ya wakazi.
 
Jamii nyingi za Kiafrika kiuhalisia hazina uelewa wa kutosha kuhusiana na mchango wa sayansi na teknolojia katika kuleta maendeleo nchini hali inayopelekea kuzorota kwa maendeleo ya nchi nyingi za Kiafrika.
 
Hivyo Wanasayansi ulimwenguni wanatakiwa kujenga utamaduni wa kukutana mara kwa mara na kujadili mambo yanayohusu Sayansi na teknolojia ili kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii hizo.
 
Endapo vijana nao wakichangamkia fursa mbalimbali za masomo yanayohusiana na mambo ya rasilimali zipatikanazo nchini mwao kama vile gesi asilia, mafuta na madini mengine wataweza kutatua kitendawili cha umasikini Barani Afrika na nchini mwao, hasa vijana wa kike kujenga utamaduni wa kujikita katika masomo ya sayansi ili waweze kuwa wabunifu na kujikwamua na maisha yao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad