UMEME WETU : MITAMBO YA IPTL YAANZA KUZALISHA MEGAWATI 100 - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


4 Jul 2014

UMEME WETU : MITAMBO YA IPTL YAANZA KUZALISHA MEGAWATI 100

·        IPTL kuongeza uzalishaji hadi megawati 200 mwakani
·        Kushusha zaidi bei ya umeme hadi chini ya senti nane za marekani

Na Mwandishi Wetu

UZALISHAJI umeme katika kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) umefikia megawati 100 ambayo ni kiwango cha juu cha uwezo wa mitambo yake, kiwango kilichofikiwa tarehe 15 Juni, huku uongozi wa kampuni hiyo wakiahidi kutekeleza mipango mkakati yake yote ya utanuzi kwa awamu.  

Hayo yalibainishwa na Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL/Pan African Power Solutions (PAP), Bw. Joseph Makandege alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa ahadi za viongozi wa kampuni hiyo kwa umma na mamlaka za serikali tangu PAP iliponunua IPTL.

“Tarehe 15 mwezi wa sita mwaka huu, mitambo ya IPTL iliyopo eneo la Tegeta, ilianza kuzalisha megawati 100 za umeme, ambazo ndiyo uwezo wa mitambo hiyo. Hii ni moja ya ahadi zilizotolewa na uongozi wa PAP wakati wa ununuzi wa mitambo ya IPTL,” alisema Makandege .

Alisema IPTL ambayo inamilikiwa na kampuni ya kizalendo ya Pan African Power Solutions Tanzania Limited, inaendelea na jitihada zake za kutimiza ahadi yake ya kuwapunguzia wateja/walaji adha ya gharama ya umeme Tanzania.

“Tumepanga kuzalisha megawati 200 kwa kutumia mitambo inayoendeshwa kwa kutumia gesi ifikapo Desemba 2015, ambapo tutauza umeme wake kwa chini ya dola nane za kimarekani, ikiwa ni awamu ya kwanza ya utanuzi. Katika awamu ya pili ya utanuzi, tumepanga kuzalisha megawati 300 ifikapo Desemba 2017.

“Tuliahidi kupunguza bei zetu, kuongeza uzalishaji mpaka kufikia kiwango cha juu cha mitambo yetu na kuendelea kutanua mitambo yetu ili kuweza kuzalisha megawati 500 baada ya kibadilisha mfumo yake iweze kutumia gesi. Hatua hii itawezesha IPTL kupunguza zaidi bei zake hadi kufikia kati ya senti sita na nane za kimarekani kwa kila unit. Ndani ya kipindi hiki kifupi, tumeweza kudhihirisha uwezo wetu wa kutimiza ahadi zetu zote,” alisema Bw. Makandege.

Alisema kuwa ingawa bei ya umeme kwa kampuni yao kwa sasa zimesimama kati ya senti 26 na 30 za kimarekani kwa unit, wateja wajiandae kuanza kufurahia bei zilizopungufu hivi karibuni baada ya kampuni kubadilisha mashine zake na kuanza kutumia gesi kuzalishia umeme.
Kwa sasa, wazalishaji umeme wengine katika soko wanatoza kati ya senti 38 na 60 za kimarekani kwa kila unit. Bw. Makandege aliongeza kuwa mitambo yote ya IPTL imefanyiwa marekebisho makubwa baada ya kufanya kazi kwa zaidi ya miaka karibia sita bila matengenezo.

Alisema uongozi mpya unaendelea na uboreshaji wa barabara zote za ndani ya kiwanda kwa kiwango cha lami, pamoja na marekebisho mengine ambayo yatabadilisha muonekano mzima wa IPTL.
“Tukiwa kama kampuni ya ufuaji umeme, tunatambua faida za kiuchumi za kutumia umeme wa bei rahisi kwa mteja na kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi kwa ujumla.
“Hii ndiyo maana tunafanyakazi kwa jitihada zote ili kuweza kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha umeme wa bei rahisi ambao utasaidia kuboresha uchumi wa nchi hii,” alisema Makandege.

Bw. Makandege alisema kuwa kampuni yake imeamua kutafuta njia bora za uzalishaji wa umeme wenye gharama nafuu, ikilinganishwa na washindani wengine katika soko, sababu inaamini uwepo wake utasaidia katika kuboresha maisha ya wateja wake na jamii inayoizunguka.


“Uongozi mpya wa IPTL/PAP unaamini katika kuwapatia wateja wake matokeo yaliyo chanya. Njia pekee ya kufanya hivyo ni kutoa
bidhaa/huduma zilizo na gharama nafuu kwa wateja, licha ya utofauti waliokuwa nao katika viwango vyao vya mapato,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad