WANA HABARI KAZI KWETU :VYOMBO VYA HABARI VYAASWA KUTOA KIPAUMBELE KWA HABARI ZINAZOJENGA JAMII - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


10 Apr 2014

WANA HABARI KAZI KWETU :VYOMBO VYA HABARI VYAASWA KUTOA KIPAUMBELE KWA HABARI ZINAZOJENGA JAMII


Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene (kushoto) akizungumza na wahariri wa Gazeti la Jamhuri Bw. Deodatus Balile, Muhariri Mtendaji (katikati) na Bw. Manyerere Jackton , Naibu Muhariri Mtendaji (kulia) alipotembelea Ofisi za gazeti hilo mtaa wa Samora jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa watendaji wa Idara ya Habari kuvitembelea vyombo vya habari kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kutatua changamoto zinazoikabili tasnia ya Habari nchini.
Muhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri Bw. Deodatus Balile (kulia) akizungumza jambo na viongozi wa Idara ya Habari waliotembelea ofisi za gazeti hilo jijini Dar es salaam. Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari-Usajili wa Magazeti Bw. Raphael Hokororo,Afisa habari wa Idara ya Habari Bi. Jovina Bujulu na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji wa Serikali Bw. Assah Mwambene.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari-Usajili wa Magazeti Bw. Raphael Hokororo akifafanua utaratibu wa utoaji wa vitambulisho kwa waandishi wa habari (Press Card) na namna Idara ya Habari inavyozingatia kigezo cha elimu cha taaluma ya Habari katika kutoa vitambulisho kwa waandishi wa Habari (Press Card) hapa nchini.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Vyombo vya habari nchini vimeaswa kutoa kipaumbele kwa habari zinazojenga jamii kwa kuihamasisha kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo, kudumisha uzalendo  na kuepuka habari zinazoweza kusababisha mgawanyiko  na chuki katika jamii.
Wito huo umetolewa jijini Dar es salaam na Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene  alipotembelea ofisi za gazeti la Jamhuri zilizoko mtaa wa Samora  jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa Idara hiyo kuvitembelea vyombo mbalimbali vya habari nchini kwa lengo la kukuza ushirikiano na kujadili changamoto mbalimbali za tasnia ya habari hapa nchini.
Amesema kuwa serikali inaheshimu mchango mkubwa unaotolewa na tasnia ya habari  hapa nchini na kuongeza kuwa  habari ni moja ya sekta inayokuwa kwa kasi, yenye uwekezaji mkubwa na inayoajiri watu wengi hapa nchini.
“Sisi kama serikali ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tasnia ya habari hapa nchini inapiga hatua kutokana na umuhimu wa pekee ilio nao katika jamii,hivyo utaratibu huu wa kuvitembelea vyombo vya habari ni wa kawaida ikiwa ni sehemu ya kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kutatua changamoto mbalimbali zilizopo” .
Akizungumza na wahariri wa gazeti hilo Bw. Mwambene amesema kuwa vyombo vya habari hapa nchini vinao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa vinatoa kipaumbele kwa habari  zinazogusa masuala mbalimbali ya wananchi na kuibua changamoto mbalimbali zilizo katika jamii kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ustawi wa taifa.
Amelipongeza gazeti hilo kwa kuendelea kuzingatia weledi katika utoaji wa habari zake kwa kuweka msisitizo wa utoaji wa habari zinazohamasisha uzalendo.
“Kwanza nawapongeza kwa kazi mnayoendelea kuifanya  hasa moyo wa uzalendo mliouonyesha mlipokuwa mkiandika habari na kuchapisha makala kuhusu uhusiano wa Tanzania na nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia katika masuala mbalimbali yenye kuhamasisha uzalendo nchini”
Ameeleza kuwa  hivi sasa taifa la Tanzania liko katika mchakato wa masuala makubwa yanayogusa maisha ya watu na maendeleo yao  yakiwemo ya Uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka ujao  na zoezi linaloendelea  la kupata katiba mpya  na kufafanua kuwa katika hilo vyombo vya habari vina wajibu wa kuhamasisha umoja wa kitaifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari – Usajili wa Magazeti Bw. Raphael Hokororo amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa taaluma ya habari inaendelea kulindwa hapa nchini  na waandishi wa habari wanafanya kazi zao bila vikwazo idara ya Habari  imekuwa ikitoa vitambulisho vya waandishi wa habari (Press Card) kwa waandishi wenye sifa na taaluma ya habari.
Amesema utoaji wa vitambulisho kwa waandishi wa habari umesaidia kudhibiti uwepo wa waandishi wasio na sifa katika shughuli mbalimbali za serikali ikiwemo mkutano wa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
“Katika hili tumeweka msisitizo wa matumizi ya vitambulisho hivi na tumeanza na Bunge maalum la Katiba waandishi wote wanaoandika habari za bunge la katiba tumewapatia vitambulisho” Amesema Bw. Hokororo.
Kwa upande wake Muhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri Bw. Deodatus Balile amewapongeza viongozi hao wa Idara ya Habari wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara hiyo Bw. Assah Mwambene kufuatia utaratibu huo wa kuvitembelea vyombo vya habari na kuongeza kuwa  unaongeza ushirikiano baina ya vyombo vya habari na 
serikali.
Kuhusu mchakato wa kupata katiba mpya  na uchaguzi mkuu ujao Bw. Balile ameeleza  kuwa  gazeti la Jamhuri linaendelea kutoa kipaumbele kwa habari zenye maslahi kwa taifa na pia habari za vyama vya siasa vyenye kujenga hoja kwa wananchi.
Aidha amesema kuwa wao kama chombo cha habari makini wataendelea kuihabarisha jamii kwa kuzingatia maadili, uzalendo na kukemea vitendo viovu vinavyorudisha nyuma maendeleo ya taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad