WANA DIASPORA :KAAT WAJITAMBULISHA KWA MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


18 Aug 2014

WANA DIASPORA :KAAT WAJITAMBULISHA KWA MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (Kushoto) akiwakaribisha viongozi wa KAAT walipokwenda kumtembelea na kufanya nae mazungumzo nyumbani kwake. Katikati ni Rais Mpya wa KAAT, Bw. Stephen Katemba na Kulia ni Bw. Bukheti Juma ambaye ni Makamu wa Rais, KAAT (Zanzibar).
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (Kushoto) akifurahia jambo na viongozi wa KAAT, Bw. Stephen Katemba (Katikati) na Bw. Bukheti Juma (Kulia). Viongozi hao walipokwenda kumtembelea na kufanya nae mazungumzo nyumbani kwake mjini Zanzibar.
 Rais Mpya wa KAAT, Bw. Stephen Katemba (Katikati) akiongea na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (Kushoto) wakati walipokwenda kumtembelea na kufanya nae mazungumzo nyumbani kwake mjini Zanzibar. Kulia ni Bw. Bukheti Juma ambaye ni Makamu wa Rais, KAAT (Zanzibar).
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (Kushoto) akitilia mkazo umuhimu wa jamii kusaidia wazee wasiojiweza, wakati alipofanya mazungumzo na viongozi wa KAAT, Bw. Stephen Katemba (Katikati) na Bw. Bukheti Juma (Kulia). Viongozi hao walipokwenda kumtembelea na kufanya nae mazungumzo nyumbani kwake mjini Zanzibar.
Baadhi ya wanachama wa KAAT wakiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (Katikati).
*********************************
*Yadhamiria kuwasaidia wazee wasiojiweza
Na Saidi Mkabakuli
Uongozi mpya wa Jumuiya ya Watanzania waliosoma Korea (KAAT) wamekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi mjini Zanzibar na kutoa ombi rasmi la kuharakishwa kwa kufunguliwa kwa Ofisi za Kibalozi nchini Korea Kusini.
Wakizungumza mara baada ya kukaribishwa na Mhe. Balozi Iddi, Rais wa KAAT, Bw. Stephen Katemba alitoa wito kwa Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kufikiria kufungua ubalozi nchi Korea Kusini kwa kuzingatia umuhimu wa nchi hiyo katika uchumi wa Tanzania.
Bw. Katemba alisema kuwa kufunguliwa kwa ubalozi huo kutaongeza chachu ya mahusiano ya kibiashara na kindugu baina ya nchi hizi mbili zenye urafiki wa hali ya juu.
“Tunakosa fursa nyingi za kufanya biashara na Korea Kusini kwani wengi wa wafanyabiashara wa Korea Kusini tuliokutana nao nchini humo wanaona usumbufu kufuata huduma za kibalozi nje ya nchi yao,” alisema Bw. Katemba.
Kwa mujibu wa Bw. Katemba, Korea Kusini ina soko kubwa kwa bidhaa za Tanzania ikiwemo bidhaa za vyakula na matunda, pia Tanzania ina fursa kubwa ya kupata ujuzi hasa kwenye eneo la kiteknolojia na ujenzi.
Kwa upande wake Balozi Iddi, alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu na fursa zilizopo nchini Korea, na kuahidi kulifanyia kazi ombi hilo.
Wakati huo huo, katika kutimiza wajibu wa kusaidia wazee na watu wasiojiweza, uongozi mpya wa Jumuiya ya Watanzania waliosoma Korea (KAAT) upo mbioni kufanyia matengenezo nyumba za kukaa wazee za Sebuleni, mjini Zanzibar.
Akizungumzia mpango huo, Makamu wa Rais, KAAT (Zanzibar), Bw. Bukheti Juma amesema “KAAT inatambua mchango mkubwa wa wazee nchini Tanzania, hivyo katika kuhakikisha wanaishi katika mazingira safi na salama, KAAT tutafanyia matengenezo baadhi ya majengo yaliyo kwenye hali mbaya kituoni hapo,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Juma zoezi hilo linatarajiwa kufanywa katikati ya mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad