WANAWAKE WAANDISHI WACHANGAMKIE FURSA : WAANDISHI WANAWAKE WANAFANYA KAZI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU-UTAFITI - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


12 Mar 2014

WANAWAKE WAANDISHI WACHANGAMKIE FURSA : WAANDISHI WANAWAKE WANAFANYA KAZI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU-UTAFITI

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova, ( kati kati) akizungumza wakati wa majadiliano kuhusu Teknolojia ya habari na mawasiliano na mchango wa vyombo huru vya habari katika kuwawezesha wanawake na watoto wa kike, katika majadiliano hayo, wazungumzaji waliokaa meza kuu ambao ni kutoka kushoto, Bi. Elisa Munoz, Mkurugenzi Mtendaji wa IWMF, Muwakilishi wa Kudumu wa Austria Balozi Martin Sjdik, Bw. Peter Launsky-Tieffenthal Katibu Mkuu Msaidizi na mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa , Anne Bennett, Mkurugenzi Mtendaji wa Hirondelle ( USA) na Pamela S. Fall, anayeripoti katika kituo cha CBS na Rais wa chama cha Waadishi wa habari Umoja wa Mataifa walijadili kwa kina umuhimu wa teknolojia ya habari na mawasiliano kama nyezo muhimu ya uwezeshaji wa wanawake na watoto wa kike, lakini pia kama nyezo muhimu katika kuwapatia habari na taarifa mbalimbali, habari zinazoandaliwa na vyombo huru na ambavyo waandishi wake wenyewe na weledi wa matumizi ya ICT.
sehemu ya washiri wa majadiliano kuhusu ICT ambayo yaliandaliwa kwa pamoja na UNESCO na Uwakilishi wa Kudumu wa Austria na kufanyika sambamba na mkutano wa 58 wa Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake. katika majadiliano hayo, Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya International Women's Media Foundation, (IWMF mwenye suti nyekundu, alitoa taarifa kuhusu uzinduzi utakaofanywa wa ripoti ya utafiti kuhusu mazingira hatarishi wanayofanyia kazi waandishi wa habari wanawake. Ripoti hiyo yenye kurasa 40 inahusu utafiti uliofanywa kwa kuwashirikisha waandishi wa habari wanawake 1,000 kutoka duniani kote.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bibi. Anna T. Maembe, akifutilia majadiliano ambayo yameingia siku ya pili ya ajenda kuu ya Mkutano wa 58 wa Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake, ajenda hiyo ni mafanikio na changamoto za utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia, ( MDGs) kwa wanawake na watoto wa kike. Mkutano wa 58 wa CSW ulifunguliwa siku ya jumatatu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.

Na Mwandishi Maalum

Utafiti wa pamoja uliofanywa na Taasisi mbili za kimataifa, zijulikanazo kama The International News Safety ( INSI) na The International Women’s Media Foundation ( IWMF) umebainisha kwamba, waandishi wa habari wanawake, wanakumbana na vurugu za aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na unyanyaswaji wa kijinsia.

Ripoti ya utafiti huo yenye kichwa kisemacho “ vurugu na unyanyasaji dhidi ya wanawake katika vyombo vya habari; picha halisi. inaeleza kwamba sehemu kubwa ya udhalilishaji huo unafanyika katika vyombo vya habari ambako wanafanyia kazi.

Taarifa ya uzinduzi wa ripoti hiyo yenye kurasa 40 imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa IWMF Bi. Elisa Lees Munoz, wakati wa majadiliano ya mada kuhusu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na mchango wa vyombo huru vya habari katika uwezeshwaji wa wanawake na watoto wa kike.

Majadiliano hayo yalifanyika siku ya jumanne, sambamba na Mkutano wa 58 wa Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake ( CSW) unaoendelea hapa Umoja wa Mataifa na yaliandaliwa kwa pamoja kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni ( UNESCO ) na Uwakilishi wa Kudumu wa Austria katika Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa Bi, Munoz ripoti hiyo ni matokeo ya utafiti uliofanywa taasisi hizo mbili kuanzia mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu. Kwa kuwahoji waandishi wa habari wanawake 1,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Bi Munoz anasema utafiti huo umefanyika kwa ufadhili wa UNESCO na Austria na unaotoa picha ya kwanza ya aina yake na ya kina kuhusu hatari inayowakabili wanawake wengi wanaofanya kazi katika vyombo vya habari duniani kote.

Akielezea matokeo zaidi ya utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa IWMF anasema, karibu theluthi mbili ya wahojiwa walikiri kupokea aina moja ama nyingine ya vitisho kutokana na kazi yao, udhalilishwaji wa kijinsia, vikiwamo pia vitendo ya kukaripiwa au kutukanwa pasipo sababu au hata kuitwa majina ya ajabu ajabu.

Aidha kwa mujibu wa utafiti huo wengi wa wahojiwa hao walieleza kwamba hawakuwahi kutoa taarifa mahali popote dhidi ya ukatili na udhalilishwaji wanaofanyiwa licha ya kwamba waliathirika kisaikolojia.

“ Tunapozungumzia usalama wa waandishi wa habari, mara nyingi tunafikiri ni usalama wa waandishi wanaoripoti katika maeneo hatari kama vile kwenye vita, migogoro au majanga asilia. Lakini ni kwa namna gani tunafikiri kwamba hata vyumba vya habari vinaweza kuwa mahali hatari” anaeleza Munoz Na kuongeza Utafiti huu unaonyesha kwamba waandishi wanawake mara nyingi wamo katika mazingira hatarishi katika ofisi zao wenyewe wanakofanyia kazi, wanashambuliwa na wafanyakazi wenzao, na wanaangushwa na watu ambao wanapashwa kuwaamini na kuwasaidia.

Utafiti huo unaonyesha pia udhalilishwaji wa waandishi wanawake haufanywi na wakuu wao wa kazi peke yao au wafanyakazi wenzao, bali hata na watu wa kada mbalimbali wakiwamo wale ambao waandishi hao hutumwa kwenda kuwafanyia mahojiano au kutafuta habari .

Wazungumzaji wengine katika majadiliano hayo walikuwa ni Mkrugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova, Bw. Peter Launsky-Tieffenthal ambaye ni Katibu Mkuu Msaidizi na mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa , Muwakilishi wa kudumu wa Austria, Balozi Martin Sjdik, Anne Bennett, Mkurugenzi Mtendaji wa Hirondelle ( USA) na Pamela S. Fall, anayeripoti katika kituo cha CBS na Rais wa chama cha Waadishi wa habari Umoja wa Mataifa

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad