MAKALA : MAKALA MAALUM YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


16 Jul 2014

MAKALA : MAKALA MAALUM YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Joyce Mapunjo akizungumza na moja ya chombo cha habari wakati wa maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ambaye ni Msemaji wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Vedastina Justinian akimsikilia mwananchi aliyetembelea banda la wizara hiyo kwenye maadhimisho ya wiki ya Utumishi ya Umma yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.Picha na Hussein Makame-MAELEZO.
============  =========
Hussein Makame-MAELEZO.

WAKATI Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki walipotia saini Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1999, kila upande ulilenga maslahi ya kiuchumi na maendeleo kwa nchi na wananchi wake katika nyanja mbalimbali. Lakini ni ukweli ulio wazi kwamba mafanikio ya nchi katika jumuiya hiyo hutegemea kwa kiasi kikubwa na ushiriki wa wananchi katika hatua za mtanagamano huo kwani wao ndio walengwa wakuu katika mchakato huo.

Ni miaka 14 imepita tangu wakuu wa nchi za Afrika Mashariki waliposaini Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na miaka 9 tangu kuanza kwa utekelezaji wa hatua ya kwanza ya mtangamano wa jumuiya hiyo. Pamoja na mafanikio ambayo Tanzania imeanza kuyapata kutokana na hatua mbalimbali za mtangamano wa jumuiya hiyo, inaelezwa kuwa bado mwitikio wa wananchi katika kuchangamkia fursa zilizopo uko chini.

Msemaji wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Vedastina Justinian anasema baada ya maandalizi ya miaka sita, nchi tano wanachama wa jumuiya hiyo zilianza kutekeleza rasmi hatua ya Umoja wa Forodha mwaka 2005.
 
Katika hatua hiyo nchi ziliwekeana muda wa kipindi cha miaka mitano za utekelezaji ambapo nchi ya Kenya ilianza kuingiza bidhaa katika nchi ya Tanzania na Uganda kwa kutozwa ushuru ambao ulikuwa unapungua mwaka hadi mwaka. “Sisi Tanzania na Uganda tulikuwa tunapeleka bidhaa zetu Kenya bure bila ya kutozwa ushuru kwa sababu Kenya ilikuwa imeendelea kiviwanda, kwa hiyo ilitupa muda na sisi tuwe tumejiandaa vizuri” anasema Vedastina.

Anafafanua kuwa mpaka mwaka 2010 Kenya ilianza kuingiza bidhaa katika nchi hizo mbili bila ya kutozwa ushuru na baadaye nchi wananchama zilianza hatua ya pili ya mtangamano huo ambayo ni Soko la Pamoja. Soko la pamoja lilianza kutekelezwa kuanzia Julai mwaka 2010 na lilijumuisha soko huru la bidhaa, soko huru la mitaji, wananchi kuingia na kukaa katika nchi anayotaka ilimradi ana pasipoti pamoja na soko huru la ajira.

Vedastina anasema kuwa kila nchi ilianisha maeneo ambayo iliyafungua kwa mfano Tanzania ilifungua maeneo ya walimu wanaofundisha lugha za kigeni, maafisa ugani, madaktari, marubani na maeneo mengine ambayo yalikuwa yanaonekana kuwa na upungufu.

Anasema kwa sasa shirikisho hilo liko kwenye hatua ya Umoja wa Fedha ambao itifaki yake ilisainiwa Novemba mwaka 2013, muda wa miaka 10 uliwekwa kufanya maandalizi ya kutekeleza hatua hiyo.

“Maandalizi hayo ni kuweka uchumi wetu ukae vizuri tuwe na mfumuko wa bei angalau unayofikia asilimia 8 kila nchi, tuwe na bajeti zisiyotegemea misaada kwa nakisi za bajeti zetu zisizidi asilimia 3 ya Pato la Taifa” anafafanua Vedastina na kuongeza kuwa:

“Vile vile tuwe na akiba za fedha za kigeni ya kutosha ambayo tulijiwekea kuwa kila nchi iwe na akiba ya fedha za kigeni za kukutosheleza muda wa miezi minne na nusu, pia nchi tuwe tumejiwekea taasisi muhimu za utekelezaji wa umoja wa fedha kwa mfano benki kuu kuna taasisi ambazo zinatakiwa ziwepo.”.

Anasema baada ya miaka hiyo 10 nchi wanachama zitakaa chini kuangalia kama zimejiandaa vya kutosha kuanza utekelezaji wa matumuzi ya sarafu moja  na hatua hizo zitakapotekelezwa ipasavyo nchi zitaanza utekelezaji wa shirikisho la kisiasa.
Akizungumzia matarajio ya Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Vedastina anasema baada ya miaka 10 hatua inayofuata ni sarafu moja ambapo gharama za kufanya biashara zitapungua.

“Sasa hivi unapokwenda kufanya biashara nje ya Tanzania katika nchi za Jumuiya kwa mfano Kenya inabidi ubadilishe fedha kwenda shilingi ya Kenya au Franga za Burundi au Rwanda au uende kwenye fedha ya Uganda” anasema Vedastina.Anafafanua kuwa kwa sasa mtu anapobadilisha fedha kuna fedha anayokatwa  kwa sababu anayekubadilisha anataka faida, lakini ikifikia hatua ya umoja wa sarafu kutakuwa na fedha ya aina moja itakayotumia katika nchi zote za Jumuiya.

Akizungumzia mwitikio wa Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo, Vedastina anasema katika eneo la ajira Watanzania bado wanajiweka nyuma kwamba hawataki kuvuka mipaka kwenda kufanya kazi nchi nyingine.

“Katika eneo la ajira natoa wito tu kuwa Watanzania wachangamkie hizi fursa kwani,Watanzania bado wanajiweka nyuma kwamba hawataki kuvuka mipaka kwenda kufanya kazi sehemu nyingine, ni wachache ambao wameweza kuthubutu na wameweza kufauru kwenda katika nchi nyingine” anasema Vedastina.

Anawataka Watanzania wanapotafuta ajira wasiangalie tu kwa Tanzania na kusema wamekosa ajira badala yake waangalie soko la Afrika Mashariki kwani ajira zipo na pia kwa bidhaa kuna soko la watu milioni 140 katika jumuiya hiyo.

“Wakati mtu anatafuta ajira aingie kwenye mtandao aangalie hata kwa wenzetu wanataka watu wa aina gani kama ana sifa zinazohitajika aombe, anaweza akaajiriwa Kenya, Uganda, Rwanda na hata Burundi” anasisitiza Vedastina. Anasema kuwa katika kipindi hiki ambapo wanafunzi wanahitimu katika vyuo vikuu waanze kuchngamkia soko la ajira la Afrika Mashariki.

Kwa upande wa wafanyabiashara, Vedastina anasema bado wako nyuma na kutoa mfano kuwa wakulima wanasubiri wafanyabiashara watoke nchi jirani waende wakachukue bidhaa mashambani huku wao hawataki kuvuka mipaka.

Anatoa wito kwamba Watanzania wachangamkie fursa hizo na watoke nje ilimradi wawe na pasipoti, bidhaa zao zinakidhi ubora na viwango na zina uasilia wa bidhaa. “Kama umezalisha bidhaa zako Tanzania tafuta cheti cha uasilia wa bidhaa ambacho kinapatikana TRA auTCCIA uweze kukidhi vigezo vya kuvuka nje ya Tanzania na kuweza kuangalia soko kubwa kwani sasa hivi tunategemea tutaingiza bidhaa hadi Sudan Kusini” anasema Vedastina.

Anasema Watanzania wana bidhaa nyingi za kilimo na bidhaa zao zina ubora huku akitolea mfano maonesho ya Juakali Nguvukazi, ambapo watu wanakimbilia bidhaa za Tanzania ikiwemo asali, batiki, vinyago,   mchele na nyingine. Kutokana na hali hiyo, Vedastina anawataka Watanzania waache woga wa kwenda nchi za Afrika Mashariki kwani wafanyabiashara wa nchi nyingine  wanachangamkia masoko bila kujali mipaka ya nchi yao.

Anafafanua kuwa “unajua sasa hivi wafanyabiashara kutoka nje labda Kenya, anakuja ananunua shamba zima anasema nitavuna mwenyewe, nakulipa tu shamba zima nitavuna mwenyewe nitapeleka nje.

Kwa nini ukubali mtu anunue shamba ajivunie mwenyewe, vuna mwenyewe wauzie wafanyabiashara wavushe mipakani au vuka mwenyewe ukauze nje uvumbuke macho.

Bila kuangalia wenzetu wanafanya  nini utakaa tu unalaliwa bei unaouza kwa bei ya chini wenzako wanauza kwa bei ya juu sana, kwa hiyo natoa wito kwamba Watanzania waaamke wasisubiri watu kutoka nje kingia hadi mashambani”.

Anasema iwapo Watanzania watabaki hivyo walivyo matokeo yake hawatapata faida kubwa ya mazao yao na pia unakosa uzoefu wa kujifunza kwa kuangalia wafanyabiashara wa nchi nyingine wanafanya nini kuboresha biashara zao.

“Kwa mfano Tanzania, wafanyabiashara au wakulima hawajajua hata jinsi ya kufungasha vizuri hizi bidhaa utakuta wenyewe ufungashaji wao ni hafifu sana, lakini unapotoka nje akaangalia wenzetu wanafanya nini mtu anajifunza anakuja na yeye anafanya vizuri” anafafanua Vedastina.
Ili kuhakikisha Watanzania hawaachwi nyuma katika mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Vedastina anawataka Watanzania wajielimishe kuhusu mambo ya Jumuiya hiyo kwani bado wako nyuma na hawana uelewa wa kutosha.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad