MABORESHO YA UWANJA NDEGE : MWANRI ;UWANJA WA NDEGE WA MTWARA KUBORESHWA - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


20 Mar 2014

MABORESHO YA UWANJA NDEGE : MWANRI ;UWANJA WA NDEGE WA MTWARA KUBORESHWA

 Mmoja wa viongozi wa Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (aliyevaa fulana nyeusi) akihoji uimara wa sehemu ya kutulia ndege wakati walipofanya ziara ya kujionea maendeleo ya Uwanja wa Ndege wa Mtwara.
 Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Mtwara kwa ajili ya kujionea maendeleo ya uwanja huo.
Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara, Mhandisi Mugasa Mlondo akitoa maelezo juu uimara na ubora wa uwanja wake wakati Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipofanya ziara kwa ajili ya kujionea maendeleo ya uwanja huo.

                           <<<<<<<<<<<>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>
Na Saidi Mkabakuli
Katika kukabiliana na kasi ya maendeleo ya ukuaji wa uwekezaji katika maeneo ya viwanda vikubwa na biashara za huduma mkoani Mtwara, Serikali imesema kuwa kuna haja ya kuuimarisha Uwanja wa Ndege wa Mtwara ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa watumiaji wa uwanja huo, hasa kufuatia kugundulika kwa gesi mkoani humo,
Hayo yamebainishwa mmoja wa viongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri  wakati ilipofanya ziara kwa ajili ya kujionea maendeleo ya uwanja wa huo.
Bibi Mwanri alisema kuwa Serikali inaendelea kufanya tathmini na mikakati mbalimbali itakayopelekea kuuimarisha uwanja wa ndege wa Mtwara ili kuweza kuhudumia uwekezaji mkubwa unaofanywa na makampuni mbali mbali ya ndani na nje ya nchi mkoani humo. Aliongeza:
“Tathmini ya awali inaonesha kuwa miradi mingi ipo mkoani Mtwara kufuatia kugundulika kwa gesi hivyo kuna haja ya dhati ya kuuimarisha uwanja wa ndege wa Mtwara kwa lengo la kutoa huduma za uhakika wakati huu wa mfumuko wa kiuchumi mkoani Mtwara,” alisema Bibi Mwanri.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Naibu Katibu Mtendaji (Uchumi Jumla), Prof. Longinus Rutasitara ambaye alikuwa kiongozi mwenza wa ukaguzi, alisema kuwa kuna haja ya dhati ya kuwekeza katika uwanja huo ili kukabiliana na kasi ya maendeleo ya mkoa wa Mtwara kufuatia wawekezaji wengi kuendelea kumiminika na kuwekeza mkoani humo.
“Uwanja wa ndege wa Mtwara una fursa za nyingi za kuhudumia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, hakika ni lango la biashara hasa kipindi hiki cha uchumi wa gesi mkoani Mtwara, hivyo uendelezaji wa uwanja huu ni jambo lisilo epukika,” alisema Prof. Rutasitara.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16),  Miundombinu ni kipaumbele cha kwanza, hasa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya nishati, usafirishaji (bandari, reli, barabara na usafiri wa anga), maji (safi, taka na ya uzalishaji) na TEHAMA.
Serikali imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 -2015/16) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo kuu la Mpango huu ni kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka misingi ya ukuaji mpana wa uchumi na unaolenga watu walio masikini zaidi. Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha katika mfumo mmoja wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa utekelezaji na kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi ya maendeleo kitaifa.
Lengo la Dira ni  kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad